MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 2)

MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 2)

Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa masomo kwa wanawake, katika sehemu ya kwanza tumeona, ni kwanini Bwana alipokutana na yule mwanamke mwenye dhambi, alimtambua kwa jinsia yake (Yaani “mwanamke”) na sio kwa mwonekano wake wa kike pengine wa kiumri au  wa kimaumbile. Hiyo ni kufunua kuwa ujumbe alioubeba yule mwanamke ulikuwa ni wa kijinsia.. yaani maalumu kwa wanawake. Hivyo kama hukupata maelezo yake, unaweza kunitumia ujumbe inbox nikakutumia.

Leo tutaenda katika sehemu ya pili: ya BINTI.

Mahali pengine, Bwana Yesu, aliwatambua wanawake wengine kama, binti zake.. Na cha ajabu ni kuwa, wengine walikuwa pengine wana umri mkubwa kuliko yeye, lakini bado aliwaita BINTI zake, akifunua kuwa kutazama kwake hakukuwa katika jicho la kimwili bali la rohoni. Embu tusome, kisa hiki kimoja..kisha tuone ni ujumbe gani Bwana alitaka kuupitisha kwa ulimwengu kupitia mwanamke huyu.

Mathayo 9:20 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.

21 Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.

22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, BINTI YANGU; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.”.

Swali la kujiuliza ni kwanini alimtambua mwanamke huyu kama binti na sio pengine kama Mama, au bibi?

Ni kwasababu ya Imani yake ya kipekee aliyokuwa nayo kwake..Ambayo hakuiona kwa watu wengine wote waliomfuata, ijapokuwa alihangaika kwa miaka 12 kutafuta suluhu la matatizo yake asipate, lakini alipofika kwa Yesu kwa mara ya kwanza tu hakumuhesabia kama mmojawapo wa wale matapeli aliokutana nao, huko nyuma, waliomchukulia fedha zake.

Bali alimwamini moja kwa moja kwa asilimia 100, akasema, nitakapoligusa tu pindo la vazi lake, muda huo huo nitakuwa mzima, kumbuka hakusema sio “naamini nitapona, au pengine nitapona” hapana, bali alisema “NITAPONA” kuonyesha kuwa alikuwa na uhakika wa yule aliyekutana naye sio mbabaishaji au tapeli…. Na ndio maana akaona hata hakuna sababu ya kwenda kumsumbua kuzungumza naye, au kumwomba aje kumtembelea, Bali aliona pindo la vazi lake, tu linatosha yeye kuwa mzima..

Na Yesu alipoiona Imani yake saa ile ile akamgeukia na kumwita “Binti yangu”.. Akampa nafasi ya kipekee sana Kama Mtoto wa kike aliyemzaa yeye mwenyewe, ambaye ana haki zote za kupokea mema yote ya Baba yake.

Tujiulize ni wanawake wangapi leo Bwana anaweza kuwaita binti zangu? Usidhani Kristo kukuita binti yake, kwasababu ya umri wako mdogo, au mrembo wako, au utanashati wako, hilo halipo, yeye hana jicho la mwilini, kama sisi tulilonalo, haangalii umri wala umbile.

Kama wewe ni mwanamke lakini unafika kwa Kristo ili kujaribu jaribu tu, uone kama Bwana atakujibu au la!,atakusaidia au la! unamlinganisha na wale waganga wa kienyeji uliowahi kuwatembelea huko nyuma.. uone kama atajibu au la!. Ujue kuwa wewe sio binti wa Yesu.

Mabinti wa Yesu, tangu walipokutana na Yesu utawakuta wametulia kwa Bwana hadi sasa, wanaouhakika na waliyemwendea, hawahitaji kusaidiwa na mtu, kuelewa kuwa Yesu ni muweza, wanafanya mambo yao wakiwa wame-relax, huwezi kuwakuta leo kanisani Kesho, disco,  leo wamevaa magauni, Kesho wanakatiza barabarani na visuruali na vikaptura, leo kwa nabii huyu Kesho kwa yule..huwezi kuwakuta wapo namna hiyo.

Hao ndio binti za Mungu. Na faida yao ni kuwa kwasababu wameshaitwa binti za Mungu, tayari wanaourithi kutoka mbinguni. Jambo ambalo wengi hawajui wakidhani kila mtu atakuwa mrithi wa kila baraka ya Mungu mbinguni.

Dada/mama/bibi tambua ni nini Kristo anatamani kuona kwako, acha kutangatanga na huu ulimwengu, Acha kujaribu jaribu, maanisha kumfuata Kristo.. Yeye mwenyewe anasema.

2Wakorintho 6:17 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu WANANGU WA KIUME NA WA KIKE”,

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, Kristo anarudi siku yoyote. Bado tu hujatulia kwa Bwana? Injili tuliyobakiwa nayo sasa hivi sio ya kubembelezewa tena wokovu, ni wewe mwenyewe aumke usingizini, umtafute Mungu wako. Kwasababu muda umeshaisha.

Maran atha..

Usikose sehemu ya tatu na ya mwisho ya Makala hii, ambayo, tutaona pia ni kwanini Bwana Yesu aliwatambua wanawake wengine kama MAMA.

Bwana akubariki..

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments