Korazini na Bethsaida ilikuwa ni miji iliyokuwepo kandokando ya bahari ya Galilaya.. Sasa Bahari ya Galalilaya, iliitwa hivyo bahari lakini kiuhalisia sio bahari bali ni ziwa, kwasababu bahari ni lazima iwe na maji ya chumvi, lakini Hili la Galilaya lilikuwa na maji yasiyo chumvi (yaani maji barini), hivyo lilikuwa ni ziwa mfano wa Ziwa Victoria, isipokuwa halikuwa kubwa kama ziwa Victoria, Ziwa hilo la Galilaya mpaka leo lipo huko kaskazini mwa Israeli.
Sasa kando ya hilo ziwa la Galilaya (au Bahari ya Galilaya) kulikuwepo na miji maarufu mitatu, ambayo ni Korazini, Bethsaida na Kapernaumu. Miji hiyo kwamfano mrahisi tuseme Mji wa Mwanza, Mara na Kagera, iliyoizunguka ziwa Victoria, na ndio hivyo hivyo miji hiyo mitatu ilikuwa imeizunguka hiyo bahari ya Galilaya.
Sasa kipindi ambacho Bwana Yesu yupo duniani, sehemu za kwanza kwanza kabisa kuhubiri injili zilikuwa ni katika hiyo miji mitatu kwasababu haikuwa mbali sana na mji wa Nazareti aliokulia Bwana Yesu. Hivyo miji hii mitatu ilipata neema isiyokuwa ya kawaida kuona miujiza mikubwa. Tofauti na miji mingine yoyote ya Israeli kama Yerusalemu na Bethania au Samaria. Hivyo kwa miujiza iliyoiona ilitegemewa iwe ndio miji ya kwanza kutubu na kumkubali Mwokozi, lakini ilikuwa kinyume chake…Ndipo Bwana Yesu akaiambia siku moja maneno haya…
Mathayo 11:20 “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu. 21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu. 22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo. 24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.
Mathayo 11:20 “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu.
21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.
23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.
Maandiko hayo yanatuonyesha kuwa japokuwa watu wa Sodoma na Gomora walihukumiwa kwa adhabu ya moto, na kuchomeka kikatili, kutokana na dhambi zao, lakini kumbe bado haitoshi, wataendelea tena kuadhibiwa baadaye.
Hiyo inaogopesha sana, kama uliwahi kuona picha za ajali ya watu walioungua kwa moto, huwezi kufikiri kwamba watu kama hao wanaweza tena kwenda kuadhibiwa huko wanakokwenda…Lakini biblia inatufundisha kuwa watenda dhambi hata wakifa hapa kwa kuadhibiwa na Mungu, huko wanakokwenda watakutana na adhabu iliyo kubwa kuliko hiyo walioadhibiwa hapa..Ndicho Bwana Yesu alichokisema hapo kwenye huo mstari wa 24.
“Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.
Maana yake watu wa Sodoma, wataendelea kuadhibiwa..na sasa wapo kuzimu wanateseka, na siku ile ya Mwisho katika hukumu ya kiti cheupe cha enzi cha mwanakondoo, watahukumiwa na kutupwa kwenye ziwa la moto lenye mateso mara nyingi zaidi.
Lakini, Bwana Yesu anazidi kusema… “itakuwa heri kwa watu wa Sodoma kustahimili adhabu siku ile kuliko wewe”. Yaani hiyo miji ambayo ilihubiriwa na kuona miujiza mingi lakini haikutubu.
Hiyo inatupa picha nyingine kuwa, katika ziwa la moto, viwango vya kuadhibiwa vitatofautiana…wapo watakaoteseka sana kuliko wengine… Shetani hawezi kuteswa sawa na mzinzi, wala nabii wa uongo hawezi kuteswa sawa na kahaba..viwango vitatofautiana.
Lakini hapo Bwana anasema adhabu ya wale ambao hawatatubu, baada ya kuona miujiza mingi ya ki-Mungu ikitendeka..hao Bwana anasema dhambi yao ni kubwa kuliko ya watu wa Sodoma na Gomora, hivyo watahukumiwa zaidi kuliko watu wa Sodoma na Gomora,.
Hii ni tafakari fupi tu ya leo, ambayo ningependa tuitafakari pamoja leo. Na kujua kuwa miujiza Roho Mtakatifu anayoifanya kwenye maisha yetu, tunayoina kila mahali, sio kwa lengo la kutuburudisha, bali ni kwa lengo la kulihakikisha Neno lake kuwa ni kweli. Hivyo ni wajibu wetu kutubu na kujitakasa sana. Na kama bado Yesu yupo nje ya maisha yetu, huu ndio wakati wa kumkaribisha ili tusiangukie mikononi mwa hukumu ya Mungu.
Kwasababu ni dhahiri kuwa sisi tunaoishi sasa tunaona miujiza mikubwa ya Bwana Yesu kuliko wale watu wa kanisa la kwanza, Mpaka tunaizoelea. Kristo atusaidie tuchue hatua sahihi.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.
CHUKI ULIZO NAZO KWA MAADUI ZAKO, SIZO ALIZONAZO MUNGU JUU YAO.
Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?
Nguo za magunia katika biblia ni zipi?
Wevi na wanyanga’anyi waliomtangulia Yesu walikuwa ni wapi?
Rudi Nyumbani:
Print this post