NEEMA YA MUNGU KWA MARIAMU.

by Admin | 11 February 2022 08:46 am02

Karibu tujifunze Biblia.

Je umewahi kujiuliza ni NEEMA IPI MARIAMU ALIYOPEWA NA MUNGU?

Luka 1:28 “Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, ULIYEPEWA NEEMA, Bwana yu pamoja nawe.

29 Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?

30 Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, KWA MAANA UMEPATA NEEMA KWA MUNGU”.

Kwa haraka haraka ni rahisi kufikiri kuwa Neema Mariamu aliyopewa na Mungu ni yeye kumzaa BWANA YESU!.. Lakini nataka nikwambie kuwa hiyo sio neema ambayo Mungu alimpatia Mariamu. Kumzaa Bwana Yesu ni matokeo tu, ya Neema aliyopewa.

Neema kuu Mungu aliyompatia Mariamu ni “YEYE KUYAAMINI MANENO YA MUNGU”, hiyo ndio Neema kubwa ambayo hata sisi sote tunaihitaji.

Kikawaida si jambo rahisi kukubali au kuamini mtu anayekujia na kukwambia maneno ambayo hujayatazamia au kuyategemea na kuyaamini!. Lakini ilikuwa ni kinyume chake kwa Mariamu, kwani yeye aliyaamini maneno yale magumu, aliamini kuwa “ROHO MTAKATIFU ANAWEZA KUJA JUU YAKE NA AKAPATA MIMBA KIMIUJIZA PASIPO HATA KUMKARIBIA MWANAUME”. Hiyo ndiyo neema Mariamu aliyopewa!!. Si jambo rahisi kuamini hilo!.. Ukitaka kuamini kuwa si jambo rahisi mkumbuke Zekaria, baba yake Yohana Mbatizaji.

Malaika huyo huyo aliyemtokea Mariamu, alimtokea kwanza Zekaria na kumpa taarifa kama hizo hizo alizompa Mariamu, tena zake zilikuwa ni nyepesi kuliko za Mariamu, kwasababu yeye aliambiwa tu!, atakutana na mke wake Elizabeth na katika uzee wao watapata mtoto kama vile Ibrahimu na Sara walivyopata mtoto katika uzee wao.

Lakini ijapokuwa Zekaria alikuwa ni kuhani, ambaye angepaswa awe na Imani kubwa kuliko Mariamu, na tena ijapokuwa anao ushuhuda kama huo katika maandiko (Habari ya Ibrahimu na Sara), lakini tunaona bado hakumwamini Gabrieli? Mwishowe Malaika yule akakasirika na kumpiga Ububu, mpaka lile neno lilipotimia.

Hebu tusome kidogo..

Luka 1:7 “Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.

8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,

9 kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.

10 Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.

11 Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.

12 Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.

13 Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.

14 Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake………..

18 Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.

19 Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.

20 Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake”.

Hapo Zekaria hakuambiwa kuwa “mke wake atachukua mimba kimiujiza” kama alivyoambiwa Mariamu.. lakini ilikuwa ni kizaazaa, hakumwamini yule Malaika mpaka akapigwa ububu!!… sasa hebu jiulize kama yule Malaika angempa taarifa ngumu kama za Mariamu kuwa “mke wake atachukua mimba kimiujiza bila kukutana naye” ingekuwaje!..si angeweza hata kumlaani yule Malaika pale pale, na pengine Zekaria angepigwa kwa pigo kubwa kuliko hilo la ububu!!.

Kwahiyo unaweza kuona Neema Mariamu aliyopewa ni “KUYAAMINI MANENO YA MUNGU KWA ASILIMIA ZOTE”..Jambo ambalo ni Zuri sana!.

Walikuwepo mabikira wengi pale Yerusalemu na Nazareth, lakini Malaika Gabrieli hakutumwa kwao, kwasababu taarifa hizo zilikuwa ni ngumu kuaminika!..

Bwana Yesu alisema maneno haya mahali Fulani..

Luka 4:24 “Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.

25 Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima;

26 WALA ELIYA HAKUTUMWA KWA MMOJAWAPO, ILA KWA MJANE MMOJA WA SAREPTA KATIKA NCHI YA SIDONI”.

Mwanamke wa Sarepta anafananishwa na Mariamu. Kwani Mwanamke wa Sarepta aliyaamini maneno ya Nabii Eliya kwa asilimia zote, aliamini kwamba inawezekana kabisa Mungu kumlisha kwa unga mdogo uliobakia kwa kipindi cha miaka mitatu au hata 10..kama vile Mariamu alivyoamini kuwa inawezekana yeye kupata ujauzito kimiujiza.

1Wafalme 17:8 “Neno la Bwana likamjia, kusema,

9 Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.

10 Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.

11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.

