AKAWAPONYA WALE WENYE HAJA YA KUPONYWA

by Admin | 18 July 2022 08:46 pm07

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, ambalo ni Mwanga wa njia zetu na taa iongozayo miguu yetu! (Zab 119:105).

Si watu wote waliokuwa wanamfuata Bwana au waliokuwa wanamjua Bwana walikuwa wanafunguliwa au kuponywa magonjwa yao!.. Wengi walikuwa hawafunguliwi..Na hiyo ni kwasababu walikuwa hawana HAJA YA KUPONYWA!.. aidha kutokana na kwamba hawamwamini, au walimdharau!.

Luka 9:11 “Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, AKAWAPONYA WALE WENYE HAJA YA KUPONYWA”.

Utaona pia kipindi Bwana Yesu anaenda Galilaya, hakufanya miujiza mingi huko kutokana na kwamba watu hawakumwamini..

Mathayo 13:53 “Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

54 Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?

55 Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?

56 Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?

57 Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe.

58 WALA HAKUFANYA MIUJIZA MINGI HUKO, KWA SABABU YA KUTOKUAMINI KWAO”.

Umeona hapo?..hakufanya miujiza mingi, kwasababu moja tu!..walimdharau na hawakumwamini!

Vile vile utakumbuka kipindi Bwana Yesu ameingia katika lile eneo lenye birika la Bethzatha..ijapokuwa mule ndani kulikuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ambao walihitaji kupona…lakini wengi wao hawakuwa na haja ya kuponywa na Bwana Yesu…wenyewe akili zao na tumaini lao lilikuwa katika yale maji yaliyoaminika kwa wakati huo kama MAJI YA UPAKO!!.

Bwana akawa anapita katikati ya wagonjwa hao…pengine akakutana na baadhi na kuwauliza kama wanataka kuponywa na pengine hata hawakumjibu neno, au walimdharau na  kumfukuza..lakini alipokutana na mmoja na kumwuliza kama anataka kuwa mzima, akakiri kuwa anataka kupona lakini hakuna mtu wa kumtia birikini..Na Bwana Yesu akamwambia asimame ajitwike godoro lake aende..na alipotii na kuamini Neno hilo akawa mzima!.. Lakini wale wengine waliendelea kusubiri Maji yale yachemke..

“1 Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu.

2 Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano.

3 Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke.

4 Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.]

5 Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane.

6 Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, ALIMWAMBIA, WATAKA KUWA MZIMA?

7 Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.

8 YESU AKAMWAMBIA, SIMAMA, JITWIKE GODORO LAKO, UENDE.

9 Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo”.

Je na wewe una haja ya kuponywa roho yako na mwili wako leo?. Basi usijitumainishe katika maji wanayoyaita ya upako, au chumvi wanayoiita ya upako, au mafuta wanayoyaita ya upako.. Mwamini Bwana Yesu leo na maneno yake na pia chukua hatua ya kusimama.

Huenda umeshatumia hayo maji sana, au mafuta kwa muda mrefu lakini hujaona matokeo yoyote…leo hii yageukie maneno ya Bwana YESU katika biblia, yanayosema.. “KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA (ISAYA 53:5)” Wala usiuangalie umati..ukiona mahali pana umati mkubwa wa wagonjwa, ambao hawajapona matatizo yao lakini wanatumainia vitu kama maji, kuwaponya!..fahamu kuwa hapo ni Bethzatha kiroho!.. Uponyaji kutokea ni bahati sana (tena ni kwasababu tu ya huruma za Mungu, na wala si kwasababu vitendea kazi hivyo vina upako)…ndio maana utaona sehemu kama hizo zina msururu wa wagonjwa ambao hawajafunguliwa, lakini wenye matumaini ya kufunguliwa siku moja.. Mahali ambapo Bwana Yesu yupo, hakuna mlundikano wa wagonjwa… kwasababu yeye ni mponyaji na sio daktari!.

Leo hii kwa imani tupa hayo mafuta, tupa hayo maji, halafu liamini hili Neno la Bwana Yesu..halafu subiria uuone muujiza kwa macho yako!. Utashangaa huko kwenye maji ulikuwa unafanya nini siku zote!..

Bwana Yesu akubariki.

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua (Mithali 13:12)?.

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

NUNUA MAJI YA UZIMA.

BIRIKA LA SILOAMU.

NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/07/18/akawaponya-wale-wenye-haja-ya-kuponywa/