by Admin | 30 March 2021 08:46 pm03
SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? (Luka 23:31)
JIBU: Tunaona sehemu mbalimbali katika biblia Bwana Yesu alijifananisha na MTI, utaona kuna mahali anasema mimi ni mzabibu wa kweli, mtu akikaa ndani yake huzaa sana.(Yohana 15:1-8), Sehemu nyingine katika kitabu cha Ufunuo Yesu anajulikana kama mti wa Uzima (Ufunuo 22:2).Akiwa na maana kuwa yeye ni kama mti ulio hai mbichi, utoao matunda,..wenye maneno ya uzima, wenye ishara na miujiza mingi ya wazi, aliyewaponya watu wote waliomwendea bila kushindwa na chochote. Aliyewaweka huru waliokuwa wanasumbuliwa na mateso, na mapepo, aliyekuwa na uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao, Mtu ambaye hakuwahi kuwa na doa lolote la dhambi hapa duniani, lakini hilo halikuwa na thamani machoni pao, badala yake walimdhihaki, na kumpiga na kumuua.
Mti mbichi ambao haukustahili kuchomwa moto, lakini waliuchoma moto.. vipi kuhusu miti mikavu isiyozaa,wakiiona si ndo wataifanyia zaidi. Pengine Hawataikata hata, bali wataichomea pale pale ilipo kama kuni angali imesimama,.
Na sisi ndio kama hiyo miti mikavu, ambao tumezaliwa katika dhambi, ambao hatuna ishara kama za Yesu, hatufanyi uponyaji mkuu kama wa Bwana Yesu, tunamkosea Mungu mara kwa mara, hatutoi maneno ya uzima yanayowaokoa watu muda wote, tunajikwaa kila wakati, tunategemea vipi ulimwengu utatupokea?. Tusidhani kuwa chochote tutakachojitahidi kukitenda kwa ajili ya Kristo kitakuwa ni kitu cha kupendwa sana na wao.
Yeye mwenyewe alisema..
Yohana 15:18 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.
19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.
20 Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.
21 Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka”.
Kwahiyo maneno hayo ni kuwa Bwana Yesu alikuwa anatoa tu angalizo, kwamba yatakapotutokea tusiogope au tusidhani kuwa sisi hatupendwi na Mungu au tumekosea sehemu fulani na ndio maana yametukuta kama hayo, hapana badala yake tujue kuwa kama alivyoyapitia yeye ndivyo tutakavyoyapitia na sisi pia.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/30/kama-wakitenda-mambo-haya-katika-mti-mbichi-itakuwaje-katika-mkavu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.