Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

by Admin | 6 October 2021 08:46 am10

Tusome,

Warumi 3:22 “ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;

23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;”

Hapo maandiko yanasema “Wote wamefanya dhambi” na sio “Wote wanafanya dhambi”. Ikiwa na maana kuwa kuna dhambi ambayo imeshafanyika huko nyuma ambayo imewafanya wote wawe katika dhambi.

Na dhambi hiyo si nyingine Zaidi ya ile ya Adamu na Hawa. Maandiko yanasema kwa kukosa kwake mtu mmoja Adamu, sisi wote tumeingia katika hali ya kukosa.

Warumi 5:19 “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki”.

Umeona?..Kwa dhambi ya Adamu na sisi tunaonekana tumefanya dhambi, kwasababu tulikuwa katika viuno vya Adamu, wakati Adamu anafanya makosa hayo..Hivyo kwa dhambi yake ikafanya vizazi vyake vyote kuwa katika dhambi. Ndio maana wanadamu wote tunazaliwa na dhambi ya asili bila hata ya sisi kutaka, tunazaliwa tayari tukiwa tumepungukiwa na utukufu wa Mungu.

Ndio maana utaona mtoto anazaliwa na hasira, uchoyo, kiburi n.k.. Hiyo ni kutoka na dhambi ya asili aliyoirithi kutoka kwa Adamu. Na ndio maana maandiko yanasema “wote tumetenda dhambi” na sio tunatenda dhambi.

1 Yohana 1:8 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.

9 tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.

10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”.

Na hiyo ndio sababu pia tunamhitaji Bwana Yesu, atuondolee hiyo dhambi ya asili.

Kwasababu Kristo anafananishwa na Adamu wa pili. Maana yake kama Adamu wa Kwanza alivyotuingiza matatizoni sisi wanawe katika vizazi vyote, kadhalika Adamu wa pili (yaani Yesu Kristo), atatuingiza katika hali ya kuwa watakatifu, endapo tukimwamini na kumpokea..

Warumi 5:18 “Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.

19 Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki”.

Pale tunapompokea na tunapotubu dhambi zetu na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, tunakuwa tumezaliwa mara ya pili, na hivyo ile dhambi ya asili tuliyozaliwa nayo inaondoka. Tunakuwa watakatifu, kwasababu Kristo anashusha nguvu ya kipekee juu yetu ya kutusaidia kushinda dhambi…Hivyo tunajikuta tunaishi maisha ya utakatifu na usafi bila sheria.

1Yohana 3:9 “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba, wote walio ndani ya Kristo, dhambi haiwatawali, kwasababu wameuvua utu wa kale na kuvaa utu upya.

2Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya”.

Na ndio maana maandiko pia yanatuonyesha kuwa watakatifu waliopo duniani ndio wanaompendeza Mungu..ikimaanisha kuwa duniani kuna watakatifu.

Zaburi 16:3 “Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao”.

Je! Na wewe ni Mtakatifu?.. Umempokea Yesu na kutubu na kubatizwa ubatizo sahihi?. Kama bado kumbuka Kristo yupo mlangoni, na atakaporudi atawachukua tu wale wateule wake na kwenda nao mbinguni, yaani wale wote waliozaliwa mara ya pili, na kuishi maisha ya utakatifu. Lakini wengine waliosalia ambao hawamtaki yeye watatupwa katika lile ziwa la moto.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Je! Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

TABIA ZITAKAZOMTAMBULISHA MPINGA-KRISTO AJAYE.

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/10/06/biblia-inaposema-wote-tumetenda-dhambi-si-inamaanisha-hakuna-mtakatifu-duniani/