“Nitampiga mchungaji na kondoo wa kundi watatawanyika”,Maana yake nini?

by Admin | 12 August 2022 08:46 am08

Nini maana ya “Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika”. Kwanini Bwana Yesu apigwe? Na kwanini kondoo wake watawanyike!… Na je! Anayempiga ni nani?.

Tusome,

Mathayo 26:31 “Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika”

Bwana Yesu alipigwa na Mungu, lakini si kwasababu ya makosa yake, (yeye hakufanya dhambi hata moja, hakufanya kosa hata moja)…Lakini lakini ni kwasababu gani alipigwa??.. ni kwaajili yetu sisi..

Kumbuka Bwana Yesu hakuja kuiondoa adhabu, ambayo tayari ilikuwa imeshatolewa juu yetu..bali alikuja kuichukua adhabu.. Kwasababu kama ingekuwa kaja kuiondoa adhabu, basi hata yeye asingepanda msalabani(asingeadhibiwa)...Adhabu juu yetu tayari ilikuwa imeshatolewa, na ilikuwa ni lazima itekelezeke(Imfikie mlengwa).. Ni sawa na mtu akutupie jiwe kutoka mbali, na jiwe lile likiwa hewani, ghafla anatokea mtu anakaa mbele yako ili lile jiwe lisikupate wewe bali limpate yeye!..

Sasa kiuhalisia mtu huyo kakuokoa wewe na madhara ya jiwe lile, lakini hajaondoa madhara ya lile jiwe..au hajazuia jiwe lile lisirushwe kutoka kwa aliyerusha!!..Ni lazima limpate tu!..yeye kachukua tu maumivu yako, maana yake atachubuka yeye badala yako wewe, ataumia yeye badala yako wewe, atapigwa yeye badala yako wewe.. Mlengwa ulikuwa ni wewe, lakini yeye kajitokeza katikati ya safari ili yeye aumie wewe upone.

Ndicho Bwana YESU alichokuja kukifanya.. si kuondoa Adhabu iliyokwisha kutamkwa juu yetu na Mungu, si kuondoa laana iliyokwisha kutamkwa juu yetu, si kuondoa dhiki na mateso na masikitiko yaliyokwisha kukusudiwa juu yetu tangu siku ile pale Edeni, bali ni kuyachukua yeye hayo masikitiko, kuyachukua yeye hayo maumivu, kuyabeba yeye hayo mapigo..

Ndio maana maandiko yanasema…

Isaya 53: 4 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; LAKINI TULIMDHANIA YA KUWA AMEPIGWA, AMEPIGWA NA MUNGU, NA KUTESWA.

 5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, NA KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA”.

Umeona hapo?.. Tulipomwona kaangikwa msalabani, tulidhania kuwa Mungu kamwadhibu kwa makosa yake..Kumbe sio!.. Mungu shabaha yake ilikuwa ni kwetu sisi wala si kwake..lakini yeye akajitokeza kuyapokea yale mapigo!..Hivyo ni sawa na kusema KAPIGWA NA MUNGU KWA MAPIGO AMBAYO SI YAKE!!

Kwahiyo alipopigwa namna hiyo na MUNGU kwa mapigo ambayo si yake.. Kwa kitambo kidogo,  dunia ilikaa kimya!.. Wanafunzi wake (na wafuasi wake), walitawanyika kwasababu Mchungaji hayupo, walibaki bila mchungaji kwa kipindi cha siku tatu!..walikaa kwa huzuni na maombolezo wakati dunia inafurahia…Lakini baada ya kitambo kifupi, Bwana Yesu alipofufuka, ndipo wakakusanywa tena..

Yohana 16:19  “Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, BADO KITAMBO KIDOGO NANYI HAMNIONI, NA TENA BADO KITAMBO KIDOGO NANYI MTANIONA?

20  Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha”.

Hiyo ndio sababu ya Bwana Yesu kusema haya maneno…

Mathayo 26:31 “Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, NITAMPIGA MCHUNGAJI, NA KONDOO WA KUNDI WATATAWANYIKA”

Mungu alimpiga Bwana Yesu kwa kosa lisilo lake pale Kalvari, na kondoo wakatawanyika kwa kitambo..

Hivyo mimi na wewe baada ya kujua haya, na Mhanga, Bwana wetu Yesu Kristo aliouingia kwaajili yetu, basi tutazidi kuuheshimu  wokovu wetu kuliko kawaida..

Tunapotafakari kuwa tulipaswa tufe katika huzuni, katika tabu na baada ya hapo tutupwe katika ziwa la moto milele, lakini Bwana Yesu kaja kutuzuilia hilo, kwa kuchukua yeye laana zetu..basi tunajikuta tunakuwa wanyenyekevu mbele zake, na kuzidi kumheshimu Mungu katika maisha yetu, na kudumu katika Imani na utakatifu, na usafi.

Bwana Yesu atusaidie tuzidi kuuthamini msalaba!.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE! UNAMPENDA BWANA?

Gongo na Fimbo ni nini? Na vinawezaje kumfariji mtu? (Zaburi 23:4).

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

UAMINIFU NI KIGEZO KIKUBWA CHA KUTUMIWA NA MUNGU.

Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/12/nitampiga-mchungaji-na-kondoo-wa-kundi-watatawanyikamaana-yake-nini/