VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 13 (Kitabu cha Hosea).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 13 (Kitabu cha Hosea).

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, libarikiwe!…karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu wetu. Neno la Mungu ni Taa iongozayo hatua za miguu yetu na Mwanga unaoongoza Njia yetu.

Huu ni mwendelezo wa ufupisho wa vitabu vya Biblia, Tumeshavitazama vitabu kadhaa nyuma, kama bado hujapitia uchambuzi huo, basi Unaweza kufanya hivyo kwa kufungua link hii>>VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1. Au ukawasiliana nasi kupitia namba zilizopo mwisho wa somo hili, au katika tovuti yetu, ili tuweze kukutumia masomo hayo kwa njia ya Whatsapp.

Vile vile ni muhimu kujua kuwa huu ni Ufupisho tu!, na muhtasari, ambao utakuwezesha kuvielewa vitabu hivi kiurahisi, hivyo baada ya kusoma ufupisho huu ni vizuri kwenda kusoma kitabu husika, ili ukajazilishe vile vichache ulivyovitapata huku. Kwa kusoma ufupisho huu pekee yake bila kushika biblia, hakuna chochote utakachonufaika nacho, Zaidi sana ni afadhali kuisoma biblia bila ufupisho wowote, kuliko kusoma hapa na kutoishika kabisa biblia.

KITABU CHA HOSEA.

Kitabu cha Hosea, kimeandikwa na Hosea Mwenyewe na maana ya jina Hosea ni “Wokovu”.. Hosea alikuwa ni Nabii wa Mungu, kama vile alivyokuwa Yeremia, Isaya au Danieli.. Kitabu cha Hosea, kinakadiriwa kuandiwa kwa muda wa miaka 40. Ndani ya muda huo Hosea alipokea mfululizo wa maono kutoka kwa Mungu na akayaandika katika kitabu hicho chenye sura/milango 14.

Nabii Hosea ni moja ya manabii watatu ambao Bwana aliyatumia Maisha yao kama Ishara… Wengine ni Nabii Isaya, ambaye kuna wakati aliambiwa atembee uchi (kuelewa zaidi kwanini aambiwe atembee uchi fungua hapa >> KWANINI NABII ISAYA ALIAGIZWA KUHUBIRI UCHI? ), na mwingine ni Ezekieli ambaye aliambiwa ale mikate iliyookwa juu ya kinyesi cha Mwanadamu, na vile vile alale kwa upande mmoja kwa siku nyingi, kuwa ishara juu ya wana wa Israeli.

Lakini Nabii Hosea yeye Mungu aliyafanya Maisha yake kuwa ishara, kwa namna nyingine, na namna hiyo ni “katika eneo la Ndoa”.. Kwa kawaida Bwana hakuwahi kuwapa watu maagizo ya kuoa watu wazinzi au makahaba. Lakini Hosea aliambiwa akaoe mwanamke “Kahaba”..Mwanamke ambaye tabia yake si kutulia na mwanaume mmoja, Ambaye hawezi kukaa na mwanaume mmoja. Huyo ndio Bwana alimpa maagizo Hosea akamwoe kwa sababu maalumu..

Lengo la kumpa maagizo hayo ni ili kuwafundisha Israeli ni kwajinsi gani wanaonekana mbele zake, kwamba mbele za Mungu wanaonekena kama Mwanamke kahaba, ambaye hatulii ni mume wake mmoja. Na Taifa la Israeli katika roho linafananishwa na mwanamke, na Mungu ni kama MUME wake.

Yeremia 31:31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.

32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, INGAWA NALIKUWA MUME KWAO, asema Bwana”.

Umeona hapo?.. anasema tangu siku ile aliyowatoa Misri, yeye alikuwa ni MUME KWAO, lakini walilivunja agano lake..pia Yeremia 3:14, inazungumzia jambo hilo hilo…

Yeremia 3:14 “Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana; maana mimi ni MUME WENU; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni”

Kwahiyo Kwajinsi Israeli walivyokuwa wanamwacha Mungu, kiroho ni kama walikuwa wanamsaliti MUME WAO, ambaye ni Mungu. Na matendo yote mabaya waliyokuwa wanayafanya kiroho yalitafsirika kama UASHERATI.

