Fadhili ni nini? Nini maana ya “fadhili zake ni za milele” kibiblia?

by Admin | 8 December 2020 08:46 pm12

Biblia inapozungumza juu ya fadhili za Mungu, ni zaidi ya zile fadhili ambazo tunazojua  ambazo mtu anaweza kuzifanya kwa mtu mwingine, yaani kumuonyesha ukarimu na wema..

Kibiblia Fadhili za Mungu ni Neno pana sana, kwa kiebrania linatamkwa “Hesed”, ambalo tafsiri yake huwezi kuelezea kwa neno moja, au kwa maneno machache.

Fadhili za Mungu sio tu wema na ukarimu Mungu anaotufanyia sisi, bali linamaanisha pia Upendo wa Mungu usioelezeka, upendo wa kusaidia, upendo wa kuvumilia, Upendo wa kuokoa upendo wa kutoa,..

Ni wema usio na masharti, kwamba hatutendei fadhili zake kisa sisi tumemfanyia kitu kwanza, au tumekuwa marafiki zake, Hapana. Anatenda kama vile ni wajibu wake kufanya, Wema huo hauwezi kuelezeka, kwasababu unagusa kila Nyanja, ambazo haziwezi kufikiwa na mwanadamu yoyote Yule, au kiumbe chochote kile mbinguni au duniani., umeingia ndani kabisa.

Na ndio maana Neno hili utalisoma sehemu nyingi sana katika biblia,  Na pia utaona Daudi kila alichokiona  au alichokitaja alihitimisha na neno “kwa maana fadhili zake ni za  milele”..

ZABURI 136

1 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2 Mshukuruni Mungu wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

3 Mshukuruni Bwana wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

4 Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

5 Yeye aliyefanya mbingu kwa fahamu zake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

6 Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

7 Yeye aliyefanya mianga mikubwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

8 Jua litawale mchana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

9 Mwezi na nyota zitawale usiku; Kwa maana fadhili zake ni za milele. 10 Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

11 Akawatoa Waisraeli katikati yao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

12 Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

13 Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

14 Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

15 Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

16 Yeye aliyewaongoza watu wake jangwani; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Vipo vifungu vingi sana Soma pia.. 1Nyakati 16:34, Zaburi 106:1 n.k.

Utaona pia Musa alipofumbuliwa macho yake na kumwona Mungu kwa sehemu, alipokuwa kule mlima alitangaza na kusema;

Kutoka 34:6 “Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, MWENYE FADHILI, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;

Vivyo hivyo kilichomchea Mungu kumtuma mwanawe duniani kuja kutuokoa, hakikuwa kingine zaidi ya Fadhili zake za milele zinazodumu kwetu daima..

Alikuwa tayari kumtoa mwanawe wa pekee kafara ili sisi tupate wokovu, Jiulize wewe unaweza kumtoa mwanao, tena yule unayempenda kuliko wote awe sadaka ili jirani yako ambaye hakusaidii chochote apone au afaidike? Unaweza kufanya hilo?  Huwezi kwasababu hujafikia kiwango hicho cha fadhili za Yehova.

Hivyo kama  tukiyajua hayo ni wajibu wetu kumwimbia usiku na mchana, kumshukuru juu ya wema wake aliotuonyesha na anaotufanyia kila siku. Na Tunampa Mungu sifa za vinywa vyetu, pamoja na kwa MATOLEO YETU.

Jina la Yesu Kristo libarikiwe daima.

 Haleluya.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

NI NANI ATAKAYETUTENGA NA UPENDO WA KRISTO?

KWA KUWA NGUVU ZA MBINGUNI ZITATIKISIKA.

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/08/fadhili-ni-nini-nini-maana-ya-fadhili-zake-ni-za-milele-kibiblia/