HAMA KUTOKA GIZANI

by Admin | 13 September 2022 08:46 am09

Je unajua ni kwanini watu watahukumiwa?

Hebu tusome maandiko yafuatayo..

Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa NURU IMEKUJA ULIMWENGUNI, NA WATU WAKAPENDA GIZA KULIKO NURU; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu”.

Umeona sababu ya hukumu ya Mungu juu ya watu siku ile?.. Ni kwasababu watu walipenda GIZA kuliko NURU.

Nataka tulitafakari hilo neno “wakapenda” na hilo neno “kuliko”. Unajua mtu akikipenda kitu kuliko kingine, maana yake amekichunguza, akakitafakari na mwisho akachukua uamuzi wa kukichagua hiko kitu.

Na ndivyo Neno la Mungu linavyosema, kuwa hukumu yake itakuja juu ya watu, kwasababu “WATU WALIPENDA GIZA KULIKO NURU”. Ni heri kama Nuru isingekuwepo, halafu watu walipende giza!… lakini hapa inamaanisha Nuru ilikuwepo halafu watu wakalipenda giza kuliko Nuru… hilo ni jambo baya sana..

Hebu tafakari mpo ndani ya chumba chenye giza, halafu taa inawashwa na kumulika nyumba nzima, halafu ghafla unaanza kuona watu wanatoka kwenye hicho chumba chenye nuru, wanaelekea gizani, na zaidi ya yote hawataki kuja kwenye nuru!.. bila shaka utashangaa sana…

Ndicho Bwana Yesu alichomaanisha hapa kuwa watu kwa mapenzi yao wenyewe, wamechagua giza kuliko Nuru, ijapokuwa Nuru wameiona!..

Watu walipenda anasa kuliko kumcha Mungu, watu walipenda uchafu kuliko usafi, ijapokuwa tayari Nuru ilikuwepo (Roho Mtakatifu wa kuwatakasa alikuwepo, lakini hawakumtaka)…Watu walipenda ulevi, uzinzi, uuaji, ulafi, ufiraji, utukanaji, tamaa mbaya kuliko UTAKATIFU. Kwasababu hiyo basi hawatakuwa na udhuru siku ile (kulingana na Neno hilo).

Na ni kwasababu gani watu wanalipenda giza kuliko Nuru?, ni kwasababu matendo ya giza siku zote ni ya aibu, na yasiyokubalika na huwa hayapatani na mwanga.. Wezi wanaiba usiku, wachawi wanafanya shughuli zao usiku, walevi wanalewa usiku, hali kadhalika wazinzi, na makahaba wanafanya kazi zao katika giza…

Ayubu 24:15 “Tena jicho lake mzinifu hungojea WAKATI WA GIZA-GIZA, Akisema, Hapana jicho litakaloniona; Naye huuficha uso wake.

16 Wao hutoboa nyumba gizani; Hujifungia ndani wakati wa mchana; Hawaujui mwanga”.

Umeona tabia za wazinifu na watu wafanyao mabaya?..huwa zinasubiria kagiza kaingie!!..hawawezi kufanya shughuli zao mbele za watu!.

Yohana 3:20 “Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.

21 Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.”

Je! Na wewe umependa nini?,, umechagua nini?, NURU AU GIZA!, kwa matendo yako utatambulika umechagua nini, kamwe usimsingizie shetani!, kwasababu hapo Bwana hajasema “shetani akawachagulia kupenda giza” bali anasema “watu wakachagua wenyewe kupenda giza kuliko Nuru”. Kwahiyo ni watu wenyewe ndio wamechagua matendo ya giza, baada ya kukubali mapendekezo ya shetani.

Je! Na wewe umechagua nini leo?..kumbuka kama unafanya matendo ya giza, na huku unamjua Yesu…fahamu kuwa upo gizani, na umechagua giza kwa hiari yako mwenyewe, na upo hatarini kuangukia katika hukumu ya Mungu siku ile,.. Kwasababu Nuru ipo ulimwenguni na hujataka kuifuata, na Nuru hiyo si nyingine zaidi ya Yesu Kristo.

Yohana 9:5 “Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu”.

Amua leo kutoka katika hilo giza la ulimwengu, na kuja Nuruni.. na Unaingia Nuruni kwa kumwamini Bwana Yesu, na kupokea Roho Mtakatifu ambaye atakutakasa na matendo yote ya giza, na kwa kufanya hivyo utakuwa umetoka gizani na kuingia uzimani, na hivyo utakuwa ni mwana wa Nuru.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Hazina za gizani ni zipi? (Isaya 45:3).

MKUU WA ANGA.

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

Je ni kweli imani ya mtu ndiyo itakayomuokoa, na si kitu kingine?

Nuru yetu inapaswa iangaze au isiangaze kulingana na Mathayo 5:16 na Mathayo 6:1?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/09/13/hama-kutoka-gizani/