WAKATI WA JUA KALI NDIO WAKATI WA KAZI:

by Admin | 2 June 2020 08:46 pm06

Hebu tuchukue muda kidogo kuisoma habari ifuatayo naamini tutajifunza kitu,

1Samweli 11: 1 “Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni ,akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi;na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi,na sisi tutakutumikia.

2 Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang’olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia.

3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea.

4 Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia.

5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng’ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.

6 Na roho ya MUNGU IKAMJILIA SAULI KWA NGUVU, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana.

7 Naye akatwaa jozi ya ng’ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng’ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.

8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.

9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, WAKATI WA JUA KALI, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.

10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema.

11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata WAKATI WA JUA KALI; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja”.

Biblia inasema taa ya mwili ni jicho, maana yake mtu akitolewa macho anakuwa kipofu, giza linaingia katika mwili wake wote, hebu fanya utafiti wa kufunga macho yako uone utakachokiona…bila shaka ni giza tupu…

Mathayo 6:22 “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.

23 Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!”

Kwahiyo kwa tukio hilo hapo juu, kuna wakati Mfalme wa Moabu alitaka kuingia katika ardhi ya Israeli inayoitwa Yabeshi, na alipoingia kwasababu ya wingi wa majeshi yake akawatishia Israeli vikali, nao wakaogopa, wakanyenyekea chini yake wakamwambia fanya mapatano nasi (maana yake kama unataka kitu chochote kutoka kwetu hata kama ni kodi tutakupatia)..lakini Yule mfalme kwa kiburi akasema hatataka kitu chochote bali kumng’oa kila mtu wa mji huo wa Yabeshi jicho la kuume…Na lengo la kuwaambia hivyo ni ile awaaibishe na pia aliingize giza katika mji ule, kwasababu alijua jicho la mtu ndio mwangaza wake..mtu hakuna chochote anaweza kufanya.

Jambo hilo liliwahuzunisha watu wa Yabeshi, mpaka kufikia hatua ya kwenda kuomba msaada wa ndugu zao waisraeli walio kwenye majimbo mengine, na wakati huo Israeli walikuwa wameshajitakia mfalme, na walimteua Sauli…lakini kila mtu alikuwa anamdharau Sauli kwa kuwa walimwona kama ni kijana laini asiye na uwezo wa kutawala wala wa vita. Lakini biblia inasema ROHO YA MUNGU ilimjia Sauli kwa nguvu na kumpa moyo wa ujasiri na ushujaa, na kutoka kwenda kuwapiga wamoabu na kuwaangamiza wote kabisa…Lakini jambo pekee ni kwamba hawakuwapiga wakati wa jioni, au wakati wa asubuhi, bali waliwapiga wakati wa JUA KALI linaloangaza…Kuashiria kuwa wao sio WANA WA USIKU bali wa Mchana.. Na kamwe Nuru ya macho yao haiwezi kuzimwa…wala giza haliwezi kuingia kwao.  Hivyo kwa imani waliwaua wakati wa jua kali..

Kama tujuavyo wakati wa jua kali, ndipo watu wanazimia nguvu, ndio wakati watu wanachoka haraka, ndio wakati ambao mwili unapungukiwa maji….Lakini kwa majeshi ya Bwana, hicho ni kinyume chake…wakati wa mchana ndio wakati wa kushinda na kupambana…

Wakati wa mchana(jua kali) ndio wakati wa kuingia vitani, wakati wa mchana ndio wakati wa kwenda kuyavamia majeshi ya adui, wakati wa mchana ndio wakati wa kwenda kuteka nyara, ndio wakati wa kumnyang’anya shetani mateka, wakati wa jua kali ndio wakati wa kuhubiri injili..

Bwana Yesu alisema…

Yohana 9:4 “Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi

5 Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”.

Wakati huu wa jua kali ndio wakati adui yetu kukosa nguvu, ndio wakati anaoungua, ndio wakati ambao anakimbilia kivulini na mafichoni…hivyo ndio wakati wa kumfuata huko kwa vishindo kama Sauli alivyofanya, na kumwangusha na kumnyang’anya mateka sio wakati wa sisi kulitafuta giza au kivuli kama wao.. “Na Yesu ndio Nuru yetu, ndio jua letu..na sisi ni wana wa Nuru, jua lake halituchomi wala halituumizi wala halituchoshi, wala halitumalizi maji mwilini”..linawadhoofisha maadui zetu lakini si sisi.

Isaya 18:4 “Maanaa Bwana ameniambia hivi, Mimi nitatulia, na kuangalia katika makazi yangu, kama wakati wa mwangaza mweupe wa JUA KALI, mfano wa wingu la umande katika hari ya mavuno”.

Ifanye kazi ya Mungu wakati huu wa Neema, wakati huu wa jua kali…usiku unakuja ambao hutaweza…wakati adui atakuwa na nguvu…na wakati huo ni kipindi cha dhiki kuu…wakati ambao neema ya Yesu itafungwa…huo ndio wakati wa mamlaka ya nguvu za giza kutenda kazi..kutatokea dhiki isiyo ya kawaida!. Yule joka atakapopata nguvu…..Bwana atuepushe na hiyo dhiki, ili wakati huo utakapofika utukute tuwe tumeshanyakuliwa na watakatifu wengine kwenda mbinguni kwa baba na tumeshaimaliza kazi yake.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?

USIHUZUNIKE.

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.

Nuhu alipataje ujuzi wa kuwatambua wanyama wale wote na kuwaweka ndani ya Safina?

JE! UMEFUNDISHWA?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/02/wakati-wa-jua-kali-ndio-wakati-wa-kazi/