ILI TUONEKANE SAFI MBELE ZA MUNGU TUFANYE NINI?

ILI TUONEKANE SAFI MBELE ZA MUNGU TUFANYE NINI?

Atukuzwe Yesu Kristo Bwana wetu milele na milele. Sifa na utukufu ni vyake yeye sikuzote..

Biblia inatuambia, mambo yote yaliyoandikwa katika agano la kale, yalikuwa ni kivuli cha agano jipya la rohoni. Hivyo maagizo mengi ya mwilini, unayoyasoma kule, yalikuwa ni muhtasari wa agano jipya lili bora Zaidi.

Ni sawa na mwanafunzi anayeanza chekechea, ukitaka kumfundisha  Hesabu za KUJUMLISHA na KUTOA, huwezi moja kwa moja ukamwandikia  5-3=2. Ukadhani ataelewa, ni kweli kwa upande wako ni rahisi kwasababu tayari upeo wako ulishatanuka, lakini kwa mtoto, huna budi kutumia njia ya vitendo kwa mwanzoni..

Ndipo itabidi umwekee vijiti, au mawe, ahesabu kimoja mpaka cha tano, kisha aondoe hapo vitatu, ndipo vile viwili vinavyosalia, viwe jibu. Hivyo akilini mwake anajua hesabu ni vijiti na mawe, lakini kihalisia sio hivyo.. Atakapokomaa akili, ndipo atakuwa hana haja ya vijiti, au vidole, au mawe tena.

Vivyo hivyo katika biblia, agano la kale la mwilini lilikuwa ni hatua za awali za kulielewa agano lilibora la rohoni..(Waebrania 10:1, Wakolosai 2:16-17).

Sasa tukirudi katika kichwa cha somo letu. Tufanye nini ili tuonekane safi mbele za Mungu?.

Kumbuka, katika torati Mungu aliwaatenga Wanyama wote katika makundi mawili makuu.

  1. Kundi la kwanza ni Wanyama safi
  2. Kundi la pili ni Wanyama najisi

Sasa ili mnyama aitwe safi, ilikuwa ni sharti, akidhi vigezo maalumu Mungu alivyovioanisha.. Na vigezo vyenyewe zipo vitatu ambavyo ni hivi;

  1. Awe anacheua
  2. Awe na kwato
  3. Awe na kwato zilizogawanyika mara mbili

Ikiwa na maana kama hatokidhi vigezo vyote vitatu, basi huyo mnyama ni najisi, haijalishi atakuwa na kimoja au viwili kati ya hivyo. Hakuruhusiwa, kuliwa, na wengine kufugwa au  kuguswa mizoga yao.

Walawi 11:2 “Neneni na wana wa Israeli, mkiwaambia, Wanyama hawa ndio wanyama wenye uhai mtakaowala, katika hayawani wote walio juu ya nchi.

3 Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala.

4 Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

5 Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

6 Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

7 Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu.

8 Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.

Sasa utajiuliza ni kwanini, Mungu aliwaona hawafai?

Sio kwamba aliwaona wana sumu kali, au wana madhara wakiliwa, kama wengi wanavyodhani hapana, kwasababu wengi wao wanaliwa hadi sasa, na hakuna madhara yoyote yanayowapata bali alikuwa anatufundisha jambo la rohoni, ili tutakapoingia katika agano jipya tuelewe vema, Mungu anapozungumzia unajisi anamaanisha nini.

Kwamfano, anaposema,

  1. Wasiocheua, ni najisi.

Kucheua ni nini? Ni ile hali ya mnyama kuwa na uwezo wa kukirejesha tena kile chakula alichokimeza na kukitafuta tena, kwa kawaida Wanyama kama ng’ombe, twiga, ngamia, hawa wanakuwa na tumbo la ziada, ambalo linawasaidia kurejesha na kutafuna tena kile walichokila.

Hii inafunua nini sasa katika agano jipya?. Ukiwa si mtu wa kutafakari na kukitendea kazi kile unacholishwa (Neno la Mungu), wewe ni kusikia tu kilasiku, lakini hakuna tendo lolote la ziada unalolionyesha kwa kile ulichofundishwa, huzalishi chochote, mbele za Mungu ni kama mnyama najisi, asiyeweza kucheua, Na kamwe hutoweza kuingia mbinguni (patakatifu pa Mungu), siku ukifa. Mungu anataka tutendee kazi Neno lake, pia tujifunze kuzikumbuka Fadhili zake alizotutendea huko nyuma, tusiwe hasahaulifu. Usahaulifu ni tabia ya unajisi.

