MAJIBU YA MASWALI YANAYOULIZWA NA WASIO WAKRISTO (Sehemu ya kwanza).

by Admin | 26 January 2022 08:46 am01

Swali 1: Ni nani aliyemshawishi Daudi kuwahesabu Israeli ni Mungu au shetani?..Maana 2Samweli 24:1 inasema ni Mungu lakini 1Nyakati 21:1 inasema ni shetani.

Jibu: Ni shetani ndiye aliyemshawishi Daudi kwa ruhusa ya Mungu. Ayubu alijaribiwa na shetani kwa ruksa maalumu kutoka kwa Mungu. Hivyo ni sawa na kusema Mungu ndiye alimjaribu Ayubu..ni hivyo hivyo kwa Daudi pia.

Swali 02: Mungu anadanganya?maana  Ezekieli 14:9 inasema anadanganya.

Jibu: Mungu hadanganyi shetani ndiye anayedanganya, mtu mwovu anapoikataa njia ya haki, Mungu anaweza kuruhusu shetani amwingie na kumdanganya, hivyo inaweza kutafsirika kwamba kadanganywa na Mungu lakini si Mungu bali ni shetani (Soma 1Wafalme 22:20-23).

Swali 03: Nabii aliyetabiriwa na Musa kuwa atatokea si Yesu bali ni nabii mwingine kutoka Arabia,  Mohamedi (Kumbukumbu 18:15).

Jibu:

Kumbukumbu la Torati 18:15 “BWANA, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye”

Musa alikuwa mwisraeli na si Mwarabu kutoka Saudi Arabia, na ndugu zake hawakuwa waarabu bali wayahudi..Na Mohamedi hakuwa Mwisraeli bali Mwarabu.

Lakini Bwana Yesu alikuwa Myahudi na alizaliwa Israeli. Na zaidi ya yote alifanya miujiza zaidi haya ya Musa. Kwahiyo Bwana Yesu ndiye aliyetabiriwa pale na yeye ndiye Mwanzo na Mwisho hakuna mwingine. (Matendo 7:37).

Swali 04: Biblia inasema tukifika peponi tutapewa wake mara 100 ya tulionao sasa, mabikira.(Marko 10:30). Kwanini mnasema hakuna kuoa peponi?

Jibu:

Marko 10:28 “Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.

29 Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,

30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele”

Ndugu wake na ndugu waume, sio wake au waume au wachumba, bali ni ndugu wenye jinsia za kiume na za kike, na zaidi ya yote thawabu hizo ni katika ulimwengu huu huu, na sio peponi. Mbinguni hakuna kuoa wala kuolewa.(Marko 12:25)

Swali 05: Yesu alisema “kila mtu atabeba msalaba wake” iweje yeye achukue dhambi za wengine?

Jibu: Alisema “Mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake anifuate”. Marko 8:34.

Kinyozi akikwambia “ukitaka kuja kwangu kunyoa beba viwembe vyako unifuate na pia uwe tayari  kupata maumivu endapo ikitokea hitilafu”.. Je! Kwa kusema hivyo atakuwa amekataa kuchukua mzigo wako wa kukunyoa?.

Na wokovu wa Yesu ni hivyo hivyo, ukitaka  kupona, sharti ukubali gharama za wokovu. Ukikwepa gharama utakufa na dhambi zako.(Yohana 8:24).

Swali 06: Paulo kamtabiri Mohamed kupaa mpaka mbingu ya tatu 2Wakorintho 12:2, Mohamed ndiye pekee aliyefika mbingu ya tatu, Yesu hakufika huko.

Jibu: Si Mohamed aliyenyakuliwa mpaka mbingu ya tatu bali ni Paulo mwenyewe. Na Paulo aliishia hiyo mbingu ya tatu tu! Na si zaidi, lakini Bwana Yesu alifika mpaka mbingu za mbingu..ambazo hakuna aliyefika hata mmoja.

Yohana 3:13 “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu”.

Waefeso 1:20 “aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;

21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;

 22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa…”

Swali 07: Je Bwana Yesu alikuwa ni Mungu au Mwanadamu? Maana biblia inasema alikuwa ni mtu! (Matendo 2:23)

Jibu: Bwana Yesu alikuwa ni Mungu kamili katika mwili wa kibinadamu, kutimiza kusudi Fulani maalumu,

Ukivaa vazi la kiaskari na kwenda kutimiza majukumu yako ya kiaskari, utaitwa askari na vile vile utafungwa na sheria za kiaskari, lakini hiyo haikufanyi wewe usiendelee kuwa mkurugenzi katika kampuni lako uliloliacha huko nyumbani, Au haikufanyi wewe usiendelee kuwa kiongozi katika Mtaa wako au mji wako.

Na Mungu alipouvaa mwili wa kibinadamu ulioitwa Yesu, ilikuwa ni lazima aitwe mtu!  kwa kitambo lakini hiyo bado bado haimfanyi asiendelee kuwa  Mungu.

Tito 2:13 ”tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu”


Mada Nyinginezo:

FUATILIA NDOTO HII, UTAJIFUZA KITU.

KWANINI MITUME WAMUULIZE BWANA FARAGHANI?

Ni yupi aliyekuwa mkwe wa Musa kati ya Reueli na Yethro?

JE! NI DHAMBI KUIMBA WIMBO WA TAIFA?

JE! NI DHAMBI KUIMBA WIMBO WA TAIFA?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/26/majibu-ya-maswali-yanayoulizwa-na-wasio-wakristo-sehemu-ya-kwanza/