KAMA “MAMA” UMEBEBA HATIMA YA MTOTO WAKO WA KIUME.

by Admin | 23 June 2022 08:46 pm06

Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu tujifunze tena maneno ya Uzima ya Bwana wetu, Yesu Kristo. Neno la Mungu ni taa inayoongoza miguu yetu, na Mwanga wa njia zetu! (Zab. 119:105).

Ipo hali Fulani ambayo, Watoto wa kiume wengi wanakuwa na mapenzi mengi kwa mama zao, na kinyume chake asilimia kubwa ya Watoto wa kike wanakuwa na mapenzi Zaidi kwa baba zao kuliko mama zao.  Ingawa si wakati wote au kwa Watoto wote inakuwa hivi, lakini asilimia kubwa inatokea kuwa hivyo.

Na biblia pia utaona imetaja au kuonyesha kuwepo kwa aina hii ya mahusiano kati ya wazazi na Watoto wa jinsia tofauti.

Hebu tusome visa kadhaa vya baadhi ya  wafalme wa kwenye biblia, kisha kisha tuendelee mbele.

  1. MFALME SEDEKIA.

Yeremia 52:1 “SEDEKIA alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja hapo alipoanza kumiliki; naye akamiliki miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; NA JINA LA MAMA YAKE ALIITWA HAMUTALI, BINTI YEREMIA WA LIBNA.

2 NAYE ALITENDA YALIYO MABAYA MACHONI PA BWANA, sawasawa na yote aliyoyatenda Yehoyakimu.

3 Maana, kwa sababu ya hasira ya Bwana, mambo haya yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata akawaondosha wasiwe mbele za uso wake, naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.

Hapa tunaona Mama wa Sedekia anatajwa kama sababu ya Ubaya wa Mfalme Sedekia… Sasa sio huyo tu!

  1. MFALME REHOBOAMU, Mwana wa Sulemani.

1Wafalme 14:21 “Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA NAAMA, MWAMONI.

22 BASI YUDA WAKAFANYA MAOVU MACHONI PA BWANA; WAKAMTIA WIVU, KWA MAKOSA YAO WALIYOYAKOSA, KULIKO YOTE WALIYOYAFANYA BABA ZAO.

Ijapokuwa Rehoboamu alikuwa ni mwana wa Sulemani, na mjukuu wa Daudi, lakini mama yake anatajwa kumfanya awe mbaya…(sasa sio huyo peke yake..)

  1. MFALME YEROBOAMU

1Wafalme 15:1 “Mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya alianza kutawala juu ya Yuda.

2 Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; NA JINA LA MAMAYE ALIITWA MAAKA, BINTI ABSALOMU.

3 AKAZIENDEA DHAMBI ZOTE ZA BABAYE, ALIZOZIFANYA KABLA YAKE; wala moyo wake haukuwa mkamilifu na Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi babaye”.

Si huyu peke yake…

  1. MFALME AHAZIA.

1Wafalme 8:26 “Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA ATHALIA BINTI OMRI MFALME WA ISRAELI.

27 Akaiendea njia ya nyumba ya Ahabu, AKAFANYA YALIYO MABAYA MACHONI PA BWANA, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa alikuwa mkwe wa jamaa ya Ahabu”.

Sio hawa tu…Unaweza kusoma pia habari za Mfalme Yothamu (2Wafalme 15:33), na Mfalme Manase (2Wafalme 21:1-2) na wengine wengi katika biblia, ambao utaona Uovu wao umesababishwa na mama zao.

Vile vile walikuwepo watu wa kawaida ambao hawakuwa wafalme, ambao pia tabia zao ziliathiriwa na mama zao, mfano wa hao ni yule kijana wa mwanamke wa kiisraeli, ambaye Habari zake tunazisoma katika Walawi 24:10-14, kijana huyu alimtukana Mungu, na akapigwa mawe mpaka kufa,  na wengine wengi.

Lakini pia walikuwepo wafalme ambao walifanya mazuri, na Uzuri wao huo, Pamoja na sifa zao mbele za Bwana zilisababishwa na Mama zao..

