USIISHI BILA KUIFANYA KAZI YA MUNGU KABISA..

by Admin | 3 July 2020 08:46 am07

Shalom mtu wa Mungu, karibu tuyatafakari maandiko…leo ni siku nzuri Bwana aliyotupa..hivyo ni vyema tukachukua nafasi hii kulitafakari Neno lake kwa ufupi..

Kumbuka siku zote kuwa baada ya kumpokea Kristo, kila mmoja wetu anawajibu wa kuifanya kazi ya Mungu kupitia karama Mungu aliyoiweka ndani yake. Kuna hatari kubwa sana ya kutoitumia karama Mungu aliyoiweka ndani yako kabisa….Na madhara makubwa yapo baada ya maisha haya…wakati ule ambapo watakatifu watapewa thawabu zao wewe hutakuwa na chochote…

Katika siku ile waliokuwa waaminifu kwa karama zao watapewa thawabu kubwa zaidi..na wale waliokuwa walegevu na kuleta faida ndogo katika ufalme wa mbinguni watalipwa kidogo, na wale ambao hawajafanya kitu kabisa hawatapewa chochote…

Lakini ni heri kufanya hata kama ni KIDOGO sana ukapata kitu kule kuliko kutofanya kabisa…

Hebu naomba usome mfano huu Bwana alioutoa…inawezekana ulishawahi kuusoma hapo kabla mara nyingi, na kuurudia rudia…. lakini hebu chukua muda tena sasa hivi kuusoma hadi mwisho taratibu, pasipo kuruka kipengele hata kimoja, kuna kitu cha kipekee sana nataka tujifunze leo.

Luka 19:11 “Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara.

12 Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.

13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, FANYENI BIASHARA HATA NITAKAPOKUJA.

14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.

21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23 BASI, MBONA HUKUIWEKA FEDHA YANGU KWA WATOAO RIBA, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho”.

Mfano huo unamhusu Bwana Yesu mwenyewe, yeye ndio mfano wa huyo mtu kabaila..ambaye aliondoka na kwenda nchi ya mbali(mbinguni) kutuandalia ufalme…na alipoondoka alitupatia vipawa (karama) akatuambia tukawafanye watu wote kuwa wanafunzi (maana yake kuwahubiria na kuwageuza wamwamini yeye kila mmoja kwa kipawa alichopewa)…Na siku moja atarudi kutoka huko nchi ya mbali(mbinguni)…alipokwenda kututengenezea ufalme…atarudi duniani kwaajili ya utawala wa miaka 1,000 (Ufunuo 20).. Na siku atakaporudi atawaangamiza wale wote ambao hawakumkubali (yaani watu waovu)..Na baada ya kuwaangamiza waovu wote ndipo atakapowakusanya watumishi wake waliompokea…na hapo kila mmoja ataketi na kutoa hesabu ya faida aliyoileta katika ufalme wa mbinguni..

Watasimama wachungaji, watasimama waimbaji, watasimama mitume, watasimama mashemasi, waalimu, manabii, maaskofu, wazee wa kanisa, waumini wote na kila mmoja atatoa hesabu jinsi alivyoitumia karama yake…waliofanya vizuri watapewa mamlaka makubwa na waliokuwa wavivu watakosa vyote…

Sasa katika kisa hicho tunasoma kuna mmoja alifukia talanta yake chini…kwa uvivu akijitumainisha kwamba Bwana huwa hasaidiwagi kazi…yeye anang’oa pando asilolipanda, kazi ambayo hajaifanya yeye anaiharibu!…kwahiyo akajifariji kwamba Mungu huwa hasaidiwi kazi…hatutegemei hata tusipokwenda kuhubiri walio wake watakuja tu!.. kwanza unaweza kwenda kuhubiri ukakosea kosea maneno ndio ukawa umemuudhi badala ya kumfurahisha……pia sio lazima sana kumtolea kwani hata tusipochangia chochote kwenye kazi yake yeye ni tajiri na sisi ni mavumbi hivyo atafanya njia tu kwa vyovyote vile(hasaidiwi kazi)……pia yeye hahitaji sana sifa zetu, tayari anao malaika wengi wanaomwimbia….. n.k

Kwahiyo kwa kujitumainisha huko na visingizio hivyo… mtu wa namna hii akawa hafanyi kazi ya Mungu akafananishwa na mtu aliyefukia fedha yak echini ya shimo…siku ile ikafika na Bwana akamhukumu kwa kinywa chake…

Ndugu mpendwa baada ya kuokoka…usikae ufikiri kwasababu Mungu ni mkuu basi hatutegemei sisi….Ni kweli hatutegemei anaweza kufanya asilimia mia pasipo sisi…lakini hataki tuwe wajinga!…Sio kwasababu kasema maneno haya…

Matendo 7:49 “Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,

50 Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?”