Kwahiyo Hosea kuambiwa vile aoe kahaba, ni kuwapa ujumbe Israeli kuwa kama vile yeye (Hosea) anavyosumbuliwa na mwanamke Kahaba, (leo yupo na yeye ndani, kesho katoroka kwenda kufanya ukahaba)…ndivyo na Israeli inavyomsumbua Mungu kwa uzinzi wa kiroho inaoufanya..

Sasa ili kuzidi kuelewa kwa undani, juu ya Agizo hili Hosea alilopewa unaweza kufungua hapa >>> Kwanini MUNGU Anampa Nabii Hosea maagizo ya Kumuoa mwanamke kahaba?

Kwahiyo baada ya Israeli yote kuona Hosea kaoa mwanamke mzinzi na tabu anazozipata kwa mwanamke huyo, na jinsi Hosea alivyowapa majibu, baadhi ya wana wa Israeli walitubu, na kumgeukia Mungu, lakini wengine walishupaza shingo.

Kitabu cha Hosea tutakigawanya katika sehemu kuu 8.

SEHEMU YA KWANZA (mlango wa kwanza na wa pili).

 Unahusu maelekezo ya Bwana kwa Hosea, juu ya kutafuta MKE WA KIKAHABA ALIYEITWA GOMERI, na kuzaa naye Watoto watatu, mtoto wa Kwanza, ambaye atakuwa wa kiume atamwita YEZREELI (Yezreeli ulikuwa ni mji ya mfalme wa Israeli, aliyeitwa Ahabu na mkewe Yezebeli).  Ndipo palipokuwa kitovu cha maasi yote ya Isreali.

Na mtoto wa pili ambaye atakuwa wa kike ataitwa Lo-ruhama, ambayo tafsiri yake ni “Asiyehurumiwa”. Na mtoto wa tatu, ambaye ni wa kiume atamwita Lo-Ami, maana yake ni “Si watu wangu”.

Kupitia Watoto hao watatu, Pamoja na Mama yao, Mungu alipitisha ujumbe mzito sana kwa Israeli yote na Yuda. (Unaweza kupitia sura hizo mbili binafsi, kwa msaada wa Roho).

SEHEMU YA PILI (mlango wa tatu).

Unahusu maelekezo ya Bwana, kwa Hosea kuhusu kuoa mwanamke mwingine wa kizinzi, lakini huyu wa sasa, anapaswa akamchukue ambaye tayari anapendwa na mtu mwingine, lengo la kufanya hivyo ni kuwaonyesha ni jinsi gani, wana wa Israeli watatwaliwa na Mfalme Nebukadreza na kukaa siku nyingi mbali na uwepo wa Mungu aliye mume wao.

Hosea 3:1 “Bwana akaniambia, Enenda tena, mpende mwanamke apendwaye na rafiki yake, naye ni mzinzi; kama vile Bwana awapendavyo wana wa Israeli, ingawa wanaigeukia miungu mingine, na kupenda mikate ya zabibu kavu.

2 Basi nikajinunulia mwanamke huyo kwa vipande kumi na vitano vya fedha, na homeri moja ya shayiri, na nusu ya homeri ya shayiri;

3 nami nilimwambia, Utatawa kwa ajili yangu siku nyingi; hutafanya mambo ya ukahaba, wala hutakuwa mke wa mtu awaye yote; nami nitakuwa hali iyo hiyo kwa ajili yako.

4 Kwa maana wana wa Israeli watakaa siku nyingi bila mfalme, wala mtu mkuu, wala sadaka, wala nguzo, wala naivera, wala kinyago;

5 baada ya hayo wana wa Israeli watarejea, na kumtafuta Bwana, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao; nao watamwendea Bwana na wema wake kwa kicho siku za mwisho”.

