VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.

by Admin | 27 April 2022 08:46 am04

Jina la Bwana Yesu Kristo, Mkuu wa Uzima, libarikiwe.. karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu, ambalo ni taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Je unajua ni kwanini baadhi ya watu waovu, Mungu anaruhusu wafanikiwe katika ulimwengu huu, ijapokuwa wanalikufuru jina lake? Siri ipo katika mistari ifuatayo..

Mathayo 13:24 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

29 AKASEMA, LA; MSIJE MKAKUSANYA MAGUGU, NA KUZING’OA NGANO PAMOJA NAYO.

30 VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO; NA WAKATI WA MAVUNO NITAWAAMBIA WAVUNAO, YAKUSANYENI KWANZA MAGUGU, MYAFUNGE MATITA MATITA MKAYACHOME; BALI NGANO IKUSANYENI GHALANI MWANGU”.

Nataka tuone huo mstari wa 30 unaosema.. “VIACHENI VYOTE VIKUE”..

Hili ni Neno kubwa sana.. Yaani Mungu anaruhusu Magugu yasitawi ndani ya shamba lake?.. Si ajabu leo unaona waovu wanasitawi katika dunia yake, si ajabu unaona leo wachawi wanavuna, wauaji wanafanya biashara na kufanikiwa, waabudu sanamu wanaishi miaka mingi, walevi wanastawi katika dunia hii hii, wanayoishi watu wanaomcha Mungu.

Ukiona hivyo usishangae, kwasababu ni Mungu karuhusu wasitawi, wao ni magugu kati ya Ngano, ndani ya shamba lake, na Mungu kazuia wasiondolewe kwanza bali wakue Pamoja na Ngano, hata wakati wa mavuno, maana yake zile baraka za kumwagiwa maji na kuwekewa mbolea wacha nao wazifaidi mpaka wakati wa mavuno, na utakapofika wakati wa mavuno zitangamizwa milele..(Kwahiyo kumbe lengo la kuacha magugu yakue Pamoja na ngano, ni ili mwisho wa siku magugu hayo yale kuangamizwa)

Ndio maana sasa Daudi akasema maneno haya…

Zaburi 92:7 “Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele”

Na Sulemani mwanae pia akasema…

Mithali 1:32 “…kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”

Katika siku hizi za mwisho shetani anawafanya watu waangalie hali zao za kimaisha, na kuzifanya kuwa kipimo cha kwanza cha hali zao za kiroho. Kwamba ukipata mafanikio mengi basi ni Mungu kakubariki, na vile vile usipokuwa na mafaniko basi kuna tatizo, kwamba upo mbali na Mungu, Kufuatia 3 Yohana 1:2.

Ni kweli hali za kimaisha ni kipimo cha hali ya kiroho, lakini kipimo hichi si thabiti asilimia mia, kwasababu kuna matajiri wengi watakuwepo kuzimu, na vile vile kuna maskini wengi watakuwepo mbinguni (kasome Luka 16:19-31).

Hivyo kukubaliwa kwetu na Mungu hatukupimi kwa mafanikio, kwasababu yeye mwenyewe alisema “VIACHENI VYOTE VIKUE PAMOJA”. Ili wakati wa mavuno viangamizwe.

Sasa swali kama Mafanikio sio kipimo thabiti cha kukubaliwa na MUNGU, je kipimo thabiti kitakuwa ni kipi?

Kipimo kamili ni UTAKATIFU….Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana MTU ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO”.

Hicho ndio kipimo ambacho, kipo thabiti asilimia mia..Maana yake ukiwa mtakatifu utamwona Mungu, usipokuwa mtakatifu hutamwona Mungu, hakuna ambaye ataenda kuzimu akiwa mtakatifu..wala hakuna ambaye ataenda mbinguni kama si mtakatifu.. Tofauti na kipimo cha kwanza ambacho hakieleweki sana..kwasababu wapo matajiri kuzimu, na maskini mbinguni.

Kama ni hivyo, basi huu si wakati wa kutafuta kwanza mafanikio ya mwilini, bali wa kutafuta kwanza Utakatifu, ili tukae mbali na dhambi..kwasababu dhambi ndiyo itakayotutenga na Mungu milele.

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, KATIKA HAYO NAWAAMBIA MAPEMA, KAMA NILIVYOKWISHA KUWAAMBIA, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

Je! Ni kweli Yesu alirejesha kila kitu kama pale Edeni?

 MAVUNO NI MENGI

MWISHO WA MAVUNO, NI MWISHO WA DUNIA.

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/04/27/viacheni-vyote-vikue-hata-wakati-wa-mavuno/