KAA MAJANGWANI.

by Admin | 2 August 2022 08:46 pm08

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.

Sehemu ya pili: Kaa Majangwani:

Luka 1:80 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli”.

Ni kawaida ya Mungu, kuwaandalia Watoto wake, mahali maalumu pa kukulia kiroho.. Ikiwa unatamani nguvu zako za rohoni ziongozeke kwa kasi wewe kama mwongofu mpya uliyezaliwa mara ya pili, huna budi kukaa majangwani.

Mungu alipowatoa wana wa Israeli Misri, hakuwavukisha moja kwa moja na kuwafikisha Kaanani ndani ya siku moja, bali aliwapitisha kwanza jangwani, kuwalisha huko na kuwakuza kiroho, kwa muda wa miaka 40, kwasababu walikuwa bado ni Watoto wachanga, na ndipo baadaye wakaingia Kaanani, wakiwa Hodari na nguvu nyingi rohoni.

Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”.

Biblia pia inatuambia Yohana mbatizaji alipozaliwa, alikimbilia majangwani huko kuishi, na matokeo yake akakua na kuongozeka nguvu nyingi sana rohoni kwa kasi, na ndio maana hatushangai kwanini Bwana Yesu anamshuhudia na kusema katika wazao wa wanawake hakuwahi kutokea mtu aliyekuwa mkuu kama Yohana Mbatizaji.(Mathayo 11:11).. Hiyo yote ni kwasababu gani? Ni kwasababu alitumia Muda mwingi majagwani.

Sasa Kiroho jangwani ni wapi?

Haimaanishi kuwa ni sisi tukimbilie majangwani tukaishi huko, ili tukue kiroho hapana… Kama tunavyojua jangwani ni mahali ambapo hapana uwepo wa wanadamu, ni mahali pa ukiwa, pasipokuwa na huduma zozote za kijamii.. Ndivyo inavyompasa mkristo aende rohoni.

Unapaswa katika hatua zako za awali za wokovu: Kwa bidii zote uwe tayari, kuukana huu ulimwengu. Kukaa mbali na mambo yote yanayousonga wokovu wako, bila kujali unapoteza nini, au unakosa nini..

Ukiokoka, kubali kuachana na wale marafiki zako wa kale uliokuwa unakwenda nao disco, uliokuwa unakunywa nao pombe, uliokuwa unatukana nao, kubali kuwa mpweke, kwa kipindi Fulani, kwani hivyo ndivyo unavyoiponya roho yako.

Ukiokoka, kubali wakati mwingine, kupoteza hiyo kazi isiyo halali kwa Mungu, kama unafanya biashara ya pombe acha, ..wala usidhani kuwa utaangamia, kwamba Mungu atakuacha ufe, hilo wazo ondoa, uwezo wa kukulisha Mungu anao, Kama alivyofanya kwa wana wa Israeli kule jangwani, atafanya na kwako pia..

Biblia inasema..

Ufunuo 12:13 “Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.

14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, AENDE ZAKE NYIKANI HATA MAHALI PAKE, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo”.

Umeona, Mungu ameshaandaa mahali pako huko nyikani, pa kukulisha kwa wakati wako na majira yako. Hivyo usiogope wewe uliyemzaa Kristo maishani mwako.

Kama wewe ni binti kubali kukaa mbali na Fashion, kubali kujisitiri na kuchoma hivyo vimini na masuruali, kubali kuonekana umerukwa na akili kwa ajili ya Kristo, hata ulimwengu mzima ukikuona mjinga, kubali hiyo hali, weka kando kila mzigo wa dhambi, kwasababu ndivyo unavyoiponya roho yako.

Je! Faida yake ni ipi?

Faida yake ni kwamba Yesu anapata nafasi ya kukupitisha katika madarasa yake, na kwasababu husongwi na mambo mengine, hivyo kasi yako ya kukua kiroho itakuwa ni kubwa sana..

Maandiko yanasisitiza hilo katika;

Isaya 40:3 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu”.

Kuonyesha kwamba mahali pekee ambapo utamtengenezea Mungu njia, katika maisha yako ni jangwani.

Leo hii utaona watu wengi wamedumu katika wokovu kwa miaka mingi, lakini huoni mabadiliko makubwa yoyote ndani yao, bado ni wachanga kila siku wanataka wanyweshwe tu maziwa, ni kwasababu gani?

Ni kwasababu hawakumpa Kristo, nafasi ya kuwafundisha majangwani..Walilikimbia jangwa, wakakaa ulimwenguni, na hivyo Bwana akawaacha.

Ndugu/Dada uliyeokoka hivi karibuni usiipuzie hiyo sauti inayokuambia, acha hiki, acha kile, mwache Rafiki yule, acha jambo lile..usiipuuzie kabisa, fanya hivyo, ni sharti upoteze, ili upate baadaye, majira haya ni kujikana nafsi yako, kuichukia nafsi yako, na kujitwika msalaba wako kumfuata Yesu, hilo haliwezi kuepukika ikiwa unataka ukue kiroho kwa kasi anayoihitaji Kristo ndani yako.

Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

27 Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”.

Kabla ya kumzalia Mungu matunda ni lazima upitishwe jangwani, kutakaswa na Mungu, hivyo kuwa mwepesi kuacha udunia wako. Umfuate Yesu.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA: Sehemu ya 1

EE MUNGU, MUNGU WANGU, NITAKUTAFUTA MAPEMA:

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

UNYAKUO.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 13 (Kitabu cha Hosea).

NAYE ALIKUWA HANA BUDI KUPITA KATIKATI YA SAMARIA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/02/kaa-majangwani/