USINIONDOLEE ROHO WAKO MTAKATIFU.

by Admin | 5 August 2022 08:46 am08

Swali: Je! Roho Mtakatifu anaweza kuondoka juu ya Mtu?.Kulingana na Zaburi 51:11?

Tusome,

Zaburi 51:11 “Usinitenge na uso wako, Wala Roho yako mtakatifu usiniondolee“.

Jibu rahisi la swali hili ni ndio!, anaweza kuondoka juu ya mtu, na mtu akabaki kama alivyo…

Mfano wa mtu katika biblia ambaye aliondokewa na Roho Mtakatifu juu yake ni Mfalme Sauli.

1Samweli 16: 14 “Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua.

15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua”

Na sababu pekee iliyosababisha Roho wa Mungu kuondoka juu ya Sauli ni tabia ya Sauli ya kutokujali na vile vile kutoyatii maagizo ya Mungu, na kumdharau.

1Samweli 15:22 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu”.

23 Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme”.

Na madhara ya mtu aliyempoteza Roho Mtakatifu, ni KUONDOKEWA NA FADHILI ZA MUNGU JUU YA MAISHA YAKE.

Sauli aliondokewa na Fadhili za Mungu, baada tu ya Roho wa Mungu kuondoka juu yake..

2Samweli 7:14 “Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;

15 LAKINI FADHILI ZANGU HAZITAMWONDOKA, KAMA VILE NILIVYOMWONDOLEA SAULI, niliyemwondoa mbele yako”.

Mtu aliyeondokewa na Fadhili za Mungu, anakuwa anaipoteza ile Amani ya KiMungu kipindi amempokea Roho, hali kadhalika ile furaha ambayo ilikuwa ndani yake inapotea!..ile raha aliyokuwa anaipata alipokuwa ndani ya wokovu, inapotea!…Ule utulivu aliokuwa anaupata kipindi Roho yupo juu yake, unapotea….kile kibali alichokuwa nacho kipindi cha mwanzo kinaondoka..anakuwa ni mtu wa kuhangaika, na kusumbuliwa na roho chafu za wivu, hasira, uchungu, na nyinginezo, kama ilivyokuwa kwa Sauli.

Maandiko yanasema Roho wa Mungu alipomwacha tu Sauli, pale pale roho mbaya ikaanza kumsumbua…akaanza kumwonea wivu Daudi, akaanza kuwa mkatili kwa kuwaua makuhani wa Mungu..

1Samweli 22:11 “Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia”.

Hizo ndizo hasara za kumpoteza Roho Mtakatifu.. Mfalme Sauli alipoasi, Fadhli za Mungu zilimwondoka, na akawa mtu wa kukosa amani, furaha, kujiamini, na wivu…

Lakini kumbuka pia, kuondokewa na Roho Mtakatifu si kuacha kunena kwa lugha, au kufanya miujiza, au kutoa pepo. Mtu aliyeondokewa na Roho Mtakatifu bado anaweza kutoa pepo, bado anaweza hata kunena au kwa lugha..

Kwasababu matunda ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu sio Kunena kwa lugha, au kutabiri, au kuona maono, bali ni yale yanayotajwa katika kitabu cha Wagalatia 5:22 “ Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,”.. Mambo hayo ndio yanayopotea ndani ya mtu, pindi Roho Mtakatifu anapoondoka ndani yake.. Na si kunena kwa lugha, au kuona maono, au kutabiri.. Mtu anaweza kunena na kutabiri lakini Roho Mtakatifu akawa hayupo ndani yake..

Utauliza hilo tunalithibitisha vipi?.. Maandiko yanaonyesha Sauli hata baada ya Roho wa Mungu kuondoka ndani yake, bado aliendelea kutabiri..

1Samweli 18:10 “Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, NAYE AKATABIRI NDANI YA NYUMBA. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake”.

Umeona?.. Matunda ya Roho ni tofauti kabisa na kazi za Roho.. Kazi za Roho kama miujiza, unabii, ishara, zinaweza kufanyika kupitia yeyote yule. Bwana alimtumia Punda kuona maono ya malaika mbele ya Balaamu, atashindwaje kumpa maono mwenye dhambi?..

Kwahiyo maono au kunena kwa lugha, sio uthibitisho wa kwanza wa mtu aliye na Roho Mtakatifu, uthibitisho wa kwanza wa mtu mwenye Roho Mtakatifu ndani yake ni hayo matunda tunayoyasoma katika Wagalatia 5:22, ambayo ni Upendo, amani, furaha, Fadhili, kiasi..yaani kwaufupi ni utakatifu (Waebrania 12:24). Ndio maana Bwana Yesu alisema wengi watakuja siku ile na kusema Bwana Bwana hatukutoa pepo kwa jina lako, na kufanya unabii, lakini Bwana atawafukuza kutoka mbele zake.

Mathayo 7:22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Hata sasa Roho Mtakatifu anaweza kuondoka juu ya Maisha yetu!.. na tukazipoteza Fadhili za Mungu. Na ataondoka endapo TUTAMHUZUNISHA, au KUMZIMISHA.

TUNAMHUZUNISHAJE?

Maandiko yanasema katika Waefeso 4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi”.

Tabia za kutokujali Neno la Mungu, kama alivyokuwa Sauli ndizo za kwanza zitakazoweza kusababisha Roho Mtakatifu kuondoka juu yetu..Tunapolisikia Neno halafu hatulitii.. badala yake tunaendelea na mambo yale yale mabaya, hapo tunamhuzunisha Roho mtakatifu aliye ndani yetu…

Tunapoendelea kufanya mambo machafu, ambayo tunajua kabisa ni kinyume na Neno la Mungu, hapo tunamhuzunisha na hivyo ni rahisi kutuacha na tukaingiliwa na maroho mengine.

TUNAMZIMISHAJE?

Maandiko yanasema katika kitabu cha 1Wathesalonike 5:19 kuwa “Msimzimishe Roho”.. Maana yake Roho Mtakatifu anaweza kuzimika ndani yetu. 

Na tunamzimisha Roho kwa sisi kuacha kuomba, kuacha kufunga, kuacha kufanya ibada, kuacha kuifanya kazi ya Mungu, kuacha kumtolea, kuacha kumtukuza na kumsifu na kuifanya kazi yake na kuacha kuishi Maisha matakatifu. Mambo haya yanamfanya Roho Mtakatifu kuzimika ndani yetu, na hata kuondoka kabisa na kutuacha.

Bwana Yesu atusaidie tuzidi kudumu katika Neema yake na kuitunza zawadi nzuri ya Roho aliyotupatia (Matendo 2:39).

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako.

Mtakatifu ni Nani?

ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?

AKAZIDI KUENDELEA KATIKA HEKIMA NA KIMO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/05/usiniondolee-roho-wako-mtakatifu/