12 Naye akasema, KAMA BWANA, MUNGU WAKO, AISHIVYO, SINA MKATE, ILA KONZI YA UNGA KATIKA PIPA, NA MAFUTA KIDOGO KATIKA CHUPA; NAMI NINAOKOTA KUNI MBILI ILI NIINGIE NIJIPIKIE NAFSI YANGU NA MWANANGU, TUULE TUKAFE.

13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.

14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, LILE PIPA LA UNGA HALITAPUNGUKA, WALA ILE CHUPA YA MAFUTA HAITAISHA, HATA SIKU ILE BWANA ATAKAPOLETA MVUA JUU YA NCHI”.

Huyu Mwanamke wa Sarepta alipata Neema kama tu ya Mariamu.

Sasa ni kitu gani kiliwafanya hawa wanawake wapate Neema ya kumwamini Mungu, kuliko wanawake wote walio waliokuwepo Israeli?.

Biblia inatupa majibu katika…

1Petro 5:5 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote JIFUNGENI UNYENYEKEVU, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU HUWAPINGA WENYE KIBURI, LAKINI HUWAPA WANYENYEKEVU NEEMA.

6 BASI NYENYEKEENI CHINI YA MKONO WA MUNGU ULIO HODARI, ILI AWAKWEZE KWA WAKATI WAKE;

7 huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”.

Umeona hapo, kanuni ya kupata Neema kutoka kwa Mungu?… ni KUJIFUNGA UNYENYEKEVU!!!.. Kujishusha siku zote!, mbele za Mungu na wanadamu, unakuwa mdogo kuliko wote!, unakuwa tayari kuwatumikia wengine Zaidi ya wewe kutumikiwa!!

Mariamu alikuwa anazo hizo sifa!.. Biblia haijaeleza kwa urefu Maisha yake, lakini tunaweza kupata dondoo chache za jinsi Maisha yake yalivyokuwa katika mistari ifuatayo..(Zingatia vipengele vilivyoanishwa kwa herufi kubwa).

Luka 1:46 “Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47 Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;

48 Kwa kuwa AMEUTAZAMA UNYONGE WA MJAKAZI WAKE. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;

49 Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.

50 Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha.

51 Amefanya nguvu kwa mkono wake; AMEWATAWANYA WALIO NA KIBURI KATIKA MAWAZO YA MIOYO YAO;

52 AMEWAANGUSHA WAKUU KATIKA VITI VYAO VYA ENZI; NA WANYONGE AMEWAKWEZA.

53 Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu”.

Hebu tuyajadili haya maneno ya Mariamu kwa ufupi ili tujue kama kweli alikuwa mnyenyekevu au la!! (Hapo yapo mambo makuu matatu!).

 1. AMEUTAZAMA UNYONGE WA MJAKAZI WAKE:

Kwa maneno haya, kumbe Mariamu alikuwa anaonekana mnyonge mbele za watu, hakuwa mwanamke aliyejikweza..

 2. AMEWATAWANYA WALIO NA KIBURI KATIKA MAWAZO YA MIOYO YAO.

Maana yake Mariamu yeye hakuwa na kiburi!, ndio maana kasema maneno hayo.. na maandiko yanasema, Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa wanyenyekevu Neema.(Rejea 1Petro 5:5).

 3. AMEWAANGUSHA WAKUU KATIKA VITI VYAO VYA ENZI; NA WANYONGE AMEWAKWEZA.

Maneno haya yanathibitisha tena kuwa Mariamu alikuwa mnyonge!, ndio maana Mungu akamkweza.

Hivyo Kwa hitimisho ni kwamba ili na sisi tupewe NEEMA kama ya Mariamu, au kama ya wengine wengi ya KUYAAMINI MANENO YA MUNGU, na hatimaye kufanya makubwa..hatuna budi tuwe wanyenyekevu. Tukubali kujihusisha na mambo manyonge, mambo madogo!.. Tusijione sisi ni bora mbele za Mungu, tukiwa watu wa namna hiyo basi Mungu atatuongezea NEEMA ZAIDI, na tutajikuta tunafanya makubwa sana.

Unapokuwa kanisani, jifunze kujishughulishe na yale mambo ambayo yanayoonekana yanadharaulika kuliko yote!, siku moja utaona matokeo yake, Zekaria alikuwa anajulikana na wakuu, tena anafanya kazi ya ukuhani lakini maneno ya Gabrieli yalimchanganya…wakati huo huo Mariamu ambaye pengine alikuwa anadumu tu katika kusali na kuomba!, na kujisitiri na kujishusha, na kuwaombea wengine, anakuja kupewa Neema kubwa ya kuyaamini maneno makuu ya Mungu.

Bwana atusaidie, Bwana atupe unyenyekevu, Bwana atuongezee Neema yake.

Bwana wetu yu aja!.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/11/neema-ya-mungu-kwa-mariamu/