IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

by Admin | 30 December 2020 08:46 pm12

Shalom, karibu tena tuyatafakari maneno ya Bwana wetu Yesu, biblia inasema manabii wengi na wenye hekima walitamani sana kusikia tunayoyasikia na kuyaona tunayoyaona lakini hawakupata neema hiyo, Lakini mimi na wewe tumepewa neema ya kuyasikia maneno ya Bwana wetu Yesu. Ni furaha iliyoje?

Yesu ambaye aliiumba dunia kwa Neno lake, leo hii inakaa na sisi kutufundisha hilo hilo Neno lake, unadhani ni rahisi sisi kuacha kuyatafakari maneno yake kwa kuyarudia rudia kila siku? Tutafanya hivyo kwa msaada wake.

Leo tuutafakari tena kwa pamoja mfano huu alioutoa. Unaweza ukawa umeusoma mara 100, lakini tuutafakari tena, Neno la Bwana huwa haliishi ubora.

Luka 15:3 “Akawaambia mfano huu, akisema,

4 Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?

5 Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.

6 Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.

7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

8 Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?

9 Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.

10 Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye”.

Katika maneno hayo, tunaweza kujifunza jambo moja, kwa hawa watu wawili, kwanza, furaha yao haijaja katika kukipata kitu kipya, bali ni katika kitu kile kile cha zamani walichokuwa nacho.  Lingekuwa ni jambo la heri kama wangekuwa wamezalisha kitu jipya na kwa hicho kikawapatia faida, hapo ndio tungesema furaha yao inamaana, lakini tunaona ni vilevile walivyokuwa navyo hapo mwanzo ndivyo wanavyovifurahia.

Furaha hii sio ya kawaida, bali ni furaha inayojificha ndani ya uthamani wa kitu. Inazuka pale kitu hicho kinapoathiriwa na kupata suluhisho.

Furaha ya namna hii inaweza kujengeka hata kwako, kwamfano unaweza ukawa na simu yako nzuri, lakini ghafla kibaka akapita mbele yako akakupokonya akakimbia nayo..Ni wazi kuwa hilo jambo litakuudhi sana kama sio kukuhuzunisha. Lakini baada ya wiki moja pengine wakati unafikiria labda kwenda kununua simu  nyingine, unashangaa unapigiwa simu na polisi, unaambiwa simu yako tumemshika nayo mtu mmoja mwizi alikuwa anakwenda kuiuza.. Hivyo njoo chukua simu yako.

Ni wazi kuwa taarifa hizo zitauchangamsha moyo wako, na kukufurahisha sana kana kwamba ni jambo fulani la maana sana umelipata, kumbe ni kitu kile kile. Furaha hii inakuja yenyewe tu ndani, haulazimishwi, unasema daah! Afadhali nimeipata simu yangu, asante Mungu. Tena ukikutana na Yule mtu aliyekusaidia utataka hata umpe chochote cha kumpongeza au kumfuta jasho kwa kukuhangaikia.

Sasa huzuni na  furaha ya namna hiyo, ndiyo Mbingu yote na malaika wa Mungu wanayoipitia kila siku, pale mwenye haki mmoja anapoicha imani, mbinguni wanahuzunika, na kukasirika, lakini pale mwenye dhambi aliyeiacha imani anapotubu , Malaika wanamshukuru Mungu,wanasema afadhali fulani kapatikana, siku yao huwa inakwenda vizuri sana, wanamshukuru Mungu sana kwa hilo. Hivyo na sisi tusichoke kuwahubiria wenye dhambi wamgeukie Mungu hata kama hapo mwanzo walikuwa wameokoka wakapotea, Unaweza kudhani wakitubu na kumgeukia Mungu,ndio basi, mbinguni wanalichukulia hilo jambo kawaida tu, fahamu kuwa huko mbinguni ni shangwe tu.

Biblia inatuonyesha hilo jambo huwa linawafurahisha na kuwachangamsha sana malaika. Wapo kondoo wa Mungu wengi sana leo hii wamepotea, wengine wamerudi nyuma, ule moto waliokuwa nao umezima,

Idadi ya wakristo walioacha imani ni kubwa kuliko idadi ya watu ambao hawakuijua imani kabisa kwasasa hivi..tafakari tu mpaka Yesu mwenyewe  anasema mwenye dhambi MMOJA TU, atubupo, hajataka wengi, bali mmoja tu, inaipa furaha mbingu. Itakuwaje wakitubu mia, au mia mbili au elfu, Hivyo kwa pamoja tusimame katika karama zetu, kuwarejesha wale waliopotea katika imani tena, na Bwana atusaidie.

Vilevile ikiwa na wewe unayeusoma ujumbe huu, hapo mwanzo ulikuwa kwa Mungu lakini sasa umeurudia ulimwengu, hapo Mwanzo ulikuwa moto lakini sasa umekuwa baridi tena, fahamu kuwa umemuhuzunisha Mungu sana kwa maamuzi yako hayo mabaya. Mungu anasikitika gharama alizoingia kukukomboa na leo hii unamwacha na kwenda kuunufaisha ulimwengu. Hilo jambo linamsikitisha kweli kweli ndugu, yangu pamoja na malaika wake.

Mungu anataka leo hii umrudie tena, ujumbe huu unakuhusu wewe, mwana mpotevu, leo mrudie muumba wako, hizi ni siku za mwisho, dunia hii haina muda mrefu mpaka iishe, na hata kama bado itakuwepo, wewe hauna garantii ya kuiona kesho.Au unayo? Vifo vinakujaga ghafla tu bila hodi, ziwa la moto halishibi watu, na kila sekunde maelfu ya watu wanashuka huko. Wanajuta kwa majuto ambayo hayaelezeki, mfano wake ni Yule tajiri wa Lazaro, habari yake unaifahamu.

Huko walipo sasahivi wanatamani wewe utii injili uokoke, ili usifike hizo sehemu za mateso walizopo. Dakika moja tu ya uhai uliyopewa, usiichee rafiki yangu, itathamini, shetani anaiwinda roho yako, kwa namna isiyo ya kawaida. Hivyo tubu mgeukie Kristo upokee ondoleo la dhambi. Na yeye mwenyewe atakutia muhuri kwa Roho wake mtakatifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/30/ifahamu-huzuni-na-furaha-ya-malaika/