Kama Malkia Esta alijipamba je! Kuna ubaya gani wanawake wa wakikristo wa leo kujipamba?.

by Admin | 18 May 2021 08:46 pm05

 Shalom!

Ni vizuri kulisoma Neno la Mungu kwa makini, huku tukimshirikisha Roho Mtakatifu, vinginevyo kwa kupitia biblia hii hii, tunaweza hata kumhalalisha shetani kuwa ni Mungu. Wako watu wanaotumia biblia hii kuhalalisha pombe, kadhalika wapo watu wanaotumia biblia hii hii kuhalalisha ndoa za jinsia moja, na wapo wanaotumia biblia hihi kuhalalaisha ndoa za mitara. Hivyo ni muhimu sana kumtumia Roho Mtakatifu katika kuyatafsiri maandiko..

2Wakoritho 3:6 “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa MAANA ANDIKO HUUA, BALI ROHO HUHUISHA”.

Sasa tukirudi katika habari ya Malkia Esta.

Malkia Esta hakwenda kupambwa kabla yakuingia kwa mfalme Ahasuero. Mfalme Ahasuero hakuwa anataka kuona uso uliopakwa make-up. Hapana!. Alichokuwa anafanyiwa Esta kwa miezi 12, sio kubadilishiwa lipstick kila siku, au hereni, au mavazi mazuri, mpaka awe mzuri.. Hapana!..Hata kwa akili za kawaida tu haileti maana. Mtu awekwe miezi 12 anapodolewa tu!..haina maana!.

Alichokuwa anafanyiwa Esta katika miezi 12, ni KUTIBIWA!.

Kumbuka wanawake waliojitokeza kutafuta nafasi ya umalkia walikuwa ni wengi, na wa madaraja yote, ndio maana hata Esta aliyekuwa daraja la chini kabisa alipata nafasi ya kuingia katika shindano lile. Sasa katika hali ya kawaida, mwanamke hata kama ni mzuri, lakini kama kaishi maisha  fulani ya chini (duni) ni lazima ngozi yake itafifia kwa sehemu Fulani, au itakuwa na mabaka kadhaa, au makovu au michubuko, na makunyanzi, haiwezi kuwa sawa na ngozi ya mtu yule ambaye hapigwi na jua yupo ndani tu siku zote.

 Sasa ili kuyaondoa hizo kasoro chache katika uso, na mabaka katika ngozi na kumrudisha mtu katika hali yake ya ASILI, yapo matibabu maalumu ambayo mtu anaweza kuwekwa chini ya hayo kwa miezi kadhaa, huku akizuiliwa pia na hari za kimaisha na baada ya kumaliza hayo, mtu Yule ngozi yake inaweza kurudi na kuwa kama ya mtoto mdogo. Na mtu akawa ni mzuri bila make-up yoyote.(Uso wake unakuwa ni mzuri lakini hauna make-up yoyote). Anakuwa anatakata, Ndicho Malkia Esta alichofanyiwa.

Esta 2:8 “Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake.

9 Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; NAYE AKAMPA UPESI VIFAA VYA UTAKASO, pamoja na posho zake, na vijakazi saba walio haki yake, wa nyumbani mwa mfalme. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake..…….

12 Basi ilipowadia zamu yake mwanamwali mmojawapo aingie kwa mfalme Ahasuero, hali akiisha KUFANYIWA SAWASAWA NA SHERIA YA WANAWAKE MIEZI KUMI NA MIWILI; YAANI, NDIVYO ZILIVYOTIMIA SIKU ZAO ZA UTAKASO, MIEZI SITA KWA MAFUTA YA MANEMANE, NA MIEZI SITA KWA MANUKATO NA VIFAA VYA UTAKASO WA WANAWAKE”

Kwahiyo alichokuwa anafanyiwa Esta tunaweza kusema hakikuwa tofauti sana na walichokuwa wanafanyiwa wakina Danieli, Shedraka, Meshaki na Abedinego, kabla ya kuingia kwa mfalme..

Hivyo Esta hakuwa anajipaka wanja kwa miezi 12, wala kubadilisha badilisha wigi kichwani mwake mpaka apate litakalomkaa vizuri, wala hakuwa anajibangua bangua ngozi kwa miezi hiyo yote, wala kubadili  hereni mpaka itakayomfaa,  wala kuvaa vinguo vya kubana, wala kushona rasta kichwani, wala kupaka rangi uso wake, wala kuweka nyusi za plastiki, au kuzichonga, wala hakuwa anaweka kucha za bandia kwa miezi 12, ndipo aingie kwa mfalme. Hata kwa akili za kawaida ni mfalme gani anataka kuona mtu mithili ya kinyago, kimeingia ndani  kwake, na tena kinyago hicho akiandae kwa miezi 12. Kama ni kujipodoa tu, siku moja tu! Ingetosha kumkamilisha Malkia Esta.

Hivyo ni muhimu kusoma maandiko kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Dada unayesoma ujumbe huu, kama unaweka wigi, fahamu kuwa unafanya jambo lisilo sahihi, kama unapaka wanja, au unajichubua ili uwe mweupe, Esta hakuwa anajichubua, kama angekuwa anafanya hivyo, ingemtosha siku mbili tu kukamilisha hilo zoezi, hivyo usidanganyike na injili za jehanamu, zinazokuambia kujichubua sio dhambi, kadhalika kama unapaka kucha rangi, au unavaa nguo za kubana, na zisizokupasa kama suruali, napenda nikushauri viache vyote hivyo kavichome moto, na wala hata usimpe mtu mwingine, kwasababu vitakupeleka jehanamu. (Mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu na si roho yako). www wingulamashahidi org.

Kama unajipenda mwili wako hujakatazwa kuutunza, utunze, ioshe ngozi yako, paka mafuta yako ya asili, kama hutaki iwe na mabaka, hujakatazwa usitembee juani, kuwa mtu wa kukaa kivulini. Lakini hakikisha unakuwa wa asili siku zote.

Wengi wa wanawake wanaosumbuliwa na roho sugu leo, wengi ni kutokana na kutoithamini miili yao. Asilimia kubwa lazima utakuta hawataki kuacha kuichafua miili yao. Wapo radhi waache kila kitu, lakini si kuacha kujipaka wanja, au kuvaa suruali na mengineyo hawataki, hivyo miili yao inakuwa ni lango la maroho kuingia na kutoka.

1Wakorintho 3:17  “Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

1Timotheo 2:9  “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10  bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?

ESTA: Mlango wa 5, 6 & 7

Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?

Mahali pa hukumu upo uovu,Na mahali pa haki upo udhalimu.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/18/kama-malkia-esta-alijipamba-je-kuna-ubaya-gani-wanawake-wa-wakikristo-wa-leo-kujipamba/