by Admin | 28 June 2021 08:46 am06
Ukweli ni kwamba hatuishi tena wakati wa mavuno, kama ilivyokuwa kipindi cha mitume. Bali tunaishi wakati wa makusanyo ya masazo. Utauliza ni kwa namna gani?
Zamani kulingana na desturi za wayahudi kulikuwa na makundi mawili ya watendaji kazi shambani, kundi la kwanza ni lile lililoajiriwa rasmi kwa kazi ya uvunaji, hilo lilikuwa linatangulia mwanzoni kabisa mwa uvunaji, na lilikuwa linavuna kila kitu kilichoonekana mbele yao.. Hivyo mpaka wafike mwisho wa shamba, walikuwa na magunia kwa magunia ya mavuno. Lakini pamoja na kuwa wanafanikiwa kuvuna mavuno mengi, bado hawakuweza kumaliza kila kitu shambani.
Hapo ndipo linaporuhusiwa kundi la pili la wavunaji, sasa tabia ya hili kundi la pili ni kuwa lenyewe linatembea likizunguka zunguka kwenye shamba lote, kuangalia walau kama kuna kitu kimebakishwa na wavunaji nyuma, wakichukue wakatumie kwa ajili ya matumizi yao na chakula. Watu hawa waliokuwa ni wale maskini waliokuwa wanaishi katika nchi na wageni (Walawi 19:9)..Kazi yao ilikuwa ni ngumu kwasababu walikuwa wanaweza kuzunguka shamba nzima lenye ekari hata 100 wakaumbulia tu kadebe kamoja cha mahindi, kwasababu mavuno mengi yalishavunwa na wanavunaji wa kwanza.
Ruthu alikuwa ni mmojawapo wa hili kundi la pili la wavunaji. Wakati ule utaona alikwenda kukusanya masazo hayo katika shamba la tajiri mmoja aliyeitwa Boazi.
Ruthu 2:2 “Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda.
3 Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki.
4 Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, Bwana akae nanyi. Nao wakamwitikia, Bwana na akubariki”.
Sasa kibiblia Wavunaji wa kwanza waliwawakilisha mitume wa Bwana. Na ndio maana utakumbuka wakati ule, wakihubiri injili kidogo tu, idadi ya maelfu ya watu ilikuwa inakuja kwa Kristo ndani ya siku moja.. Hiyo ni kuonyesha kuwa hao ndio waliokuwa wavunaji, Mungu aliowachagua.
Lakini leo hii hujiulizi licha ya kuwa kila mtu ameshasikia habari za Kristo, ameshasoma mafundisho ya mitume kwenye biblia takatifu, ameshaona miujiza mingi Kristo aliyotenda, lakini bado hawageuki, wala hawana mpango wa kutubu..hata ikitokea wamegeuka basi ni mmoja kati elfu.. Hiyo ni kuonyesha kuwa hakuna mavuno tena shambani.
Wanaopita leo hii ni akina Ruthu,(ambao ndio watumishi wa Mungu wa wakati huu) kukusanya masalio machache sana..Vinginevyo kama yasingekuwepo hadi wakati huu, Mungu angeshakuwa ameshauangamiza ulimwengu wote kwa moto. Soma
Isaya 1:9 “Kama Bwana wa majeshi ASINGALITUACHIA MABAKI MACHACHE SANA, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora”.
Ndugu kama wakati wa mavuno ya kwanza ulikupita, basi usifanye mchezo na huu wakati wa mwisho wa masalia tuliobakiwa nao, Ni neema kubwa sana tumepewa sisi, vinginevyo habari yetu ilikuwa tayari imeshakwisha..Si unakumbuka hili andiko linavyosema..
Yeremia 8:20 “Mavuno yamepita, wakati wa hari umekwisha, wala sisi hatukuokoka”.
Umeona? Lakini Mungu ameahidi yatakuwepo masalia machache sana…
Lakini hivi karibuni huduma ya Ruthu, inakwenda kuisha. Boazi wetu ambaye anamwakilisha YESU KRISTO, anakaribia kurudi shambani mwake, kukagua kazi yake.
Kristo atakaporudi, katika awamu hii, halafu akakuta bado hujaingia ghalani mwake, Ujue, adhabu yako itakuwa ni kubwa sana kwenye lile ziwa la moto siku ile. Kwasababu umejua likupasalo kutenda na hujatenda kwa wakati..
Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.
48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi”.
Unangoja nini? Unasubiri nini usimgeukie Kristo. Huu ulimwengu hauna muda mrefu sana, Kristo yupo mlangoni kurudi, dalili zote zinaonyesha, mwisho umefika, Tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa, kubali kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kwa jina la Yesu Kristo upate ondoleo la dhambi zako. Na Bwana akutie muhuri kwa Roho wake Mtakatifu, ili uwe salama katika nyakati hizi za hatari.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/28/inayoendelea-sasa-ni-huduma-ya-ruthu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.