Kutazama bao ni kufanya nini?

by Admin | 22 August 2022 08:46 am08

Kumbukumbu 18:10 “Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu ATAZAMAYE BAO, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,

11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.

12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako……………….

14 Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na KUTAZAMA BAO; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo”.

Kutazama bao ni aina ya uchawi, ambayo inahusisha kuwasiliana na wafu, au miungu kwa njia ya kipande kidogo cha Ubao..

Katika Nyakati za kale, na hata nyakati za sasa katika baadhi ya sehemu, aina hii ya uganga bado inaendelea kufanyika…ambapo, watu Fulani maalum (ambao ni wachawi/waganga) wanakuwa na “Ubao” na huo ubao unakuwa umeandikwa maandishi fulani, pamoja na tarakimu, na alama fulani zisizoeleweka.

Ambapo mtu/watu wanapotaka kujua mambo yaliyopita au yanayoendelea sasa, au yatakayokuja, basi wanaketi kuuzunguka ubao huo, na kisha kuweka vidole vyao katika sehemu mojawapo ya huo ubao kufuatia maelekezo ya huyo mganga, na kisha wanapokea taarifa wanazozihitaji kutoka kwa hiyo miungu kupitia mganga huyo, au kupitia wao wenyewe.

Katika karne ya 19, uliibuka ubao mmoja maarufu ujulikanao kama  “Ubao wa Ouija”.  Ubao huu ulipata umaarufu katika bara la Ulaya na baadaye  katika bara la Marekani, ulitumika na wachawi wengi maarufu na watu wengi waliutumainia ikiwemo watu maarufu, ukiaminika kutoa taarifa nyingi za mambo yasiyojulikana, Ubao huo hata sasa unatumika lakini si maarufu kama ilivyokuwa katika karne hiyo ya 19.

Katika biblia Bwana Mungu aliwakataza wana wa Israeli “kutazama Bao” na ‘anatukataza hata sisi leo’. Kwasababu ni aina ya uchawi, na aliye nyuma ya ubao huo ni “shetani mwenyewe”.. akiwadanganya kuwa “ni wafu”. Hivyo ilikuwa ni kosa kubwa kwenda kutazama bao, ili kupata taarifa fulani zilizojificha.

Katika biblia tunamsoma mfalme mmoja wa Israeli aliyeitwa Manase, alikuwa ni mtu wa kutazama sana bao, jambo ambalo Mungu alishalikataza, na matokeo yake akajisababishia matatizo makubwa sana, kwani Mungu kumtoa katika ufalme kwa muda mpaka alipotubu.. na hata alipotubu bado madhara ya alichokuwa anakifanya hayakuondoka yote, kwani aliwakosesha Israeli na kuwafanya na wao kuwa watu wa kutazama bao. Na hivyo ikawa pia ni mojawapo ya sababu ya Mungu kuwapeleka utumwani Babeli.

2Wafalme 21:1 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba.

2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.

3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.

4 Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu.

5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana.

6 Akampitisha mwanawe motoni, AKATAZAMA BAO, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.

7 Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;

8 wala sitawapotosha Israeli miguu watoke katika nchi niliyowapa baba zao; wakiangalia tu na kufanya sawasawa na yote niliyowaamuru, na kwa kuishika torati yote aliyowaamuru mtumishi wangu Musa.

9 Walakini hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.

Mstari wa 6 hapo, unasema “AKATAZAMA BAO” Maana yake lolote lililokuwa linaendelea asilolijua, hakutaka kumwuliza Mungu, ajibuye kwa njia ya ndoto, au manabii wake, badala yake yeye “alikimbilia kutazama bao”.. Na hivyo akadanganywa pakubwa sana na shetani..akawa anafanya machukizo mengi, ikawa dhambi kubwa sana kwake.

Na jambo lilolomchukiza Mungu kipindi hicho, linamchukiza hata leo..

Leo hii idadi kubwa ya watu wanaohudhuria kwa waganga wa kienyeji  na kupewa maagizo ya kuweka viganja vyao juu ya vibao, au vibuyu, au mashuka, na kuambiwa mambo yao, hawajui kuwa wanafanya dhambi kama tu hiyo ya kutazama bao.  Vile vile watu wanaobashiri (wanaoBET), nao pia ni watu wanaotazama Bao.

Ndugu, kama unataka kuweka sawa mambo yako ya kiroho na ya kimwili, suliuhisho ni moja tu!, mpokee Yesu maishani mwako, huyo ndiye suluhisho, kwasababu yeye ndiye Njia, Kweli na Uzima.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI, TUNAPOMWOMBA BWANA ATUGUSE MARA YA PILI.

MADHARA YA KUTOIJUA KWELI YOTE!

NINI MAANA YA UCHAWI?

NI KIPI KINAMZUIA MUNGU KUZUNGUMZA NA SISI?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/22/kutazama-bao-ni-kufanya-nini/