Ni lini na wapi Ibrahimu aliiona siku ya Bwana akashangilia?.

by Admin | 11 May 2022 08:46 am05

Tusome,

Yohana 8:56 “Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi”.

Jibu: Siku aliyoiiona Ibrahimu sio siku Kristo anamwaga damu yake pale Kalvari, kwaajili ya ondoleo la dhambi ya ulimwengu..

Sasa ni lini Ibrahimu aliiona hiyo siku?

Aliiona hiyo siku wakati anakutana na Melkizedeki, mfalme wa Salemu. Melkizedeki  maandiko yanasema alikuwa KUHANI WA MUNGU ALIYE JUU. (Hapa ndipo siri ya furaha ya Ibrahimu ilipokuwepo).

Melkizedeki alimjia Ibrahimu kama mtu, akiwa na mkate na Divai mkononi mwake, na akampatia Ibrahimu mkate ule na divai ile. Sasa Melkizedeki alikuwa ni Bwana Yesu Mwenyewe, aliyemtokea Ibrahimu kwa sura nyingine, na kwa umbile lingine, kabla ya wakati..

Waebrania 6:20 “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki”.

Ndio maana, Bwana Yesu aliwaambia Wayahudi, kwamba kabla ya Ibrahimu kuwapo yeye (Yesu) alikuwapo..

Yohana 8:57 “Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?

58 YESU AKAWAAMBIA, AMIN, AMIN, NAWAAMBIA, YEYE IBRAHIMU ASIJAKUWAKO, MIMI NIKO.

59 Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni”

Kwahiyo tumeshaona kuwa aliyekutana na Ibrahimu alikuwa ni Bwana Yesu mwenyewe katika mwili. Lakini utaona huyu Melkizedeki (Kristo), alipokutana na Ibrahimu, hakumpa nyumba, wala mali, wala fedha, wala kingine chochote, bali alimpa MKATE na DIVAI.

Sasa huo Mkate na Divai Ibrahimu aliopewa na Melkizedeki.. ulikuwa ni ufunuo wa Mwili na Damu ya Yesu ambao atakuja kuutoa baadaye kwaajili ya uzima wa ulimwengu..

Yohana 6:51 “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

52 Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?

53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake ”.

Hiyo ndiyo sababu kwanini Bwana Yesu siku ile ya pasaka alitwaa Mkate na Divai na kuwapatia wanafunzi wake, na akaagiza tendo lile la kushiriki Mwili wake na damu yake liwe endelevu.

Kwahiyo Ibrahimu alipata ufunuo wa Melkizedeki, kuwa ni Melkizedeki ni Kuhani wa Mungu ambaye atakuja kuleta upatanisho kupitia Mwili wake na Damu yake, ambao unafananishwa na ule Mkate na Divai.

Kwahiyo kitendo hicho cha Ibrahimu kupata ufunuo wa ukuhani wa Melkizedeki, atakaokuja kuufanya siku za mbeleni, ndicho kilichomfanya ashangilie.

Na alishangilia kwasababu aliona Ulimwengu unakwenda kupatanishwa, unakwenda kuokolewa na Kuhani Mkuu, unakwenda kumkaribia Mungu kupitia huyu Melkizedeki..

Ndio maana utaona Ibrahimu hakumwona Melkizedeki kama Mfalme tu!, bali alimwona kama Kuhani Mkuu..

Sasa kabla ya kuendelea mbele hebu tujikumbushe kwa ufupi kuhani ni nani na kazi ya kuhani ni ipi?

Kuhani ni mtu Maalumu aliyeteuliwa na Mungu, kuwaunganisha watu na Mungu wao. Kwasababu katika kumkaribia Mungu kuna kanuni.. katika kumtolea kuna kanuni, vile vile katika kumwomba au kupeleka haja zetu kwake kuna kanuni. Sasa Mtu asipozijua hizi kanuni na akamwendea Mungu hataambulia chochote, au hata anaweza kujitia katika laana badala ya baraka kutokana na kutokujua kanuni.

Hivyo Makuhani ni watu maalumu waliokuwa wanazijua kanuni za kusogelea Mungu na kumsogeza Mtu kwa Mungu.. Ndio maana utaona wana wa Israeli walipotaka kumtolea Mungu, kulikuwa na taratibu za Namna ya kumtolea Mungu ili sadaka hiyo ikubalike, kwamba ilikuwa ni lazima Mwanakondoo achinjwe ipatikane damu, na kupitia ile damu kuhani anaingia nayo ndani ya hema na kufanya upatanisho wa yule mtu na muumba wake..

Sasa Ibrahimu alikuwa anajua umuhimu wa Ukuhani na Makuhani. Ndio maana siku hii alipokutana na Melkizedeki alifurahi.

Sasa kwanini alifurahi?.. Ni kwasababu huyu aliyekutana naye..alikuwa ni KUHANI, na sio kuhani tu!, bali kuhani MKUU!, na sio kuhani mkuu tu!, bali kuhani mkuu wa MILELE wa Mungu aliye juu. (Zaburi 110:4).

Mwanzo 14:18 “Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa KUHANI WA MUNGU ALIYE JUU SANA”

Ibrahimu alipojua kuwa Melkizedeki ni kuhani Milele, maana yake alijua kuwa hata siku yeye atakapokufa!, bado huyu kuhani atakuwepo..kwahiyo alimuona Melkizedeki akija tena miaka mingi baadaye akiwa na Mkate na Divai na kuupa ulimwengu mzima….

Alimuona Melkizedeki akija tena duniani, Pamoja na damu, ili kuwapatanisha watu na Mungu wao..Alimuona akiingia kwenye hema ya kimbinguni akifanya upatanisho, na aliona kupitia damu yake mwenyewe watu wanapatanishwa na Mungu. Hivyo alifurahi na kushangilia..

Waebrania 6:20 “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki”.

Waebrania 5:9 “naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;

10 kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki”.

Hadi leo hii, huyu Kuhani Mkuu, Yesu.. yupo anaishi na ndiye mpatanishi wetu sisi na Baba. Wala hakuna wokovu kwa mwingine yeyote, wala hakuna njia nyingine yeyote ya kufika mbinguni isipokuwa kwa njia yake yeye.

Waebrania 8:1 “Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni,

2 mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu”.

Je umemwamini na kuoshwa dhambi zako naye?..kumbuka dini yako, tabia yako nzuri, sifa zako nzuri, dhehebu lako, na matendo yako havitakufikisha mbinguni kama utakuwa hujamwamini na kufuata kanuni zake za wokovu. Na kanuni yake ni kuamini, kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, kubatizwa ubatizo sahihi na kupokea Roho Mtakatifu. Kama umeikosa hii kanuni basi wewe upo mbali na Mungu, haijalishi unaona mambo yako yanaenda sawa..

Mkaribie leo Yesu kuhani Mkuu upate wokovu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

NI NINI BWANA ANATAZAMIA KILA TUNAPOSHIRIKI MEZA YAKE.

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

KATIKA MLIMA WA BWANA ITAPATIKANA.

Je ni sahihi kumwita mtu “Mkuu”?

TUSIWE WAVIVU WA KUSIKIA.

Je ni lazima kushiriki Meza ya Bwana?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/05/11/ni-lini-na-wapi-ibrahimu-aliioona-siku-ya-bwana-akashangilia/