Nini maana ya kumpenda Bwana kwa moyo,roho, akili na nguvu zetu zote?

by Admin | 17 October 2022 08:46 pm10

Swali: Napenda kujua tunampendaje Bwana Mungu wetu kwa mioyo yetu yote, kwa roho zetu zote, kwa nguvu zetu zote, na kwa akili zetu zote kulingana na Mathayo 12:30.

Jibu: Tuanze kusoma kuanzia mstari wa 28..

Mathayo 12:28  “Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?

29  Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;

30  nawe mpende Bwana Mungu wako KWA MOYO WAKO WOTE, na KWA ROHO YAKO YOTE, na KWA AKILI ZAKO ZOTE, na KWA NGUVU ZAKO ZOTE.

31  Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi”.

Awali ya yote ni vizuri tukajua tofauti ya “OMBI” na “AMRI”. Ombi ni kitu ambacho unaombwa ukifanye, na endapo usipokifanya basi huwezi kuhesabiwa makosa, kwasababu ni Ombi, (lina uchaguzi wa kukubali au kukataa) lakini AMRI ni kitu ambacho mtu unaamriwa kukifanya (iwe unapenda au hupendi, ni sharti ukifanye), na endapo usipokifanya basi inakuwa ni kosa!.

Sasa hapo Bwana Yesu aliposema kuwa “AMRI” ya kwanza ni kumpenda Bwana Mungu kwa moyo wote, roho yote, akili zote na nguvu zote, Hiyo Ni AMRI na si OMBI. Maana yake mtu yeyote asiyempenda Bwana Mungu wake kwa viwango hivyo, basi mtu huyo kavunja amri ya Kwanza na ataenda kuhukumiwa!.

Ndio maana Mtume Paulo kwa uweza wa Roho aliandika maneno haya..1Wakorintho 16:22  “Mtu awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa. Maran atha”.

Maana yake kutompenda Bwana ni laana kubwa!.. kwasababu ni kuvunja amri ya kwanza.

Sasa tukirudi kwenye swali letu, Nini maana ya kumpenda Bwana kwa moyo wote, roho zote, akili zote na nguvu zote?

1.KWA MOYO WOTE

Kufanya kitu kwa moyo maana yake ni kukifanya kitu kwa hiari.. pasipo kuwa na mambo au mawazo  mengine ya kando kando, kama malalamiko, manung’uniko, majivuno, au pasipo kusukumwa sukumwa.

Kwahiyo maana ya kumpenda Mungu kwa Moyo wote, maana yake ni kumpenda Mungu pasipo masharti.. Maana yake kama unamtolea Mungu zaka, au sadaka basi unamtolea kwa kupenda wewe mwenyewe,na si kwasababu umeshurutishwa au kwasababu biblia inasema tumtolee…hapana bali unamtolea kana kwamba hakuna sheria yoyote iliyokuambia ufanye hivyo..

Vile vile kama unamtumikia, katika kuhubiri, kumwimbia, kusaidia wengine n.k basi unapaswa umtumikia kwa moyo, kana kwamba hakuna sheria iliyokuambia ufanye hivyo…

Luka 17:10 “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya”

2. KWA ROHO YOTE

Roho siku zote ni chumba cha IBADA… Na mtu anayefanya ibada kwa Mungu maana yake anamwabudu Mungu, kwasababu neno lenyewe “Ibada” limetokana na Neno “kuabudu”..

Yohana 4:23 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba KATIKA ROHO NA KWELI. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu”.

Ukimpenda Bwana kwa Roho yote, maana yake kila wakati utatafakari na kutafuta kumfanyia Mungu ibada iliyo kamilifu… hutafanya ibada iliyo nje na Kweli ya Mungu.. Kila siku utahakiki ibada unayoifanya kama ni katika roho na katika Kweli ya Mungu (Neno la Mungu), na utaifanya hivyo kwa bidii sana. Hutamchanganya Mungu na sanamu!, wala hutamchanganya Mungu na matambiko ya kimila, wala hutakuwa vuguvugu katika Imani yako…utajituma kufika ibadani siku zote, utajituma kuomba siku zote na mambo yote ya kiibada yatakuwa ni mambo ya kwanza katika maisha yako.

