MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

by Admin | 7 December 2020 08:46 am12

Shalom, karibu tujifunze maneno ya uzima.. Lipo swali ambalo linaulizwa na watu wengi, kwamba kama Mungu anajua kuna jambo litakwenda kutokea mbeleni ambalo litanisababishia mauti, kwanini basi asinizuie kwenda kulifanya badala yake ananiacha mpaka naingia, na mwisho wa siku napotea na kwenda kuzimu? Mbona kama vile atakuwa sio Mungu wa upendo?

Kama na wewe swali hili lipo ndani yako basi tuzidi kutafakari pamoja somo letu la leo,

Kitabu cha Mithali kinasema..

“Kwa kuwa mtego hutegwa BURE, Mbele ya macho ya ndege ye yote”.( Mithali 1:17).

Embu jiulize, mtu anayetega mtego wa kumshika ndege kwa ajili ya kitoweo chake, Je! Unadhani Mungu hampendi ndege yule? Au unadhani Mungu hajampa uwezo wa kuwakimbia maadui zake kiwepesi?

Au mtu anayetega mtego wa kunasa panya, unadhani Mungu anawachukia panya, na hivyo kawaondolea uwezo wa kuwakimbia adui zao?

Au mtu anayetega ndoano kuvua samaki, unadhani Mungu hawapendi samaki wake,?

Sikuzote mpaka umeona kitu fulani kinaundiwa mitego, basi ujue kuwa kitu hicho kilishashindikana  kukamatika kwa njia rahisi, au ya kawaida, hivyo kimetafutiwa njia mbadala, kwamfano leo hii unaweza kumuona ndege katua hapo pembeni yako, hatua kadhaa tu pembeni, lakini embu kajaribu kwenda kumkamata kwa mikono yako kama utaweza,? Au umwone panya anakatiza kwenye kona ya nyumba, au store, halafu fanya mazoezi ya kwenda kumkata kwa mikono kama vile unavyokamata chura uone kama itakuwa ni kazi rahisi kwako.

Au umwone samaki anaelea juu ya maji, hivyo unatakwenda kwenda kumchota haraka kwa mikono yako, jaribu zoezi hilo kama litakuwa rahisi. Huwezi kuwapata kwasababu Mungu tayari kashawekea uwezo ndani yao wa kujiangua kutoka kwa maadui zao kivyepesi sana.. na wenyewe wanajua kabisa maadui zetu ni ngumu kutushika kwasababu hawana wepesi tulionao sisi, au hawana uhodari tulionao sisi wenyewe.. Na  sisi tunaowawinda tunajua kuwa ili waendelee kuwa salama ni wajibu wao, kutotuamini sisi kwa kitu chochote siku zote za maisha yao hapa duniani, haijalishi tutawavutia kwa vitu vingi kiasi gani wanavyovipenda.

Vivyo hivyo na sisi wanadamu, Mungu ameshatupa uwezo mkubwa sana ndani yetu wa kumshinda adui yetu shetani, na yeye analijua hilo, hawezi kuja na kukukamata hivi hivi kama anavyotaka, hana uwezo huo, anajua kabisa hawezi kukupata, lakini anachokifanya ni kijiundia mitego yake mbalimbali, ambayo hiyo  ikishakunasa, basi  hapo ndipo anakuwa na uwezo wa kukufanya chochote anachotaka ikiwemo hata kukuua.

Kwamfano mtego mmojawapo maarufu , ni uasherati, shetani anaweza kukuletea kahaba, ili mkazini, lengo lake sio ukutane na kahaba au uzini tu halafu basi, hapana, bali  ni ukosane na Mungu wako kwa kitendo hicho, ili apate nafasi ya kuyaachilia mapepo yake yaingie katika maisha yako kukuharibu kirahisi katika kila nyanja, ikiwemo upate na magonjwa ya zinaa kama vile ukimwi ili ufe kabla ya wakati wako.

Lakini hayo anajua hayawezi kuja hivi hivi, ni mpaka akuwekee mtego, ndipo hapo   anakuletea kahaba mzuri, au mwanaume mwenye pesa, anakulaghai na wewe bila kufikiri kuwa ule ni mtego umewekwa mbele yako unakwenda kuuva, ukidhani kuwa Mungu atakuepusha nao.. Hilo Mungu hawezi kulifanya ndugu yangu.

Kwa nafasi yako soma kitabu cha Mithali sura ya 7 yote, uone jinsi, kijana mpumbavu aliyetegwa na mwanamke mzinzi, na hatma yake inavyokuwa; hatuwezi kusoma vyote lakini vile vifungu vya mwisho mwisho vinasema..

Mithali 7:21 “Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.

22 Huyo akafuatana naye mara hiyo, KAMA VILE NG’OMBE AENDAVYO MACHINJONI; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;

23 Hata mshale umchome maini; KAMA NDEGE AENDAYE HARAKA MTEGONI; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.

24 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.

25 Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake.

26 Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, JUMLA YA WALIOUAWA NAYE NI JESHI KUBWA.

27 Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.

Ndege anayenaswa kwenye mtego ni kajitakia mwenyewe na sio kwamba alikuwa ni dhaifu, tamaa zake ndizo zilizompeleka pale,. Leo hii, unapojikuta kwenye matatizo mazito, ambayo unajua kabisa ni kwasababu ya dhambi Fulani uliyoifanya ndio yakakukuta, usianze kumlaumu Mungu ni kwanini hakukuepusha nayo hapo kabla. Mungu alishakupa uwezo huo tangu zamani,  Na Mungu naye hawezi kumlaumu shetani, kwasababu shetani naye analo la kujitetea, anasema mimi sikumuita mtu aje kwenye mtego wangu, wala sikumlazimisha mtu, kufuata kile nilichokiweka kwenye mtego, ni yeye mwenyewe alinifuata, ni ndio hapo akanasikia akaangamia, ilikuwa ni wajibu wake kuchukua tahadhari anapoishi duniani.

Na ndio maana biblia inasema..

Hosea 4: 6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;..”

 Tukikosa maarifa ya kuzijua njama za shetani, au kuyajua mafumbo ya shetani, tutajikuta tunaingia katika matatizo ambayo tutajiuliza ilikuwaje kuwaje tumejikuta hapa,

Ufunuo 2:24 “Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, WASIOZIJUA FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.

25 Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja”.

Hivyo kila mmoja anao wajibu wa kupata maarifa sahihi ya kuitambua mitego ya adui. Na maarifa hayo utayapata kutoka katika Neno la Mungu tu basi, biblia imejaa siri za kuepukana na hila za adui. Na ndio maana shetani hapendi watu waisome.

Kuwa msomaji wa biblia kila siku, tafakari , usiisome kama gazeti, hiyo tu ndio itakayokuwa nuru yako katika zama hizi za kumalizia, kumbuka mitego ni mingi, vishawishi ni vingi, na ipo ya aina tofauti toauti, uwezo umepewa, pengine umepungukiwa tu na maarifa. Hivyo ni wajibu wako kuyatafuta maarifa hayo, ambayo utayapata katika Neno la Mungu. Yaani BIBLIA.

Hakuna jaribu lolote linalotendeka leo hii, ambalo halijawahi kuandikwa katika biblia na njia ya kuepukana nalo., Hivyo jijengee desturi ya kusoma Neno la Mungu. Ili usiwe wa kumlaumu Mungu, kwanini hiki, kwanini kile, wakati ni wewe mwenyewe uliyakataa maarifa, hivyo ukanasika kirahisi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/07/mtego-hutegwa-bure-mbele-ya-macho-ya-ndege-ye-yote/