Mungu aliposema Yesu ni mwanawe pekee, alimaanisha hakuwa na wengine?

by Admin | 29 July 2020 08:46 pm07

SWALI: Mungu aliposema Yesu ni mwanawe pekee, Je! Ina maana hakuwa na wana wengine au hana wana wengine zaidi yake?


JIBU: Tusome..

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.

Hivyo ndivyo inavyotafsiriwa na watu wengi na madhehebu mengi ya dini..Lakini sivyo inavyomaanisha hapo, Mungu kumwita Yesu mwanawe pekee, haimaanishi, hajawahi kuwa na wana wengine,(ambao ndio sisi), bali alimaanisha Yesu ni mwana-wake-wa-kipekee tofauti na sisi wengine aliyebakiwa naye, mwenye mahusiano ya kitofauti na wengine, mwana wa maagano ndio maana akimwita Kristo  mwanawe pekee.

Ili kulithibitisha jambo hilo embu tutazame baadhi ya vifungu vya maandiko vinavyoelezea habari inayofanana na hiyo, Na hiyo si nyingine zaidi ya ile ya Ibrahimu na mwanawe Isaka..tusome.

Mwanzo 22:2 “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia”.

Soma tena..

Mwanzo 22:12 “Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee”.

Soma tena…

Waebrania 11:17 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee”;

Unaona ukisoma mistari hiyo yote, unaweza kudhani Isaka ndio aliyekuwa mwana  tu wa Ibrahimu hakuwa na wengine, lakini tunajua kuwa kabla ya Isaka alikuwepo Ishmaeli. Na baada ya Isaka walikuja wengine wengi (Mwanzo 25:1-4).

Lakini ni kwanini Mungu amwite Isaka kama mwana pekee wa Ibrahimu, ni kwasababu alikuwa mwana wa maagano, mwana wa ahadi, tofauti na wale wengine,…Isaka alifananishwa na Kristo

Hivyo Kristo Bwana wetu ndio mwana pekee wa Mungu, ambaye ameshikilia maagano yetu yote, kwa kupitia yeye, Mungu ametupenda tena, kwa kupitia yeye sisi tumebarikiwa, na kwa kupitia yeye, tunapata uzima wa milele, na tumaini la ufufuo baada ya kifo.  Hivyo tukimwamini na kumpokea tunaingia katika huo mnyororo wa Pendo la Mungu.

“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye”. Kama hujampokea huu ni wakati wako sasa.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

  Au Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/29/mungu-aliposema-yesu-na-mwanawe-pekee-alimaanisha-hakuwa-na-wengine/