Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika..

by Admin | 13 April 2021 08:46 am04

SWALI: Nini maana ya hili neno,

Mathayo 21:44 “Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.

45 Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao”.


JIBU: Shalom.

Maneno hayo aliyasema Bwana Yesu kuonyesha tabia ya jiwe hilo analolizungumzia.

Hapo anaposema mtu atakayeanguka juu yake atavunjika-vunjika, ni kuonyesha kuwa jiwe hilo ni “Gumu sana”, na sio laini, useme  labda ni la udongo au kitu kingine, hapana ni ligumu kiasi kwamba ukilidondokea tu ni lazima uvunjike hakuna namna.

Vilevile aliposema, na yeyote atakayeangukiwa nalo,litamsaga tikitiki, ni kuonyesha kuwa jiwe hilo ni “zito sana” na kubwa.. kama lingekuwa ni jiwe dogo tu, na jepesi, lisingeweza kumsaga saga mtu pale linapomwangukia. Lakini mpaka linamponda ponda ni kuonyesha kuwa jiwe hilo ni zito sana.

Hivyo hapo ni Bwana alikuwa anaonyesha UGUMU, na UZITO wa jiwe hilo. Na jiwe lenyewe ni yeye mwenyewe.

Lakini badala watu wajenge juu ya jiwe hilo, wawe salama, kinyume chake Wapo watu wanaangukia juu ya jiwe hilo na wengine wanaangukiwa nalo.

Ikiwa wewe ni adui wa injili ya Kristo, unashindana na kazi za Mungu kutwa kuchwa, kazi yako ni kuididimiza kazi ya Mungu isisonge mbele, unafanya uchawi, unaloga, unapiga vita watu wa Mungu au unawavuta watu wasimjue Mungu kama alivyokuwa yule Elima mchawi aliyekutana na Paulo kule Pafo.. Ujue kuwa unahatarisha Maisha yako kwasababu ndivyo unavyoliangukia jiwe hili, na matokeo yake ni kuwa utavunjika vunjika, usiwe na faida yoyote hapa duniani.

Vilevile wapo watu muda wote, ni kuyaasi maagizo ya Kristo kwa makusudi, japokuwa wanaufahamu ukweli, hawa wapo kanisani, utawaona wanazini kwa makusudi na utakuta ni wachungaji au washirika wakongwe, wanafanya dhambi zao kwa siri, japokuwa kwa nje wanaonekana ni wema.. Sasa watu kama hawa, Upo wakati hili jiwe litawaangukia, na likishawaangukia hapo hakuna kupona tena, unasagika tikitiki. Wakati ambapo ghadhabu ya Mungu juu yako imefikia kilele, huwa hakuna kupona tena.

Na ndio maana Bwana Yesu aliyasema maneno hayo, kufuatana na habari aliyokuwa anaizungumzia juu kidogo, ya wale wakuu wa makuhani na mafarisayo ambao kazi yao ilikuwa ni kumvizia wamuue, ndipo akawapa mfano huo, Na kweli jitihada zao ziliishia kuangamizwa na Warumi mwaka 70 WK, ili kutimizwa ule unabii wa Yesu kuwa watazungukwa na maadui zao, watauliwa nao hawataachiwa jiwe juu ya jiwe. Mpaka leo tunavyozungumza wayahudi hawana mwelekeo wowote wa kiimani, kutokana na ile tabia yao ya kushindana na jiwe hilo.

Na jiwe hili ndilo litakalokuja kuangusha falme zote za duniani,

Danieli 2:34 “Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.

35 Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.

36 Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme”.

Nasi pia sisi tunapaswa tuwe makini sana na hii neema ya Yesu Kristo, badala ya kuliangukia jiwe hilo, au kuangukiwa nalo ni heri tujenge juu yake. Kwasababu yeye ndio mwamba salama. Tukijenga Maisha yetu kwa Kristo, basi tutayafurahia Maisha, ya hapa na kule ng’ambo tutakapovuka.

Je! Yesu yupo moyoni mwako? Kama hayupo ni heri ukamgeukia hivi sasa akufanye kuwa kiumbe kipya, na kukupa tumaini jipya la uzima wa milele. Acha kutanga tanga na hii dunia hizi ni siku za mwisho.

Bwana awabariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MWAMBA WETU.

NITAFANYA YERUSALEMU KUWA JIWE LA KUWALEMEA .

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari?”

UFUNUO: Mlango wa 14

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/04/13/naye-aangukaye-juu-ya-jiwe-hilo-atavunjika-vunjika/