MAUTI NA KUZIMU ZIKAWATOA WAFU WALIOKUWAMO NDANI YAKE.

by Admin | 4 May 2022 08:46 am05

SWALI: Kwanini watu watakaohukumiwa siku ile ya mwisho, wanaonekana kutofautishwa katika sehemu mbili, wengine watatokea “baharini”, na wengine katika “mauti na kuzimu”. Kwanini iwe hivyo na tofauti ya maeneo hayo ni ipi?

Ufunuo 20:11 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.

12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.

13 BAHARI IKAWATOA WAFU WALIOKUWAMO NDANI YAKE; NA MAUTI NA KUZIMU ZIKAWATOA WAFU WALIOKUWAMO NDANI YAKE. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto”.


JIBU: Hukumu ya mwisho kabisa ni hukumu ijulikanayo kama “hukumu ya kiti cheupe cha enzi cha mwanakondoo”. Ni hukumu inayokamilisha wafu wote walioko makaburini, mbali na watakatifu.

Haitachagua wakubwa, wala wadogo, vijana au wazee. Waovu wote watafufuliwa wakati huu na kila mmoja atahukumiwa sawasawa na matendo  yake, kisha atatupwa katika lile ziwa la moto, aangamie huko milele.

Lakini biblia inatuonyesha siku hiyo waovu hao watatoka sehemu kuu mbili,

  1. ya kwanza, ni habarini,
  2. na ya pili ni Mauti na Kuzimu.

Kumbuka, lugha iliyotumika hapo ni lugha ya kinabii, na sio halisi kabisa kwamba bahari inayo wafu wake. Hapana.

Je Bahari ikawatoa wafu waliokuwa ndani yake, kunamaanisha nini?.

Tukianzana na wafu waliokuwa baharini. Tabia ya bahari sikuzote ni kubwa, haina mwisho, ukipotea humo, umepotea moja kwa moja. Na kibiblia maji mengi(bahari) inamaanisha ulimwengu.

Ufunuo 17:15 “Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha”.

Hii ikiwa na maana sikuile ya mwisho, wafu wote, yaani waovu wa mataifa yote, wa lugha zote, waliokufa tangu Adamu, hadi wakati wa kurudi kwa Bwana Yesu kulinyakuwa kanisa lake (siku ya unyakuo). Wote hao watakuwa katika kundi la wafu watokao baharini. Watafufuliwa na kuhukumiwa.

Mauti na kuzimu kulifunua nini?

Lakini mara baada ya unyakuo kupita. Kuna tukio lingine litafuata, ambalo linajulikana kama dhiki kuu.

Kipindi  hichi kinajulikana kama kipindi cha utawala wa shetani(mpinga-kristo), watu wengi sana watauliwa, kutokana na dhiki ambayo Mungu ataruhusu shetani aisababishe, kwa waovu wote, watakaobakia duniani. (Tukiachia mbali wale ambao watakataa chapa ya mnyama). watauawa.

Ukisoma Ufunuo 6:8 inasema.

“Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda JINA LAKE NI MAUTI, NA KUZIMU AKAFUATANA NAYE. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi”.

Umeona huyu farasi wa kijivujivu anaitwa mauti, akiambatana na kuzimu. Ambaye ni ibilisi akifanya kazi yake wakati huo. Naye atasababisha vifo vya robo ya watu waliopo duniani wakati huo. Kwamfano kwa dunia ya sasa ni Zaidi ya watu BILIONI 2, watauawa, na hiyo itakuwa ni katika mapigo ya ghadhabu ya Mungu, na vita vya Harmagedoni, na magonjwa, na wote hawa watakaokufa  moja kwa moja watakuwa chini ya “Mauti na kuzimu”.

Sasa biblia inaposema Mauti na Kuzimu ikatoa wafu wake, umeshaelewa kuwa ni wafu waliokufa katika hichi kipindi cha Dhiki kuu, ambao kimsingi walikuwa chini ya mpanda farasi wanne, aliyeitwa mauti na kuzimu.

Sasa kwanini sehemu zote mbili zitajwe?

Ni kuonyesha kuwa hukumu hiyo haitambakisha mfu hata mmoja. Itakuwa ni hukumu ya ulimwengu mzima kwa wale ambao hawakunyakuliwa, Au kuikataa cha ya mnyama.

Ikiwa leo hii umekufa kama mlevi, au fisadi, au kihaba, utakapokufa utakwenda katika Habari la kiroho. Lakini ikiwa utakufa katika dhiki kuu, vilevile utakwenda katika katika mauti na kuzimu. Na wote siku ya mwisho mtafufuliwa. Na kuhukumiwa, kila mmoja kwa kipimo chake. Kisha mtatupwa katika ziwa la moto.

Ndugu, hukumu ya Mungu ni ya kuiogopa sana, kwasababu hakuna nafasi ya pili baada ya kifo. Ukifa leo ghafla, ni moja kwa moja jehanamu ukisubiria siku hiyo ya ufufuo ifike, Kwanini hayo yote yatukute? Watu walio kuzimu leo hii Ni kilio na majuto ndivyo vinavyoendelea, wanatamani wangepata hata dakika 2 za kutubu lakini hawana. Wewe muda unao. Lakini unafurahia ulimwengu.

Mgeukie Kristo, leo akusamehe dhambi zako. Tubu kwa kumaanisha kabisa kuuacha ulimwengu na tamaa zake zote. Dhamiria kumfuata Yesu, naye atakuokoa, katika dakika hizi za majeruhi. Kumbuka Unyakuo ni wakati wowote, hilo linafahamika. Muda umeisha, dalili zote zimeshatimia. Mlango wa neema kwa mataifa hivi karibuni utafungwa.

Bwana atusaidie.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

MAOMBOLEZO YA HADADRIMONI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita.

MPINGA-KRISTO

UTAWALA WA MIAKA 1000.

JE MGOGORO WA URUSI NA UKRAINE,UMETABIRIWA KIBIBLIA?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/05/04/mauti-na-kuzimu-zikawatoa-wafu-waliokuwamo-ndani-yake/