Je mke wa Musa alikuwa ni Mweusi?

by Admin | 25 August 2022 08:46 am08

Je Sipora, mke wa Musa alikuwa Mkushi mwenye ngozi nyeusi?, Kulingana na  Hesabu 12:1? Na ni kwanini Miriamu na Haruni wamkasirikie Musa kwa kumwoa mwanamke Mkushi?, na kama alikuwa Mkushi mbona maandiko sehemu nyingine yanasema Yethro baba yake Sipora alikuwa ni Mmidiani na sio Mkushi?.. Au je! Musa alikuwa na mke mwingine tofauti na Sipora?

Jibu: Hapana! Maandiko hayaonyeshi kuwa Musa alioa mwanamke mwingine zaidi ya Sipora.

Sasa ili tujue kama Sipora alikuwa Mkushi au hebu kwanza tusome mistari ifuatayo..

Hesabu 12:1 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.

 2 Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. 

3 Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi”

Sasa Kushi lilikuwa ni Taifa gani?

Kushi ni taifa lijulikanalo kama Ethiopia kwasasa, Taifa hili lipo kaskazini mwa nchi ya Kenya, na kusini-mashariki mwa nchi ya Sudani. Wenyeji wa Taifa la Kushi(Ethiopia) ni watu wenye ngozi nyeusi tangu zamani za biblia na hata sasa. Tunalithibitisha hilo katika Yeremia 13:23.

Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya”

Umeona?.. hapo inamtaja Mkushi pamoja na ngozi yake, kwamba haiwezi kubadilika.. Kwahiyo mpaka hapo tumeshajua ngozi ya Sipora ilikuwaje?.. kwamba ilikuwa ni ngozi ya Kikushi.

Sasa swali ni je! Kama alikuwa ni Mkushi, kwanini biblia iseme baba yake alikuwa ni Mmidiani, Taifa la mbali kabisa, lililopo Mashariki ya kati, tena lenye watu wenye ngozi ijulikanayo kama nyeupe?.. na zaidi sana hata Sipora mwenyewe Musa alimpatia akiwa huko huko Midiani na sio Kushi?.

Jibu ni kwamba Yethro, baba yake Sipora, alikuwa ni Mmidiani kwa kuzaliwa, lakini kwaasili hakuwa mmidiani bali alikuwa ni Mkushi.

Ni sawa na Mzungu,au Mchina, au Mhindi aliyezaliwa katika Taifa la Tanzania, akakulia Tanzania, akaishi na watanzania, akasoma shule za kitanzania, na  hata lugha ya Kiswahili ya kitanzania akawa anaiongea.. kwa utambulisho wake ataitwa mtanzania, na atapata haki zote za kiraia…lakini  kwa asili sio Mtanzania bali ni Mzungu, au Mchina au Mhindi.

Ndivyo alivyokuwa Yethro, baba yake Sipora, alikuwa ni Mkushi kwaasili lakini Mmidiani kiuraia..(au kwa lugha rahisi, ni kwamba alikuwa ni Mkushi ambaye hakuzaliwa Kushi bali Midiani).

Ni sawa na Musa kipindi anakutana na hao mabinti wa Yethro, walikwenda kumtaja mbele ya baba yao kama Mmisri, lakini kiuhalisia Musa hakuwa Mmisri, bali mwebrania… Hivyo walimwita Mmisri kwasababu huenda aliwaambia katokea Misri.. Jambo ambalo ni kweli, Musa alikuwa ni Mmisri, kwa kuzaliwa, na kiuraia lakini hakuwa mwenye asili ya waMisri.

Kutoka 2:15 “Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.

 16 Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. 

17 Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.

 18 Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?

 19 Wakasema, MMISRI MMOJA ALITUOKOA KATIKA MIKONO YA WACHUNGAJI, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. 

20 Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.

 21 Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.

 22 Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni”

Swali lingine; Ni kwanini Miriamu na Haruni,  wakamkasirikie Musa kwasababu ya Mwanamke, Mkushi aliyemwoa?.. Je ni kwasababu alikuwa mweusi? Na ngozi nyeusi imelaaniwa?.

Jibu ni La!.. Hawakumkasirikia Musa kwasababu ya Rangi ya mke wake!..kwamba alikuwa mweusi na wao hawaipendi ngozi nyeusi,… la! Hiyo haikuwa sababu….

Sababu iliyowafanya wakasirike, ni kwasababu Yule alikuwa ni mwanamke wa kimataifa…

Maana yake ni kwamba hata kama asingekuwa Mkushi, lakini ni Mmisri, bado wangemkasirikia… vivyo hivyo hata kama angekuwa ni mzungu Yule mwenye uso mweupe kuliko wote, bado Miriamu na Haruni wangenung’unika.. kwasababu wayahudi na mataifa hawachangamani(kuoana).. Na mataifa walikuwa ni watu wote, nje na Taifa la Israeli.

Sasa swali la mwisho.. Kwanini Musa amwoe mwanamke wa kimataifa, na ilihali anajua kabisa haitakiwi kuwa hivyo?

Musa alimpata Sipora kabla ya sheria. Na ilipokuja sheria kuwa si ruhusa wao kuoa wanawake wa kimataifa, tayari Musa alikuwa na Sipora, hivyo asingeweza kumwacha!!!… na kipindi Mungu anatoa hiyo sheria ya kutooa wanawake wa kimataifa, ndio hicho hicho kipindi ambacho Musa na Haruni walinyanyuka kumlaumu. Kabla ya hapo utaona hawakuongea chochote.

Ni nini tunajifunza hapo?

Kwanza tunajifunza kuwa biblia haijichanganyi ni fahamu zetu ndizo zinazojichanganya.. Pili tunajifunza kuwa si sawa kumwacha mke wako baada ya wewe kuokoka, hata kama huyo mwanamke ni mpagani kiasi gani, wala si sawa kumwacha mume wako baada ya wewe kuokoka hata kama huyo mwanaume ni mpagani kiasi gani.. Ndicho biblia inachotufunza pia katika…

1Wakorintho 7:12  “Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.

13  Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.

14  Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu”

Lakini hiyo pia haitupi ruhusa kuoa wanawake wa kipagani, ikiwa tumeshaokoka tayari na tunataka kuoa, vile vile haitoi ruhusa kuolewa na mwanaume wa kipagani kama bado hujaolewa na unataka kuoelewa..

Kama umeshaokoka, na umesimama na  unataka kuoa/kuolewa.. ni sharti uolewe au uoe mtu mwenye imani moja na wewe, Bwana mmoja, roho mmoja, na Ubatizo mmoja.  Ukienda kutafuta binti wa kidunia na kumwoa hapo utakuwa umejifunga nira na wasioamini, jinsi isivyo sawa(2Wakorintho 6:14)..na unafanya machukizo yale yale walioyafanya watu wa kipindi cha Nuhu, yaliyowasababishia kuangamizwa kwa gharika (kwani wana wa Mungu waliowaona binti za wanadamu, wakawatamani na kuwaoa).

Hizi ni siku za Mwisho, kama hujampokea Yesu, fahamu kuwa hata uwe na maarifa kiasi gani, bado utapotea tu!, hivyo wokovu ni lazima!, kama unapenda maisha.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Midiani ni nchi gani kwasasa?.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI.

MJUMBE ASIYEKUWA NA UJUMBE.

BWANA alimaanisha nini kwenye mstari huu Marko 2:21″ Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kukuu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/25/je-mke-wa-musa-alikuwa-ni-mweusi/