  1. MFALME YEHOSHAFATI.

1Wafalme 22:42 “Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA AZUBA BINTI SHILHI.

43 AKAIENDEA NJIA YOTE YA ASA BABAYE; WALA HAKUGEUKA, AKIFANYA YALIYO MEMA MACHONI PA BWANA…..”.

  1. MFALME YEHOASHI.

1Wafalme 14:2 “Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; NA JINA LA MAMAYE ALIITWA YEHOADANI WA YERUSALEMU.

3 AKAFANYA YALIYO MEMA MACHONI PA BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi”.

  1. MFALME UZIA.

1Wafalme 15:2 “Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA YEKOLIA WA YERUSALEMU.

3 AKAFANYA YALIYO MEMA MACHONI PA BWANA, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia”.

Sasa katika maandiko hayo yote, unaweza kujiuliza ni kwanini ni waMama, wanahusishwa na si waBaba?.. Ni kwasababu kuna muunganiko wa kipekee kati ya Mama na mtoto wake wa kiume, ambapo Mama asipoutumia vizuri huo muunganiko, anaweza kujikuta anaharibu hatima ya  mtoto wake wa kiume moja kwa moja. (Ni vizuri kulijua hili mapema, ili mambo yatakapoharibika huko mbeleni, usije ukasema ulikuwa hujui!!)

Mama unapokuwa mtu wa kidunia, unakuwa mtu wa kumkataa Mungu, fahamu kuwa na mtoto wako wa kiume ni rahisi sana, kuamini hiyo njia yako kuwa ni njia sahihi, kuliko hata mtoto wako wa kike.

Lakini mtoto wako wa kiume anapokuona wewe ni mtu unayemcha Mungu, ni mtu unayeutafuta sana uso wa Mungu, na kuukataa ubaya, ni rahisi sana, mwanao  wa kiume, na yeye kuwa kama wewe, hiyo ni (Siku zote weka hilo akilini).

Wafalme wote waliofanya machukizo kwa Bwana, waliharibiwa na Mama zao. Vile vile wafalme wote waliofanya Mema mbele za Bwana, na hata kusifiwa ni kutokana na Mama zao. Hakuna mahali popote wababa wametajwa, katika kutenengeneza hatima za Watoto wao wa kiume.

Hivyo kama Mama, Jifunze kuwapeleka Watoto wako Kanisani, ukiwapeleka wewe Zaidi ya baba hawawezi kuiacha hiyo njia, hata kama watakuja kuyumba kidogo, lakini watairudia tu njia hiyo siku moja!..

Vile vile wafundishe kusoma Neno, na kushika vifungu vya biblia, na kuomba.. Ukifanya hayo kwa Watoto wako wewe kama Mama, ni rahisi mambo hayo kuwaingia Zaidi kuliko kama angefanya Baba.

Halikadhalika msifie mwanao katika mambo ya ki-Mungu na mema, zaidi ya mambo ya ulimwengu huu tu…sauti yako ina thamani kubwa zaidi kwake kuliko baba yake, angefanya hivyo.

Na vile vile wewe Mtoto wa kiume, jifunze kumsikiliza Mama yako, anayekufundisha njia za Mungu, na kukuelekeza njia sahihi.. Kwasababu usipomsikiliza huyo, hakuna mwingine utakayekuja kumsikiliza tena katika Maisha yako.

Ipo methali ya watu wa ulimwengu isemayo “ASIYEFUNZWA NA MAMAYE, HUFUNZWA NA ULIMWENGU”. Ni watu wa kidunia wameitunga methali hii kufuatia uhalisia waliouona, kuwa kwa Mama kunayo mafunzo makuu, Zaidi ya kwa baba.

Hivyo Wewe kama Mama mtengeneze mwanao katika njia ya haki Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”., ..na wewe kama mtoto wa kiume, msikilize Mama yako.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)

MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 2)

Je suruali ni vazi la kiume tu?

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

VIJANA NA MAHUSIANO.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/06/23/kama-mama-umebeba-hatima-ya-mtoto-wako-wa-kiume/