USIWE ADUI WA BWANA

by Admin | 17 February 2022 08:46 am02

Kuna siku Fulani nikiwa nasafiri kwenye gari, nikamsikia mtu fulani kwenye redio akisema “Rafiki wa adui yako ni Adui yako”..akimaanisha kuwa “mtu yeyote ambaye atashirikiana na yule mtu anayekupinga wewe, au anayekuchukia au anayekupiga vita basi huyo naye pia ni adui yako”..Haijalishi hakujui wewe wala hajawahi kukutana na wewe, wala hajawahi kukuona..kitendo tu cha kuwa Rafiki wa adui yako, tayari ni yeye kashafanyika kuwa adui wako.

Usemi huo ni wa kidunia lakini una kauhalisia fulani ndani yake..

Hebu tusome maandiko yafuatayo..

Yakobo 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba KUWA RAFIKI WA DUNIA NI KUWA ADUI WA MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu”

Hapo maandiko yanasema.. “Kuwa rafiki wa dunia” tayari wewe ni adui wa Mungu…Maana yake haijalishi hujawahi kumwona Mungu wala kumsikia, au kukutana naye, haijalishi hujawahi kulikufuru jina lake, wala kumtukana. Kitendo cha wewe tu kuwa Rafiki wa ulimwengu tayari umeshakuwa adui yake!.

Na hiyo ni kwanini?

Kwasababu ulimwengu upo kinyume na Mungu siku zote, anasa zote zinautukuza ufalme wa giza, Fahari zote za kidunia zinautukuza ufalme wa giza ambao upo chini ya shetani, na ufalme wa giza wote upo kinyume na ufalme wa Nuru wa Mungu.

Luka 4:5 “Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja.

6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo”.

Ndugu fahamu kuwa unapokuwa Rafiki wa mambo ya kidunia tayari wewe ni umeshakuwa adui wa Mungu. Unapokuwa Rafiki wa tamthilia za kidunia tayari wewe ni adui wa Mungu, haijalishi kinywani unakiri wewe ni Rafiki wa Mungu… Neno lake linasema wewe tayari ni adui yake.

Unapokuwa Rafiki wa filamu za kidunia, wewe ni adui wa Mungu, Unapokuwa Rafiki wa michezo ya kidunia kama kubeti, kupambana ndondi, karate, mipira, n.k wewe ni adui wa Mungu kwasababu michezo hiyo ipo kinyume na Mungu, na inamtukuza shetani.

Unapokuwa rafiki wa miziki ya kidunia, wewe tayari ni adui wa Mungu, haijalishi hujawahi kumtukana Mungu kinywani mwako, tayari wewe ni adui yake, kadhalika unapokuwa Rafiki wa starehe na anasa zote za kidunia umeshajifanya mwenyewe kuwa adui wa Mungu. Huhitaji kutangaza kinywani kwamba wewe ni adui wa Mungu, kitendo tu! Cha kuwa Rafiki wa ulimwengu, wewe tayari ni adui yake.

Na madhara ya kuwa adui za Mungu, ni kuitazamia ni kuitazamia ghadhabu ya Mungu itakayoijia ulimwengu na hata baada ya ulimwengu katika ziwa la moto.

Yeremia 46:10 “Maana hiyo ni siku ya Bwana, Bwana wa majeshi, SIKU YA KISASI, ILI AJILIPIZE KISASI JUU YA ADUI ZAKE; Nao upanga utakula na kushiba, Utakunywa damu yao hata kukinai; Maana Bwana, Bwana wa majeshi, ana sadaka yake Katika nchi ya kaskazini karibu na mto Frati”.

Na tena linasema..

Nahumu 1:2 “Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; BWANA HUJILIPIZA KISASI JUU YA ADUI ZAKE, HUWAWEKEA ADUI ZAKE AKIBA YA HASIRA”.

Umeona? Bwana ameahidi kuwaharibu maadui zake.. Na maadui zake ni akina nani?.. Ni wale wote walio “Rafiki wa ulimwengu”.

Je wewe ni adui wa Bwana kwa kuupenda kwako ulimwengu?.. Kama ndio kwanini leo usifanyike Rafiki wa Bwana kwa kujitenga mbali na ulimwengu, na anasa zake zote, na Fahari zake zote?.. Bwana Yesu aliukataa ulimwengu mbele ya shetani!, na sisi hatuna budi kuukataa Dhahiri, na Bwana huyo huyo, aliyeukataa ulimwengu mbele ya shetani, alituachia na sisi Neno hili la kutafakari..

Marko 8:36 “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?”

Kama leo hii umeamua kuisalimisha roho yako kwa Kristo, bali uamuzi utakaouchukua ni mwema, ambao hautaujutia Maisha yako yote. Basi hapo ulipo jitenge binafsi, sehemu ya utulivu. Kisha piga magoti na kufuatisha sala hii fupi ya Imani.

Sema Bwana Yesu, ninakuja leo mbele zako, nimetambua mimi ni mwenye dhambi, na nilikuwa adui yako pasipo kujujia, leo hii ninatubu dhambi zako zote nilizotangulia kuzifanya, na zile nilizokuwa nimepanga kukuzifanya. Natubu kwa kumaanisha kuziacha!, ingia ndani yangu leo. Ninakiri kuwa wewe ni Bwana na Mwokozi wa Maisha yangu!, na kwamba ulikuja kufa kwaajili yangu, ukafufuka na utarudi tena kuwachukua wateule wako, nisaidie niwe miongoni mwa wale utakaokuja kuwachukua siku ile.

Leo hii ninamkataa shetani na kazi zake zote!.. ninaukataa ulimwengu na kazi zake zote!..ninakataa unasa, na ushabiki mambo yote ya kiulimwengu!, na urafiki wa mambo yasiyofaa, yanayoniweka mbali nawe Bwana wangu.

Roho Mtakatifu karibu ndani yangu leo, nisaidie na niongoze katika kuijua kweli yote na kuushinda ulimwengu. Asante Bwana Yesu kwa kunisamehe na kuniingiza katika neema yako.

Amen!

Ikiwa umefuatisha sala hii yote kwa Imani, tayari Bwana Yesu kaingia ndani yako, kuanzia sasa yupo tayari kukupeleka katika hatua nyingine kiimani. Unachopaswa kufanya ni kujitenga mbali na vichocheo vyote vya dhambi, mfano kama simu yako ina miziki, au mipira, tamthilia, filamu, picha za ngono au link za kubet, zifute zote wakati huu, ili umpe Roho Mtakatifu nafasi ya kukupeleka viwango vingine, kadhalika kama ulikuwa na kampani za marafiki zipunguze, au anza kuzungumza nao Habari za wokovu tu!.

Na mwisho kabisa unapaswa ubatizwe ili ukamilishe hatua ya mwisho ya wokovu wako, ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, Hivyo mapema sana tafuta mahali sahihi ukabatizwe, na kama utahitaji msaada huo wa ubatizo basi wasiliana nasi kwamba namba hapo chini, tutakusaidia kwa hilo.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Nini maana ya vifungeni viuno vya Nia zenu? (1Petro 1:13).

KUWA RAFIKI WA DUNIA NI KUWA ADUI WA MUNGU.

 Je kualikwa kwenye sherehe za watu ambao si wakristo ni dhambi?

KUWA RAFIKI WA DUNIA NI KUWA ADUI WA MUNGU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/17/usiwe-adui-wa-bwana/