Hivyo jiangalie ndani yako je! Wewe ni mtu wa kulitendea kazi Neno la Mungu? Tangu uliopoanza kusikia ni mangapi umeyatendea kazi, Kama sio, basi bado hujawa safi.

2) Awe na Kwato:

Kucheua tu haitoshi, walikuwepo Wanyama wenye uwezo huo kama ngamia, lakini walikosa kwato.. yaani ni kama nyama tu imeshuka mpaka chini, ni sawa na kusema hawana kiatu.

Awe na Kwato:

Hivyo, ni dhaifu kwa upande mmoja, kwasababu wamekosa ulinzi miguuni, ukipita msumari mrefu, basi safari yao imekwisha, hawawezi kutembea kila mahali, penye miiba, hawawezi kuruka, kwasababu miguuni ni wadhaifu.

Tofauti na mnyama  farasi,au swala, yeye ana kwato ndio maana ni mwepesi kutembea popote, ngombe anakwato, ndio maana anaweza kulima hata kwenye mashamba n.k.

Hii inatupa tafsiri gani rohoni?

Waefeso 6:14 “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani”;

Hapo anasema, ukiwa askari wa Kristo ni lazima ujifunze kusimama ukiwa umejifungia utayari miguuni.. utayari wa nini? Utayari wa kumtumikia Mungu kwa hali zote. Na je utayari huo unatokea wapi? Unatokea kwenye kuisikia injili ya Yesu Kristo, kwa kupitia hiyo tunapokea hamasa, na nguvu na uweza wa kumtumikia yeye.

Wanajeshi, kwa kawaida ni lazima wavae viatu vigumu miguuni waendapo vitani, ili kuwasaidia kukatisha katika mazingira yoyote magumu, vinginevyo wakienda peku peku, hawataweza kwenda mbali

Halikadhalika na wewe, ukiwa umejivika UTAYARI huo wa kumtumikia Bwana katika mazingira yoyote, rohoni unaonekana kama ni mnyama mwenye kwato. Unafaa kwa kazi,

3) Mwisho, kwato ziwe zimegawanyika.

Wapo Wanyama ambao walikuwa wanacheua, walikuwa wana kwato, lakini kwato zao zilikuwa hazijagawanyika mara mbili. Hapo bado walikuwa ni najisi.

kwato zilizogawanyika

Ni kwanini, Bwana alitaka kwato za mnyama zigawanyike mara mbili, ili waonekane safi?  Ni siri gani ipo nyuma yake?

Kama tulivyotangulia, kuona kwato, Ni utayari tuupatao katika injili…

Lakini lazima tujifunze kuligawanya Neno la Mungu. Ndio maana biblia inayo agano la kale na jipya. Ili tuweze kuwa askari kamili ya Kristo, hatuna budi kufahamu kuweka injili ya Kristo kama atakavyo yeye, kwa uongozo wa Roho Mtakatifu.

Kwa kukosa, kuelewa ufunuo uliokatika agano lake, ndio inayopelekea, watu kufundisha kuwa vyakula ni najisi kwasasa..

1 Timotheo 4 : 1-5

1 Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

3 wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.

4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani;

5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

Wengine wanaona Ibrahimu, Daudi, wameoa wake wengi, anadhani ndio hata sasa ndivyo ilivyo, na Mungu anapendezwa navyo. Hawajui ni ufunuo gani ulikuwa nyuma yake.

Hivyo biblia inatutaka sana tujifunze kuligawanya vema Neno la Mungu. (2Timotheo 2:15).

Ni muhimu sana. Na hiyo inamuhitaji Roho Mtakatifu.

Hivyo kwa kukidhi vigezo hivi vitatu; 1) Kutendea kazi Neno la Mungu 2) Kumtumika kwa Bwana 3) Kuwa na maarifa ya Neno la Mungu. Basi utakuwa mnyama safi mbele za Mungu.

Na hivyo tutamkaribia Mungu.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Lumbwi ni nini katika biblia?

Wibari ni nani?(Mithali 30:26)

Bwana alimaanisha nini aliposema enendeni mkaihubiri injili kwa kila kiumbe?

Maji ya Farakano ni nini katika biblia?

NI SALAMA ROHONI MWANGU Lyrics

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Ubarikiwe sana mwalim

Anonymous
Anonymous
1 year ago

God bless you!!