NENO LA MUNGU NI UFUNUO MKAMILIFU.

by Admin | 10 February 2022 08:46 pm02

Jina kuu la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze Biblia, (Neno la Mungu wetu), ambalo ndio taa iongozayo miguu yetu katika safari yetu ya kwenda mbinguni kwa Baba.

Neno la Mungu ni ufunuo mkamilifu zaidi ya Ndoto tuotazo au maono tuonayo..

Leo tutajifunza kwa mtu mmoja katika maandiko, aliyepokea Ndoto kutoka kwa Mungu, na jinsi alivyoipambanua na kisha tutajifunza kitu. (Na mtu huyo si mwingine Zaidi ya mke wa Pilato)

Kabla ya Bwana Yesu kusulubiwa aliota ndoto!. Na ndoto yenyewe ilikuwa inamwonesha kuwa Bwana Yesu kuwa hakustahili kupitia yale mateso. Ndoto ile ilikuwa ni ya kiMungu ikimwonesha kuwa Bwana Yesu alikuwa ni mtu wa haki, na hakustahili kwa vyovyote kusulubiwa. Na pengine labda mke wa Pilato aliota Zaidi ya mara katika  ule usiku, ikiwa na ujumbe ule ule, kuwa Bwana Yesu hapaswi kusulubiwa. (Kwasababu maandiko yanasema Mke wa Pilato aliteswa sana katika ndoto).

Mathayo 27:19 “Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, USIWE NA NENO NA YULE MWENYE HAKI; KWA SABABU NIMETESWA MENGI LEO KATIKA NDOTO KWA AJILI YAKE”.

Sasa ndoto hiyo ilitoka kwa Mungu, kwasababu kamwe shetani hawezi kumshuhudia Bwana Yesu kuwa ni mwenye Haki!..wala hawezi kujifitini mwenyewe, kwamaana huku nje kanyanyua jeshi la kutaka kumsulubisha Bwana na wakati huo huo hawezi kumpa ndoto mke wa Pilato kwamba asimsulubishe!.. ni jambo ambalo haliwezekani!. Kwahiyo ni wazi kuwa Ndoto aliyopokea Mke wa Pilato ni kutoka kwa Mungu asilimia mia.

Lakini wakati huo huo maandiko yanasema kuwa KRISTO ni lazima asulubiwe!! Afe, azikwe na siku ya tatu afufuke!.

Sasa swali ni je! Mungu anajichanganya?, huku aseme kuwa Kristo ni lazima asulubiwe na kufa na kufufuka  halafu sehemu nyingine amwoneshe mke wa Pilato kuwa Kristo ni mwenye haki hapaswi kusulubiwa?.

Jibu ni la! Mungu kamwe hajichanganyi!..isipokuwa sisi pambanuzi zetu ndizo  zinazojichanganya!..

Maandiko yanasema..

Yeremia 23:28 “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana.

 29 Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

Umeona hapo Ndoto ni MAKAPI na Neno la Mungu ni NGANO.

Ndoto na Maono vina ukweli, lakini si ukweli uliokamilika.. Ndio maana unaona hapo! Mke wa Pilato kaishia kuoneshwa tu kuwa YESU NI MWENYE HAKI HASTAHILI KUSULUBISHWA BASI!!..jambo ambalo ni kweli kabisa!… lakini kiuhalisia sio ukweli uliokamilika, ni ukweli ulio Nusu!!.. Ukweli uliokamilika ni ule unaosema “YESU NI MWENYE HAKI HASTAHILI KUSULUBIWA LAKINI KWAAJILI YA MAKOSA YETU, AMEKUBALI KUFA ILI SISI TUOKOLEWE”..Na ukweli huo huwezi kuupata kwa ndoto wala kwa maono, wala kwa ufunuo binafsi, bali unapatikana tu kwenye Neno la Mungu(biblia)… Ambalo mke wa Pilato alilikosa.. Hivyo ndoto yake ikaishia hapo “Yesu ni Mwenye haki” ikawa ni Mapaki!, ijapokuwa imetoka kwa Mungu!.. Lakini Neno la Mungu likabaki thabiti kuwa Kristo ni mwenye haki lakini lazima afe!.

