MUNGU WETU, JINSI LILIVYO TUKUFU JINA LAKO DUNIANI MWOTE!

by Admin | 14 March 2020 08:46 pm03

Jambo mojawapo ambalo lilikuwa linamfanya Daudi asichoke kumsifu Mungu, ni vile alivyokuwa anajijengea mazoea ya kuutafakari ukuu wake kila mahali alipokuwepo.. Daudi alikuwa akizitazama mbingu sana, akiangalia jinsi nyota na mwezi vilivyowekwa angani na Mungu kwa namna ya ajabu na ya kushangaza..

Nakuambia kuna raha na changamko fulani la kipekee linaingia ndani yako, pale unapotenga muda wako mrefu kutafakari kazi za Mungu hususani vitu vya asili kama vile mbingu, na milima, na mabonde na mito na bahari….

Zaburi 8:1 “Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni; ….

3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha;”

Wakati mwingine tunajiuliza watu kama hao ambao hawakuwa na Darubini (Telescope) ya kuangalia magimba yaliyo mbali sana na dunia, lakini walimsifu Mungu kwa namna ile na kumfurahia, Je! Wangekuwepo katika wakati wetu huu, wangemsifu Mungu kwa jinsi gani?..Kwasababu ule wakati wao macho yao yaliishia kuona nyota tu za hapo angali, lakini sisi tunaishi katika kipindi cha teknolojia ya hali ya juu ndio tunaojua kuwa hata hizi nyota na hili jua, na huu mwezi, ni vitu vidogo sana ukilinganisha  na matrilioni na magimba mengine Mungu aliyoyaumba huko angani.. kwa ufupi ni kwamba kila kitu unachokiona angani, ikiwemo na hizo nyota zote, ni sawa na chembe moja ya mchanga katika michanga yote iliyopo baharini..Sasa embu jiulize  huyu ni Mungu wa namna gani, kaumba vitu vingapi tusivyovijua sisi kwa akili zetu?

Na sisi pia, ila sifa zetu ziwe na nguvu, tutoke nje tuutazame ukuu wa Mungu, tuutafakari sana, tutenge hata muda tuziangalie mbingu sana. Sio kila siku usiku na mchana tu tunakuwa bize tu na shughuli zetu, halafu jumapili ndio tunakwenda kumsifu Mungu kanisani..Ni lipi litakalotufanya tumsifu yeye kwa kumaanisha kabisa?..Wakati mwingine si tutakuwa tunafanya hivyo kinafki?…

Vile vile tutafakari jinsi alivyoviumba viumbe vyake mbali mbali, ili tujue kuwa haja bahatisha kutuumba na sisi jinsi tulivyo, Tutafakari  kwanini amuumbe mnyama mmoja na shingo ndefu, lakini mwingine amnyime lakini wote wakawa wanaishi bila shida yoyote, kwanini mwingine ampe miguu mingi (kama jongoo) lakini mwingine asimpe kabisa miguu (mfano nyoka), lakini  Yule asiye na miguu akawa na mbio, tena sana kuliko Yule mwenye miguu mingi…Kwanini mwingine amempa mbawa akawa anaruka na kupaa juu sana (Tai), na mwingine akampa  mbawa kama hizo hizo lakini hawezi kuruka(kuku) akionyesha kuwa kupewa mbawa sio kigezo cha wewe kuruka,

Tujiulize kwanini mwingine amepewa  meno lakini hawezi kula mifupa (ng’ombe) lakini mwingine hana meno na mwororo lakini chakula chake ni mifupa (konokono) kwanini mwingine hana mdomo unaofanana na binadama kama vile nyani, lakini mwingine mwenye mdomo wa ndege lakini hata haukaribiani na mtu, lakini anao uwezo wa kuiga lugha ya mwanadamu ukadhani ni mtu anazungumza kumbe ni ndege (kasuku)..Kuonyesha kuwa sio wepesi wa ulimi ndio unamfanya mtu azungumze, bali ni kujaliwa tu, bubu hana matatizo yoyote katika ulimi wake, lakini ni Mungu ndiye alimfanya awe vile. N.k n.k

Tukiyatafakari hayo na mengine mengi tutaona mambo ya Mungu jinsi yalivyo mengi..Na tutakuwa na amani na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyotuumba.. Vile vile hapo ndipo tutakapojua kuwa kumbe Mungu hategemei bidii zetu kutunyanyua au kutushusha, hategemei mpaka tupate elimu ndio atufikishe mahali Fulani, hatagemei mpaka tuwe na miguu miwili, au mikono miwili ndio atupigishe hatua nyingine…Bali ni kwa neema  zake tu..

Hivyo ni jukumu letu sote kumsifu Mungu wetu, daima, kwa mambo yake ya ajabu, na uumbaji wake. Na huko ndipo tutakapomwona katika maisha yetu.

ZABURI 150

1 Haleluya. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake.

2 Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.

3 Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;

4 Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;

5 Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.

6 Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya.

Bwana akubariki.

Tafadhali “Share” na kwa wengine.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JINSI MUNGU ANAVYOIPIGA NA KUIPONYA AFRIKA.

Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?

KAMA MHUBIRI NI WOKOVU UPI UNAUPELEKA KWA WATU?

JE! MUNGU NI NANI?

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/14/mungu-wetu-jinsi-lilivyo-tukufu-jina-lako-duniani-mwote/