Basi na sisi ndio tubweteke tusimjengee nyumba…kwasababu amesema yeye hakai kwenye nyumba zilizofanywa na mikono yetu…Ndugu Usikae ufikiri hivyo kamwe!.. Daudi aliujua vizuri huo mstari pamoja na Sulemani mwanawe lakini walimjengewa Bwana nyumba hivyo hivyo…na Mungu akapendezwa nao..Sikia maneno Sulemani aliyoyasema..

1Wafalme 8: 26 “Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu.

27 LAKINI MUNGU JE? ATAKAA KWELI KWELI JUU YA NCHI? TAZAMA, MBINGU HAZIKUTOSHI, WALA MBINGU ZA MBINGU; SEMBUSE NYUMBA HII NILIYOIJENGA!

28 Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo.

29 Macho yako yafumbuke na kuielekea NYUMBA HII usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa”.

Walijua Mungu mbingu hazimtoshi na huku duniani ni mahali pa kuwekea miguu yake..lakini walilazimisha kumjengea Mungu duniani japokuwa waliyajua hayo maandiko…na mpaka leo Hekalu la Sulemani linajulikana.

Vivyo hivyo na wewe..usiseme Bwana ana malaika wengi…usiseme Bwana hahitaji fedha yangu kwani dhahabu zote na fedha zote ni za kwake… Usiseme sio lazima kujisumbua kuhubiri kwani Bwana anao watumishi wengi…usiseme sio lazima kujisumbua kuimarisha kazi ya Mungu kwasababu Mungu hahitaji msaada kutoka kwetu..ukifanya hivyo utakuwa umefukia talanta yako chini uliyopewa…

Na Mwisho kabisa Bwana alimwambia Yule mtu aliyefukia ile fedha chini maneno haya…” BASI, MBONA HUKUIWEKA FEDHA YANGU KWA WATOAO RIBA”… Mtu anayeweka fedha kwa watoa riba…maana yake haendi kuifanyia shughuli yoyote ile hela..ni kuiweka tu baada ya wakati Fulani inajizalisha…ni kama vile umemkopesha mtu hela…Sasa kazi ya kukopesha haitumii jasho lolote…ni kuwekeza tu hela na kusubiria faida basi!….Hata hiyo kazi nyepesi ambayo haihitaji jasho! Bwana angetegemea aione kwa huyu mtu lakini hakuiona..

Kadhalika na wewe…inawezekana huwezi kabisa kusimama mimbarani, au kwenda mitaani kuhubiri… basi angalau wekeza kwenye kazi ya Mungu kwa fedha zako au mali zako kwa uaminifu, nunua kinanda, nunua mifuko kadhaa ya cement, au nunua chochote kile uwezacho kipeleke nyumbani kwa Mungu…kwasababu unapomtolea Mungu, fedha au mali zile zinakwenda kutumika katika kuifanya kazi ya Mungu na hivyo unaleta faida katika ufalme wa Mbinguni… ukifanya hivyo angalau Bwana atakuheshimu siku ile utakuwa umeiweka talanta yako kwa watoa riba…

Bwana atusaidie sana katika hayo..

Kama bado hujampa Yesu maisha yako…tunaishi katika siku za mwisho, Kristo yupo mlangoni kurudi…hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zote unazozifanya kama ulevi, rushwa, anasa, uasherati, uuaji, ufiraji, ulawiti,ushoga, usagaji, utazamaji wa picha za ngono, kujichua na nyingine zinazofanana na hizo…Tubu leo kwa dhati na amua kuziacha…na baada ya kuomba rehema Bwana atukusamehe kama alivyoahidi…Na amini kashakusamehe kama umetubu kwa dhati!..Na baada ya hapo tafuta ubatizo sahihi ambao ni wa maji tele na kwa jina la Yesu ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu…na baada ya hapo Roho Mtakatifu ambaye tayari atakuwa ameshafika karibu yako atakupa uwezo wa kuzishinda hizo dhambi ulizoziacha..ili usizirudie tena…na mengine yaliyosalia atakuongoza kuyafanya.

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano.

MAOMBI YA VITA

FAIDA ZA MAOMBI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/03/usiishi-bila-kuifanya-kazi-ya-mungu-kabisa/