Nini maana ya huu mstari? “Yeye mwenyewe ataokolewa lakini ni kama kwa moto”

by Admin | 7 March 2022 08:46 pm03

Tusome,

1 Wakorintho 3:11 “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.

12 Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri.

13 Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani.

14 Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu

15 Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ILA YEYE MWENYEWE ATAOKOLEWA; LAKINI NI KAMA KWA MOTO.”.

Awali ya yote ni muhimu kufahamu aina za Hukumu za Mungu.

Kuna aina kuu mbili (2) za Hukumu; 1)Hukumu ya Waovu na 2)Hukumu ya watakatifu.

Hukumu ya waovu ni ile inayotajwa katika Ufunuo 21, ambayo inajulikana kama hukumu ya kiti cheupe cha Mungu. Katika hukumu hii, wafu wote waliokufa katika dhambi watafufuliwa na kuhukumiwa kulingana na matendo yao mabaya waliyokuwa wanaifanya…

Kadhalika ipo hukumu ya Watakatifu, ambayo hii itakuwa mbinguni.

Hii haitakuwa hukumu ya kulaumiwa bali ya thawabu.. Wale walioshinda watasimamishwa mbele za Bwana na kila mtu atapewa thawabu kulingana na utumishi wake hapa duniani. Waliofanya vizuri watapewa thawabu kubwa na wale ambao hawakufanya vizuri sana watapewa thawabu kidogo na wengine hawatapewa kabisa.. Ingawa wataingia mbinguni kwasababu walikuwa watakatifu!.

Hivyo hukumu hiyo inayozungumzwa hapo katika (1 Wakorintho 3:13) ya kazi ya kila mtu kupimwa kwa Moto!, sio hukumu inayowahusu waovu!,  la! bali inayowahusu wale walioshinda, (watakatifu) ambao wataingia mbinguni..

Kwahiyo hawa walioshinda kama huku duniani walikuwa watakatifu lakini katika eneo la utumishi, hawakufanya vizuri..(maana yake waliyapunguza maneno ya Mungu, hawakuwafundisha watu kweli yote)…aidha kutokanana na hofu fulani, au kuhofia shinikizo Fulani..basi siku ile watapata hasara kubwa sana mbinguni.

Kwamfano utaona kuna watu wanajua kabisa, kuwa pasipo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu, lakini baada ya kujua hayo, wanaogopa kuwasisitiza watu wawe watakatifu mwilini na rohoni kama wao walivyo, wakihofia kuwakwaza wale watu..utaona wanawaambia tu! Juu juu lakini kamwe hawazami ndani kuwaeleza madhara ya kutokuwa watakatifu. Mwisho wanajikuta wanatengeneza watu wengi ambao hawataenda mbinguni siku ya mwisho, kwasababu ni vuguvugu..bali watatupwa katika ziwa la moto.

Biblia inasema maneno ya Mungu ni kama Moto. Kwahiyo siku ile matunda yao yote yatajaribiwa kwa moto.. (watu wote waliowahubiria wao)..

Sasa moto ni nini?

Biblia inasema maneno ya MUNGU NDIO MOTO!

Yeremia 23:29 “Je! NENO LANGU SI KAMA MOTO? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

Na mfano wa maneno ya Mungu ambayo ni moto ni haya…

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, KATIKA HAYO NAWAAMBIA MAPEMA, KAMA NILIVYOKWISHA KUWAAMBIA, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU.”

Mtu yeyote tuliyemhubiria atajaribiwa kwa Maneno hayo katika siku ile ya Mwisho.. Na kama atafaulu kipimo hicho, maaana yake ataingia mbinguni, kule tulipo sisi, na hivyo sisi tuliyemhubiria tutapata faida!..hapo ndio litatimia hilo neno (… Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu).

Lakini matunda tuliyoyahubiria yakifeli hicho kipimo cha maneno hayo, basi yatatupwa katika ziwa la moto na sisi tuliyoyahubiria tutapata hasara!, (hakuna thawabu yoyote tutakayopewa)..na ndio litatimia hilo neno… “Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

Sasa kwanini hapo iseme..“Ataokolewa lakini kama kwa moto” ??

Kikawaida mtu anapopata hasara, na huku alitegemea kupata faida! Moyoni hatafurahia sana..tofauti na yule ambaye alitegemea kupata faida na kule akakuta kapata faida kubwa Zaidi.

Hivyo yule aliyepata hasara lakini kaokolewa, ataingia mbinguni huku akiwa amekosa vile alivyovitarajia,(maana alitarajia thawabu kubwa lakini hakuzipata) hivyo hiyo hali ya kukosa vile alivyovitarajia na huku anaona wengine wakivishwa mataji ya ushindi ndio inaitwa “kuokolewa kama kwa moto”.

Baadhi ya dini zinatumia andiko hili kuhalalisha Imani ya “toharani” kwamba mtu akifa katika dhambi, anaweza kupitishwa kwenye mateso ya moto kwa kitambo kichache kisha akatolewa kule.. kwasababu hapo imesema ..“Ataokolewa lakini kama kwa moto”.

Imani hiyo ni Imani potofu, kutoka kwa yule adui shetani, hakuna nafasi ya pili, kwa mtu atakayekufa katika dhambi (Waebrania 9:27). shetani kalipandikiza hilo fundisho katika baadhi ya dini, ili watu wastarehe katika dhambi huku wakiamini kwamba hata wakifa katika dhambi zao, basi ipo nafasi ya pili.. watapitishwa kwenye moto kidogo kisha watatolewa siku moja.

Usidanganyike, wala tusidanganyike!..mtu akifa leo katika dhambi, Habari yake imeisha..atakachotazamia ni hukumu na kisha kutupwa katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti.

Je! Na wewe leo unahubiri injili gani?..unajenga jengo la namna gani?, la nyasi, fito au Mawe ya thamani.

Mawe ya thamani ni wale watu wanaosikia injili ya kweli isiyoghoshiwa, ambayo haujachanganywa na chochote.

Nyasi na fito ni wale watu ambao wanahubiriwa kuwa Mungu haangalii mwili anaangalia tu roho!, ni wale wanaohubiriwa mambo ya ulimwengu tu, hawahubiriwi juu ya hatima ya roho zao.

Je na wewe unatengeneza watu wa namna gani?, unajenga jengo gani?

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Walakini ataokolewa kwa uzazi wake.

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 2)

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 2)

Nini maana ya ‘Hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma’?

Kwanini Paulo, alihukumu wakati hukumu hairuhusiwi?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/03/07/nini-maana-ya-huu-mstari-yeye-mwenyewe-ataokolewa-lakini-ni-kama-kwa-moto/