KAMA SI YESU, HABARI YETU INGEKUWA IMEISHA ZAMANI SANA.

by Admin | 15 July 2021 08:46 am07

Jina la Bwana na mwokozi wetu, Mkuu wa uzima, Mfalme wa wafalme, Yesu Kristo libarikiwe.

Hajawahi kutokea duniani Mtu wa muhimu, na wa Baraka kama Yesu. Leo tutaangalia kwa sehemu, ni jinsi gani ni wa muhimu kwetu.

Je unajua kwa undani ni  kwanini maandiko yanasema, Bwana Yesu alipigwa kwaajili yetu?

Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”

Sio kwamba Mungu alikuwa anataka kutuhukumu ndio akaona amtafute mwanae aje kufa kwa ajili yetu Hapana! Ni kwamba tayari Mungu alikuwa ameshatuhukumu, adhabu ilikuwa imeshapitishwa.. ilikuwa ipo njiani kutufikia, na ndipo Bwana Yesu akaingilia kati kufa kwaajili yetu.

Ni sawa na mtu ambaye tayari amesharusha jiwe kumlenga mwingine, na lile jiwe wakati lipo njiani kumfikia mlengwa, anatokea mwingine kukubali kupigwa kwa niaba ya Yule aliyekusudiwa kupigwa jiwe hilo. Ndicho Bwana Yesu alichokuja kukifanya.. Hakuja kuifuta hukumu, bali alikuja kuichukua ile hukumu na kuwa yake.. ndio maana ilikuwa hana budi afe!..

Hivyo Kile kifo hakikuwa cha kwake, hakukusudiwa yeye, kilikuwa ni chetu tulikusudiwa sisi, ile aibu haikuwa ya kwake ilikuwa ni yetu!… Yale maumivu hakukusudiwa yeye, tulikusudiwa sisi, kifo cha mateso hakukusudiwa yeye, tulikusudiwa sisi.. Maana yake ni kwamba endapo, Mwokozi Yesu asingetokea.. ni kipindi kifupi sana mbele yetu kilikuwa kimebaki.. ghadhabu ya Mungu ingetumaliza wote, tungekufa kikatili na kwa aibu kama watu wa gharika, na sodoma na ghomora, tungesikitika, na kulia, na kuhuzunika, na kuteseka kwa maumivu, na hatimaye kufa na kuishia katika lile ziwa la moto.

Isaya 53:4 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

 5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

 6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote”.

Kumbuka hapo maandiko yanaposema “Ameyachukua masikitiko yetu”.. haimaanishi magonjwa yetu, wala shida zetu, wala huzuni tulizo nazo sasa, wala masikitiko tuliyonayo… La! Haimaanishi hivyo, (ingawa si kosa kutafsiri hivyo), lakini maana yake ya awali kabisa sio hiyo bali inamaanisha zile huzuni ambazo tungezipata baada ya sisi kupigwa na Bwana, na yale masikitiko ambayo tungeyapata baada ya kuipata ile adhabu ya Mungu.. yeye ndiyo kayachukua hayo.. yeye ndio atahuzunika badala yetu  baada ya kupigwa na Mungu, yeye ndiye atasikitika katika kuadhibiwa kule.. hiyo ndio maana ya kubeba masikitiko yetu..

Ndio maana kuna mahali Bwana Yesu alisema “nina huzuni nyingi kiasi cha kufa, Marko 14:34”

Umeona umuhimu wa Yesu kwetu?… Je unamthamini Bwana?.. bado tu hujaona umuhimu wa Yesu maishani mwako?

Kumbuka ghadhabu ya Mungu bado ipo, tena ina nguvu mara dufu kwa wale wote wanaoidharau kazi ya msalaba..

Waebrania 10:29 “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”

Umempokea Yesu?.. Kama bado unasubiri nini?.. kumbuka mlango wa neema hautakuwa wazi milele.. ingia leo ndani ya safina, kwa kutubu dhambi zako zote, ukimaanisha kuziacha na ubatizwe ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo, na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

HUDUMA YA UPATANISHO.

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/15/kama-si-yesu-habari-yetu-ingekuwa-imeisha-zamani-sana/