SEHEMU YA 3 (mlango wa 4-5).

Bwana anatoa OLE juu ya Israeli kutokana na dhambi zao wanazozifanya.

SEHEMU YA 4 (Mlango wa wa 6).

Bwana anatoa Shauri la Toba kwa Israeli, kwamba watubu naye atawarehemu..

Hosea 1 ‘Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.

2 Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.

3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi”.

SEHEMU YA 5 (Mlango wa 7-9).

Bwana anazidi kumwonyesha Nabii Hosea, makosa ya Israeli na jinsi wanavyoyategemea Mataifa kama Misri na Ashuru katika kupata msaada, zaidi ya kumtegemea Bwana.

Hosea 7:10 ‘Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia Bwana, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.

11 Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.

12 Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.

13 Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.

14 Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi”.

SEHEMU YA 6 (Mlango wa 10).

Unabii wa Israeli kuchukuliwa mateka kwenda Ashuru.

Kumbuka Israeli ilikuja kugawanyika katika sehemu kuu 2, kaskazini na kusini, kaskazini palibaki kuitwa Israeli lakini upande wa kusini kuliitwa Yuda. Sasa huu upande wa Kaskazini ulikuja kuchukuliwa mateka mpaka Taifa la Ashuru lililopo Kaskazini..kutokana na maasi kuwa mengi, lakini kabla ya kupelekwa huko Bwana alituma manabii wengi kuwaonya watubu, waache maasi, wairudie sheria ya Mungu, na mmojawapo wa manabii hao, Bwana aliowatuma kuwaonya Israeli ni huyu Nabii Hosea!.. aliwaambia maneno haya…

Hosea 10:5 “Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-Aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka.

6 NAYO ITACHUKULIWA ASHURU, IWE ZAWADI KWA MFALME YAREBU; EFRAIMU ATAPATA AIBU, NA ISRAELI ATALIONEA HAYA SHAURI LAKE MWENYEWE.

7 Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji.

8 Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni.

9 Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; ili vita vilivyokuwa juu ya wana wa uovu visiwapate katika Gibea”.

SEHEMU YA 7 (Mlango wa 11-12).

Bwana anawakumbusha Israeli Huruma zake (Jinsi alivyowahurumia kipindi wakiwa katika nchi ya utumwa ya Misri), lakini sasa wamemwacha, na hawajui kama wapo kwenye hatari.

Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”.

SEHEMU YA 8 (Mlango wa 12-14).

Bwana anazidi kuwapa shauri Israeli la kumrudia yeye kutubu, vile vile anawatahadharisha juu ya Hukumu ijayo.

Hosea 14:1 “ee israeli, MRUDIE BWANA, MUNGU WAKO; MAANA UMEANGUKA KWA SABABU YA UOVU WAKO.

2 chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie bwana; mkamwambie, ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe”.

Kwa hitimisho ni kwamba kitabu cha Hosea ni kitabu cha Maonyo ya Israeli kumrudia Mungu, na kwamba, watubu..

Na sisi (watu wa Mungu) tunafananishwa na Mwanamke, tena Bibi-arusi..na Yesu Kristo ni Bwana wetu..

2Wakorintho 11:2 “Maana nawaonea wivu, WIVU WA MUNGU; KWA KUWA NALIWAPOSEA MUME MMOJA, ILI NIMLETEE KRISTO BIKIRA SAFI.

3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo”.

Kama Bibiarusi wa Kristo, unapofanya anasa kwa makusudi, katika roho unatafsirika kuwa unafanya uasherati mbele za Bwana, kama ni mtukanaji, mwizi, mlevi, na huku unajiita umeokoka jua kuwa unamtia Bwana wivu, kwa uasherati huo wa kiroho unaoufanya.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)

KIELELEZO CHA MWANAMKE KATIKA NYUMBA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Naomba maelezo au tafakari ya hosea tokea mwanzo hadi mwisho