by Admin | 11 October 2021 08:46 pm10
Ukimtafakari yule mwanamke ambaye alitokwa na damu kwa muda wa miaka 12, na kwenda kushika pindo la vazi lake, unaweza kudhani aligundua jambo la maana sana machoni pake, au machoni pa watu waliomfuata Yesu, Jibu ni la!,
Kwa namna ya kawaida kuacha kutafuta Uso wa Yesu, unakimbilia nguo, tena sehemu ya mwisho kabisa ya nguo (pindo), ni uendawazimu na ndio maana ikambidi afanye hilo jambo kwa siri sana, kutomshirikisha mtu yeyote, hadi Yesu mwenyewe alipouliza ni nani kanigusa bado aliogopa kusema… kwasababu hata yeye mwenyewe machoni pake lilikuwa ni kama jambo la kijinga..akijua kinachofuata kama sio kugombezwa, au kuzomewa, basi ni kufukuzwa.
Lakini tunaona, Bwana Yesu alipogeuka..majibu yake yalikuwa ni tofauti, badala ya kumgombeza na kumfukiza alimwambia, “Jipe moyo mkuu”, binti yangu..kuonyesha kuwa Kristo anayathamini sana mawazo manyonge, maadamu yamekusudiwa tu kwake kwa moyo wote.
Mathayo 9:20 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.
21 Kwa maana ALISEMA MOYONI MWAKE, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.
22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile”.
Leo hii watu wengi wamekuwa na mawazo mengi ya kufanyia Mungu, Lakini wamevunjwa moyo pengine na dhamiri zao wenyewe, au na wanadamu, mpaka mawazo yale mazuri yamekufa ndani yao, wakidhani kuwa kumtumikia Mungu ni mpaka uwe askofu au shemasi. Kumbe katika mawazo hayo yanayoonekana ni ya kijinga sana, mbele za Mungu yanathamani kubwa mno, maadamu tu yameelekezwa kwake.
Hujawa mchungaji, hujawa mtume, hujawa shemasi, hujawa mwinjilisti, hujawa mwalimu, hilo lisikufanye kuona kuwa kitu kingine chochote unachoweza kumfanyia Mungu, kitakuwa hakuna umuhimu kwake..
Bwana anachokuambia leo ni kuwa JIPE MOYO MKUU. Hilo wazo ulilonalo kwake si, dogo.. pengine unaujuzi wa kuchora picha zenye jumbe tofauti tofauti za ki-Mungu, na kuzisambaza sehemu mbalimbali wazo hilo ni rahisi kudharaulika miongoni mwa watakatifu, lakini kwa Yesu, sivyo anakuambia Jipe moyo mkuu..mtumikie yeye katika hilo.
Pengine Umekuwa na wazo la kuchapisha jumbe fupi fupi, na kuzisakafia kwa karatasi gumu la plastiki, na kwenda kuzigongelea kwenye nguzo za mabarabarani..Usivunjike moyo fanya hivyo… Kama waganga wa kienyeji hawaoni shida, kwanini wewe uone haya? Jipe moyo mkuu.
Umekuwa na wazo la utengenezaji bustani kwenye nyumba za Mungu bure..fanya tu, hata kama litadharauliwa na watu. Unataka kutengeneza studio ya kurekodi kipindi vya shuhuda, bila shida fanya hivyo.. Au Unajisikia, kutoa, kitu Fulani, au mali au eneo, au uanzishe mradi Fulani ambao lengo lake kuu ni kwa ajili ya kuifikisha injili ya Bwana mbele na si kitu kingine, zidi kuitenda. N.k.
Kwasababu, huko pia kuna umuhimu mkubwa sana ambao Bwana Yesu anapafikiria pia japokuwa watu wengi hawapaoni, ni mahali ambapo panaweza kumfanya Kristo ageuke aache kuwahudumia makutano akutazame wewe na kukubariki.
Hivyo usipuuzie mawazo manyonge yaliyowahi kuingia kichwani pako kwa ajili ya Kristo. Bali yatekeleze na Bwana atakufurahia. Uwe na nia njema tu!
Kumbuka, “mwishoni mwa vazi la YESU kuna huduma na pia upo uponyaji”. Hivyo Usikae bila kufikiria ni nini utamfanyia Mungu wako angali ukiwa hapa duniani. Yeye mwenyewe alisema,
Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo”.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/10/11/jipe-moyo-mkuu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.