Je ni halali kupiga kura kanisani kuchagua viongozi?

by Admin | 17 May 2022 08:46 am05

Jibu: Ndio ni jambo la kimaandiko kabisa kupiga kura kuchagua viongozi wa kanisa!.

Lakini ni lazima kuzingatia wanaopiga kura na anayepigiwa kura. Wanaopaswa kupiga kura kuchagua viongozi ni lazima wawe viongozi au watu waliodumu muda mrefu katika Imani (yaani watu ambao hawajaongoka hivi karibuni).. Kwasababu watu waliookoka hivi karibuni bado hawajajua imani vizuri, na sifa za viongozi wa kiimani, vile vile bado hawajazijua hila za shetani, na bado hawajui mambo mengi ya kiimani, hivyo endapo wakipewa nafasi hiyo wanaweza kuchagua watu kutokana na hisia zao tu!, au mitazamo yao tu, na si sawasawa na Neno!.

Vile vile mtu anayepigiwa kura ni lazima awe Mkristo aliyedumu muda mrefu katika Imani na aliyesifika kwa sifa njema, na sio mtu aliyeokoka hivi karibu, ambaye bado hajajua mbinu na hila za shetani.

Katika biblia utaona mtume wa 12, aliyechukua nafasi ya Yuda, aliteuliwa kwa kupigiwa Kura!.

Matendo 1:21 “Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,

22 kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, INAPASA MMOJA WAO AWE SHAHIDI WA KUFUFUKA KWAKE PAMOJA NASI.

23 WAKAWEKA WAWILI, YUSUFU, AITWAYE BARSABA, ALIYEKUWA NA JINA LA PILI YUSTO, NA MATHIYA.

24 Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,

25 ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe.

26 WAKAWAPIGIA KURA; KURA IKAMWANGUKIA MATHIYA; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja”.

Umeona hapo?..Mathiya alichaguliwa kwa Kura!.. na alichaguliwa na Mitume 11, ambao wana uzoefu wa kutosha wa kimaandiko kujua kiongozi bora anapaswa aweje, hawakuhusishwa waamini wote wa Yerusalemu waje kupiga kura!..bali walipiga kura wao viongozi tu! (ili kuzuia upenyo wa shetani)..

Vile vile aliyepigiwa kura, hakuwa mtu aliyekuwa maarufu au mwenye pesa, au mwenye ushawishi.. utaona sifa ya aliyetuliwa ni “mtu aliyefuatana nao mitume tangu wakati wa Yohana hadi wakati wa kuchukuliwa kwa Bwana juu mbinguni”..jumla miaka mitatu na nusu. Kwahiyo walimchagua mtu aliyekuwa mkongwe katika Imani na vile vile aliyekuwa mwaminifu.. Ndio maana utaona Yusufu na Mathiya wote walikuwa wakongwe, lakini Mathiya alikuwa mwaminifu Zaidi ya Yusufu ndio maana alichaguliwa.

Vile vile na sisi tunajifunza namna ya kuchagua viongozi wa kanisa kama Mashemasi, wazee wa kanisa, waangalizi wa Watoto, waweka hazina, waalimu wa vijana n.k kutumia kanuni hiyo.. Kwamba baada ya kusali na kufunga, basi wawekwe wanaostahili kupigiwa kura yule anayestahili, aliye mwamifinu na ateuliwe. Kwa sisi kumteua, basi ni Bwana kamteua..kwasababu sisi tuliomchagua tumetumia vigezo vya Neno kumchagua anayestahili na si macho yetu, Ndio maana na yeye anakuwa ni chaguo la Bwana.

Huo ndio ulikuwa utaratibu wa kanisa la kwanza..Ndio maana utaona Paulo kuna mahali anawaagiza akina Tito na Timotheo vigezo vya kuchagua viongozi..

Tito 1:4 “kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.

5 Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;

6 ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii”.

Je umeokoka?.. je una uhakika KRISTO akirudi leo unakwenda naye mawinguni?, kama huna huo uhakika basi ni uthibitisho kuwa atakapokuja utaachwa!.. Tubu leo kwa kudhamiria kuacha dhambi zako na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, na upokee Roho Mtakatifu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?

Je!Sisi kama wakristo Tunaruhusiwa kuchangia ujenzi wa Imani nyingine?

Nini maana ya kupiga Kite! Katika biblia.

KWANINI UPIGE MISHALE CHINI?

JE! KUNA UMUHIMU WOWOTE WA KULIPA ZAKA?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/05/17/je-ni-halali-kupiga-kura-kanisani-kuchagua-viongozi/