MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.

by Admin | 28 July 2022 08:46 am07

Sehemu ya kwanza: LIA NA NYONYA.

Nakusalimu katika jina kuu lenye uweza la mwokozi wetu Yesu Kristo, sifa na heshima vina yeye milele na milele.

Haya ni Makala maalumu kwa waongofu wapya, ikiwa wewe umeokoka hivi karibuni, au una ndugu/mpendwa ambaye amempokea Bwana Yesu siku za karibuni basi Makala hizi ni muhimu sana kwako au kwa yule mwingine.

Tunaposema kuokoka, tunamaanisha Kuzaliwa mara ya pili. Na mtu anazaliwa mara ya pili, kwa kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kabisa kuuacha ulimwengu, na pia kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi (Yohana 3:23), na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38), na kwa kupokea Roho Mtakatifu..Kwa kuzingatia hivyo vigezo, basi mtu huyo anakuwa ameshazaliwa mara ya pili.

Lakini sasa hilo peke yake halitoshi, wengi wanapotimiliza maagizo hayo wanajisahau na kudhani ndio tayari wameshatimilika, hakuna cha ziada.. Hawajui kuwa  mtu unaweza ukawa kweli umezaliwa mara ya pili lakini ni kiumbe kilicho kufa.. Utajiuliza ni kwa namna gani inakuwa hivyo?

Mtu anayezaliwa mara ya pili katika roho anafananishwa na mtoto, anayezaliwa mara ya kwanza katika dunia. Kwa kawaida mtoto huyo, ni lazima aonyeshe tabia kuu mbili. Kabla hajaweza hata kuona, au kuzungumza, au kujitambua..Ni lazima

  1. ALIE.
  2. Baadaye ANYONYE.

ALIE kwa sababu gani.. Mtoto anapotoka tumboni mwa mama yake, anakuwa kama kiumbe mfu, wanachofanya wakunga ni kumpiga kidogo, kumshutua ila atoe sauti, wakisikia analia basi wanatambua kuwa kiumbe kilichozaliwa ni hai, hivyo baada ya muda kidogo wanamsogeza katika hatua nyingine,

Ambayo ni kunyonyeshwa.

Cha kushangaza ni kwamba mtoto yule anaposogezwa katika nyonyo ya mama yake, hakuna mtu yeyote anayemfundisha kunyonya, utaona ni yeye mwenyewe anajua wajibu wake, wa kula, ndio hapo utaona saa hiyo hiyo ataanza kufyonza maziwa kana kwamba alishawahi kufundishwa huko tumboni jukumu lake kabla hajafika duniani.

Sasa kiroho pia ndio ipo hivyo. Ikiwa wewe umezaliwa kweli mara ya pili, hizi ni hatua za awali kabisa ambazo utazionyesha. Na kupitia hizo sisi wengine tutathibitisha kweli wewe ni kiumbe kipya hai. Kwani  ni lazima utoe kelele fulani rohoni.. Huwezi kutulia, ambao sisi tuliokomaa kiroho tutazitambua, japo wewe hutoweza kuzielewa katika hatua yako ya uchanga rohoni..

Sisi tutaona kuhangaika kwako kutaka kumsaada wa kumjua Mungu, Na sisi tukishalitambua hilo, basi tunakuwa na wajibu mkubwa sana wa kukusaidia, kukosegezea matiti (Neno la Mungu) unyonye..

Embu tujifunze kisa cha Musa, pindi anazaliwa..Biblia inatuambia, alipozaliwa, mama yake alimficha ili Farao asimuue, lakini alipoona hali imekuwa  mbaya, alimtengenezea kisafina kidogo, kisha, akamtupa mtoni.. Lakini mtoto yule alipokuwa katika kila kisafina, hakukaa kimya tu, bali alikuwa anapiga kilele, analia,sana na binti Farao aliposikia alikwenda kutazama na kufungua aone ni nini kipo ndani, akakaona katoto, wakakahurumia..Embu tusome kwa ufupi kisa hicho;

Kutoa 2:6 “Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, MTOTO YULE ANALIA. BASI AKAMHURUMIA, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.

7 Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu?

8 Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto.

9 Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha.

10 Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini”.

Umeona? Mtoto yule angeangamia kama asingelia, lakini alipolia, akahurumiwa akatafutiwa msaada mapema wa kunyonyeshwa, na hatimaye akakua akaja kuwa Mkombozi wa Israeli, ndiye Musa tunayemsoma.

Ndugu/Dada uliyeokoka hivi karibuni, kutojishughulisha kwako na mambo ya Mungu, kunathibitisha kuwa wewe ni kiumbe mfu, kutoulizia kwako Habari ya ibada, kunatuambia kuwa wewe si kiumbe hai..Hupaswi kujificha, hupaswi kujiepusha na kiongozi wako wa kiimani..hupaswi kukaa mbali na wapendwa, hupaswi kupitisha siku nyingi hujulikani upo wapi, au maendeleo yako ya kiroho hayatambuliki.. kataa hiyo hali kwa nguvu zote..

Wewe tayari ni kiumbe kipya, yatamani sana maziwa ya roho.. Usisubiri kukumbushwa kumbushwa kuhudhuria mafundisho ya kuukulia wokovu, kama mtoto mchanga ambaye hafundishwi na mtu kunyonya ni wajibu wako kutafuta kufundishwa Neno la Mungu, kwa bidi zote..Sio wewe utafutwe.

1Petro 2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”

Hivyo anza sasa kubadili mwenendo wa Maisha yako.. Jifunze kuomba na wapendwa, jifunze, kusoma biblia mwenyewe kuanzia sasa, jifunze kuuliza maswali, jifunze kumshirikisha kiongozi wako wa kiroho maendeleo yako. Atakusaidia, na kukuonyesha njia sahihi.

Wagalatia 6:6 “Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote”.

Hivyo zingatia mambo hayo makuu mawili. Na Bwana akutie nguvu.

Shalom.

Sehemu ya pili itafuata…

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

Maziwa yasiyoghoshiwa ni nini? Kwanini biblia inatumia mfano huo?

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

UMEITIMIZA HAKI YOTE?

ILI TUONEKANE SAFI MBELE ZA MUNGU TUFANYE NINI?

Tofauti kati ya mbinguni, peponi, Kuzimu, Jehanamu, na Paradiso ni ipi?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/07/28/mafundisho-maalumu-kwa-waongofu-wapya/