Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi injili?

by Admin | 27 August 2021 08:46 pm08

SWALI: Naomba kufahamu Wagalatia 1:8 ina maana gani? Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi?


JIBU: Tusome,

Wagalatia 1:8 “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe”.

Ni vizuri tukafahamu kwanza ni kwanini mtume Paulo alisema kauli kama hiyo. Alisema hivyo kutokana na kuzuka kwa makundi ya watu ambao walianza  kuhubiri injili nyingine tofauti na ile waliyokuwa wanaihubiri yenye kiini cha Yesu Kristo, na matokeo yake ikapelekea mpaka imani za watu wengi kupinduliwa, ambao tayari walikuwa wameshaijua njia ya kweli.

Na ndio maana mistari ya juu yake Paulo anasema..

Wagalatia 1:6 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine.

7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo”.

Unaona? na jambo la hatari zaidi ni kuwa watu hao waliowafundisha , walikuwa wanasema mambo hayo wamefunuliwa na Mungu mwenyewe, kwa kupitia maono ambayo waliletewa na malaika wa mbinguni.

Utalithibitisha pia  hilo katika.

Wakolosai 2:18 “Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, KWA KUNYENYEKEA KWA MAPENZI YAKE MWENYEWE TU, NA KUABUDU MALAIKA, AKIJITIA KATIKA MAONO YAKE NA KUJIVUNA BURE, KWA AKILI ZAKE ZA KIMWILI;

19 wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu”.

Sasa kwa namna ya kawaida ni rahisi mtu kuamini pale anapoambiwa maono hayo au maagizo hayo, yameletwa na malaika. Ni rahisi kudhani agizo hilo ni la Mungu.

Mpaka baadaye taarifa hizo zikawafikia mitume, ndipo hapo sasa tunaona mtume Paulo, akitoa maneno makali kama hayo, na kusema, “ ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe”.

Yaani akiwa na maana kuwa maono yoyote yanayosadikika yametoka mbinguni aidha kwa mkono wa malaika, au wa nabii au mitume wowote, lakini ni nje na mafundisho ya msingi ya mitume, basi na ALAANIWE.

Lakini kumbuka kauli hiyo haimaanishi kuwa malaika watakatifu wanaweza kuleta maono ambayo hayatokani na Mungu hapana, ni mapepo ndio yanayoweza kufanya hivyo. Isipokuwa tu  mtume Paulo hapo alikuwa anaweka msisitizo wa uhakika wa injili yao. Kwamba ni ya kweli na haiwezi kupinduliwa na kiumbe chochote kilicho juu mbinguni au kilicho chini duniani, kwasababu ni injili ya kweli ya Mungu mwenyezi.

Hata sasa, ndugu yangu wapo watu wanaoishi kwa maono na ndoto, wamelitupa kapuni Neno la Mungu, wapo tayari kutii kila wanachoambiwa au kusikia hata kama kinakwenda kinyume na Neno la Mungu. Kipindi hichi roho za udanganyifu zipo nyingi, na ndio maana tumeambiwa tusiziamini kila roho bali tuzipime kama zimetokana na Mungu au la!,(1Yohana 4:1 ). Utasikia mtu anasema Mungu amenifunulia,nikamwoe mke wa fulani au nikaongeze mke wa pili, na yeye bila kutathimini hayo maagizo kama yanaendana na Neno la Mungu, yeye anakwenda kufanya vile. Kumbe hajui kuwa tayari ameshapotea, anaishi katika uzinzi na siku ya mwisho atahukumiwa.

Hivyo tuwe makini sana, suluhisho pekee ni tudumu katika mafundisho ya mitume (Neno la Mungu), ndio tutakuwa salama daima. Usitishwe na maneno ya mtu yeyote anayekuambia malaika kanitokea au nimeonyeshwa maono. Lithibitishe kwanza katika Neno la Mungu. Kama linakinzana litupe kapuni, ishi kwa Neno.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika? Ina maana gani?

Nini maana ya kuabudu malaika? (Wakolosai 2:18)

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/27/ni-kwa-namna-gani-malaika-wa-mbinguni-wanaweza-kutuhubiria-sisi-injili/