Tofuati kati ya Myahudi, Mwisraeli na Muebrania ni ipi?

by Admin | 19 December 2019 08:46 pm12

Tofuati kati ya Myahudi, Mwisraeli na Muebrania ni ipi?


Haya ni maneno matatu tofauti lakini kiuhalisia yanangumzia kitu kimoja..Ni sawa na useme, mtanzania, mtanganyika, na mswahili..Ni yule yule isipokuwa inategemea unamzungumzia katika nyanja ipi.

Ndivyo ilivyo kwa taifa la Israeli. Waebrania chimbuko lake ni Ibrahimu na kwa mara ya kwanza jina hilo linaonekana katika kitabu cha (Mwanzo 14:13) likimtambulisha Ibrahimu,ambapo kwa wakati huo akiitwa Abramu. Na baadaye tena tunaona Yusufu naye akitajwa kwa jina hilo (Mwanzo 39:14, 17)…Hivyo ni jina lililokuwa linawatambulisha wazao wote wa Ibrahimu, Japo biblia haitoi tafsiri yoyote halisi ya jina hilo, wengine wanasema jina hilo lina maana ya aliyevuka kutoka ng’ambo.

Lakini Israeli, ni jina jipya la Yakobo mwana wa Isaka, mjukuu wa Ibrahimu. aliitwa vile kutokana na kwamba alishindana na malaika wa Bwana usiku kucha katika mueleka na kumshinda, hivyo jina lake likabadilishwa na kuitwa Israeli, hivyo Watoto wake wote, waliozaliwa baada yake waliitwa wana wa Israeli, hadi walipoingia utumwani Misri walijulikana kwa majina yote mawili yaani wana wa waisraeli au waebrania. Lakini jina Israeli lilipata nguvu Zaidi hadi wakiwa wanarudi na kukaa katika nchi yao ya Ahadi..walifahamika kama waisraeli.

Lakini miaka mingi ilipopita na Taifa la Israeli kugawanyika katika pande kuu mbili, kaskazini na kusini. Wale waliokuwa upande wa kaskazini walibakia na jina hilo la Israeli, lakini waliokuwa katika upande wa kusini waliitwa Wayudea..Kutoka katika Neno Yuda, kwasababu  taifa la Yuda ndilo lililokuwa linatawala upande wa kusini.

Lakini sasa mataifa yote yalipochukuliwa utumwani, yaani wale wa kaskazini  kupelekwa Ashuru, na wale wa kusini kupelekwa Babeli, kama tunavyosoma waliorudi kwa asilimia kubwa katika nchi yao ni wale wa kusini waliopelekwa Babeli mara baada ya ile miaka 70 kuisha iliyotabiriwa na Danieli.. Hivyo walivyorudi jina lao waliendelea  nao , wakijulikana kama wayudea, na ndio huko huko jina WAYAHUDI wayahudi lilipozaliwa..Maana ya wahayudi  ni watu wa ardhi ya Uyahudi,au  Yudea au Yuda. Hivyo watu wote wa taifa zima wakaitwa Wayahudi ikijumlisha hata na wale wachache waliorudi kutoka Ashuru  walijulikana wote kama  Wayahudi.

Lakini hiyo haikubadilisha asili yao kuitwa Waisraeli au Waebrania.

Kutokana na kuwa watu wa Yuda ndio Mungu aliwachagua kusimamia ujenzi wa hekalu na mji mtakatifu wa Mungu.Vilevile ndilo Kabila lililokuwa linatazamiwa kumleta Masihi wa ulimwengu duniani, Hivyo  hiyo ililifanya kabila hilo liwe lenye misingi ya kiimani Zaidi ya mengine. Hivyo mwisraeli yoyote aliyejiita myahudi kwa wakati ule alikuwa ni sharti awe anazingatia dini na desturi zote za kiyahudi.

Hata leo hii, Taifa la Israeli ni kubwa lenye watu wengi waliozaliwa kule, ambao kiuraia wanajulikana kama waisraeli wengine waislamu, wengine wakristo, wengine hawana dini, lakini pamoja na wingi wao, na utaifa wao, si wote walio wayahudi. Wayahudi ni wale ambao wanashikilia misingi ya torati na tamaduni zao za kidini.. wanashika sikukuu zote zilizoamuriwa kwenye torati, vilevile wanafanya ibada kama vile za agano la kale.

Hivyo kwa ufupi, Myahudi yeyote anaweza kuitwa mwisraeli, au mwebrania lakini Mwisraeli yeyote hawezi kuitwa myahudi. Kama vile mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania hata kama ni mzungu anaweza kuitwa mtanzania..Lakini sio kila mtu aliyezaliwa Tanzania anaweza akawa mswahili.. Mswahili ni jambo linaloendana na chimbuko la watanzania na lugha zao na desturi zao za asili.

Hiyo ndio Tofuati kati ya Myahudi, Mwisraeli na Muebrania

Ubarikiwe. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Je! wayahudi wote wataokolewa hata kama ni watenda dhambi, Kwasababu wote ni uzao wa Ibrahimu?

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

NG’OMBE MWEKUNDU ALIYEZALIWA ISRAELI, ANAFUNUA NINI?

CHUKIZO LA UHARIBIFU

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/19/tofuati-kati-ya-myahudi-mwisraeli-na-muebrania-ni-ipi/