Hema ya kukutania ni nini, na ilikuwaje?

by Admin | 6 December 2021 08:46 pm12

Hema ya kukutania kama jina lake lilivyo, ni hema iliyotengenezwa mahususi kwaajili ya “kukutania”.

Katika biblia, Musa aliongozwa na Bwana Mungu kutengeneza Hema ndogo maalumu, ambayo kupitia hiyo, Mungu ataweza kukutana na watu wake na kuzungumza nao.

Hema hiyo Musa aliambiwa aitengeneze nje ya kambi, Na haikuwa ya kudumu, bali ya kuhama hama, kwasababu wana wa Israeli walikuwa bado wapo katika safari ya kwenda Kaanani, hivyo ilikuwa ni ya kutengenezwa na kuvunjwa. (Tazama picha juu).

Na mtu yeyote alipokuwa na jambo ambalo anataka kuuliza kwa Bwana, basi alimfuata Musa, na kisha Musa huingia ndani ya hiyo hema kusikia kutoka kwa Bwana.

Hapo awali ni Musa tu, ndiye aliyekuwa na ruhusa ya kuingia ndani ya Hema, baadaye Haruni naye alikuja kupata nafasi ya kuingia, baada ya sheria za kikuhani kuongezwa.

Na Ishara itakayoonesha kuwa Bwana ameshuka juu ya Hema hiyo tayari kuzungumza na watu wake, ni ile Nguzo ya wingu ambayo iliyokuwa inawaongoza wana wa Israeli mchana.

Nguzo hiyo iliposhuka na kukaa juu ya hema basi wana wa Israeli wote walijua Bwana ameshuka na kuna jambo au ujumbe anataka kuutoa. Nguzo hiyo kwa jina lingine iliitwa “utukufu wa Bwana”.

Hivyo uliposhuka huo utukufu basi Musa aliingia ndani ya hiyo hema kusikia Bwana anasema nini.

Mfano utaona wakati Haruni na Miriamu walipomnung’unikia Musa juu ya mke wake wakiMisri , jambo ambalo halikumpendeza Mungu…utaona “Utukufu wa Mungu”, yaani ile nguzo ya wingu ilionekana juu ya hema.

Hesabu 12:1 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.

2 Wakasema, Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao.

3 Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.

4 BWANA akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia,
Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje.

5 BWANA akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili.

6 Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto.

7 Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;

8 Kwake nitanena mdomo kwa mdomo Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?.

9 Hasira za BWANA zikawaka juu yao; naye akaenda zake.

10 Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma.

11 Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi”.

Pia unaweza kusoma juu ya habari ya Dathani na Kora walipoinuka na kutaka wao ndio wawe viongozi wa mkutano badala ya Musa.

Hesabu 16:19 “ Kisha Kora akutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote.

20 Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

21 Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja.

22 Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote?

23 BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

24 Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu”.

Mistari mingine inayozungumzia juu ya hema ya Bwana na utukufu wake huo ni pamoja na Kutoka 40:34, Walawi 1:1, na Hesabu 2:17.

Lakini je hiyo Hema ya kukutania sasa ni wapi?

Hema yetu ya kukutania sasa ni kwenye Neno la Mungu (Biblia), hapo ndipo tutakapoonana na Mungu, tutakaposikia kutoka kwa Mungu,tutakapopata maonyo na faraja. Hapo ndipo penye utukufu wa Mungu.

Hakuna mahali pengine tutakapopata kusikia Sauti ya Mungu, isipokuwa katika Neno lake.

Hivyo hatuna budi kujifunza biblia kila siku.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

MUNGU HATAZAMI MOTO WA KIGENI,KUWA MAKINI!

NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA!

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI, AU KUTOA TALAKA?

Rudi nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/12/06/hema-ya-kukutania-ni-nini-na-ilikuwaje/