Luka 9:22 “akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka”.

Je na wewe umewahi kuota ndoto za namna hiyo au zinazokaribia kufanana na hizo, kiasi kwamba ukaamini ni Bwana kazungumza na wewe ? nataka nikuambie USIRIDHIKE TU!..Kwasababu ulichokiona pengine ni ufunuo Nusu!, na si mkamilifu..

Pengine Mungu kakuonesha kwenye ndoto umenyakuliwa? Na ukaamini kuwa ni kweli utaenda mbinguni..lakini ukijitazama bado unavaa vimini, unatukana, unazungumza uongo, unaiba, unazini?.. Fahamu kuwa ndoto uliyoota pengine ni ya Mungu lakini bado ni MAKAPI!, Tafuta kuijua ngano halisi.. Ngano halisi inatufundisha endapo tukiishi maisha matakatifu ndio tutanyakuliwa, hiyo ndio ngano!.

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika HAYO NAWAAMBIA MAPEMA, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.

Hiyo ndiyo Ngano!, ambayo Mungu anaiangalia.. haijalishi umemwona malaika katika ndoto akikwambia kuwa Mungu anapendezwa na wewe!.. Kama wewe ni mwasherati, ulichokisikia kutoka kwa huyo Malaika ni makapi!.. Neno la Mungu litabaki thabiti! Kuwa utaurithi tu  uzima wa milele endapo utaacha uasherati wako, hivyo ili maono uliyoyaona yakamilike ni lazima Neno la Mungu liongezeke juu yake kwamba Uache na usherati…. Siku ile hatutahukumiwa kulingana na maono tuliyoyosikia au ndoto tulizoziota au sauti tulizozisikia au mafunuo tuliyoyapata au mahubiri tuliyoyahubiri..bali tutahukumiwa kwa NENO LA MUNGU (mambo yaliyoandikwa ndani ya kitabu cha uzima, ambacho ni BIBLIA).

Je unalithamini NENO?.. Au unaishi kwa ndoto?.. Ndoto zako ni nzuri, na pengine ni kweli zimetoka kwa MUNGU kama za yule mke wa Pilato,  lakini je! Neno la Mungu lina nafasi gani katika Maisha yako?. Jazima maono yako nyama kwa Neno la MUNGU, Jazia ndoto zako nyama kwa Neno la Mungu. Mke wa Pilato alikosa Neno tu!, ingawa alikuwa anakipawa cha ndoto, lakini ndoto zake zikawa makapi yapeperushwayo na upepo,  na sisi tusilikose Neno, ili maono yetu, ndoto zetu, funuo zetu ziwe thabiti na kamilifu.

Tenga muda mwingi sana (sio kidogo )kusoma biblia, jua nyakati na majira yaliyoandikwa kwenye biblia, tambua uweza wa Neno la Mungu, nguvu ya Neno la Mungu, jifunze kwa undani Maisha ya Bwana Yesu, soma vitabu vyote vya kwenye biblia usiache hata kimoja, tafuta sehemu mbali mbali wanazofundisha Neno la Mungu lisiloghoshiwa, jifunze hapo, linganisha mambo na mistari mbali mbali katika biblia. Na Roho Mtakatifu uliyempokea ambaye anakufunulia mambo katika ndoto atakufunulia pia na maandiko na utakuwa mwenye nguvu nyingi kiroho.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je! “Mke wa ujana wako” ni yupi kibiblia?

FAHAMU TAFSIRI ZA NDOTO MBALIMBALI.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Akawaambia Enendeni ulimwenguni mwote,MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE.(Marko16:15.) Yesu Anamaanisha nini kusema MKAIHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE?

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/10/neno-la-mungu-ni-ufunuo-mkamilifu/