3. KWA NGUVU ZAKO ZOTE.

Wakati wa kuwa na NGUVU ni wakati wa “Ujana”.. Hiki ndicho kipindi ambacho watu wote wanapaswa watie bidii katika kumtafuta Mungu.

1Yohana 2:14b  “… Nimewaandikia ninyi, vijana, KWA SABABU MNA NGUVU, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu”.

Wakati wa ujana ni wakati ambao roho zetu zinakuwa na uwezo mkubwa wa kutunza maneno ya Mungu, kuliko wakati wa uzee.. Kiasi kwamba mtu anayeyasoma maandiko katika ujana ni rahisi maandiko yale kukaa ndani yake kwa muda mrefu na kuzaa matunda zaidi ya mtu mzima (mzee), jambo ambalo shetani analiogopa sana!.. Ndio maana hapo maandiko yanasema.. “Nimewaandikia ninyi, vijana, KWA SABABU MNA NGUVU, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, NANYI MMEMSHINDA YULE MWOVU”.

Vile vile katika kitabu cha Mhubiri 12:1 maandiko yanasema “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.

Maana yake itafika kipindi (utakapokuwa mzee) utatamani Neno la Mungu likae na  kudumu ndani yako lakini halitakaa na hivyo utakosa furaha, kwasababu Nguvu zako zitakuwa zimeisha.

Kwahiyo maana ya kumpenda Bwana kwa nguvu zote maana yake ni kumpenda BWANA katika ujana wako wote; unatumia muda mwingi katika kuomba maadamu unazo nguvu za mwili, vile vile unatumia muda mwingi katika kwenda kuhubiri maadamu unayo miguu yenye nguvu, pia unatumia muda mwingi katika kujifunza Neno la Mungu katika miaka ya ujana ambayo unazo nguvu katika roho za kuyatunza maneno ya Mungu.

Wengi wanasema nitamgeukia Mungu na kumtumikia nikiwa mzee.. kamwe usijaribu kuwaza hivyo!..biblia inasema kama unamkataa Mungu leo, utakapofikia uzee hutakuwa na Furaha wala Nguvu (Mhubiri 12:1).

Na pia Bwana Yesu alimwuliza Petro mara tatu, kama anampenda angali akiwa kijana..na akamwambia ukweli kuwa kama hatajishughulisha sasa katika kumtafuta yeye, na kumtumikia angali akiwa  kijana, basi asitegemee ataweza akiwa mzee, kwasababu wakati wa uzee hatakuwa na hizo nguvu, bali atapelekwa huku na huko mahali asipopataka..

Yohana 21:15  “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, WEWE WANIPENDA KULIKO HAWA? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.

16  Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, WANIPENDA? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu.

17  Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, WANIPENDA? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.

18  Akasema, Amin, amin, nakuambia, WAKATI ULIPOKUWA KIJANA, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka

4. KWA AKILI ZAKO ZOTE.

Akili ni utashi wa kufanya mambo na kuyarahisisha yale yanayoonekana kuwa ni magumu… Kila mtu anazo akili za mwili alizojaliwa na Mungu, (Ingawa dhambi inaweza kumfanya mtu aonekane hana akili kabisa mbele za Mungu).

Hivyo kama umejiepusha na dhambi basi unazo akili, Hivyo katika hizo ulizopewa zitumie katika kumtumikia Mungu na kumtafuta.

Kwamfano katika dunia ya sasa, huwezi kusema utamtafuta Mungu halafu umkose, ikiwa umedhamiria kweli kumtafuta kwa akili zetu zote.. Yeye (Mungu) anasema tukimtafuta tutamwona (Yeremia 29:13).

Hebu tafakari Leo hii kuna simu nyingi feki kuliko orijino masokoni, lakini pamoja na kwamba feki ni nyingi mno kuliko orijino, lakini utaona kuna mtu anaitafuta orijino mpaka anaipata!.. Utaona anaulizia huku na huku, na kufanya uchunguzi huu na ule, mpaka anafikia kujua vimelea vya orijino na feki, na hatimaye anaipata iliyo orijino na kuiacha feki. (hapo ametumia akili zake zote kuitafuta simu orijino mpaka kaipata).

Lakini katika kumtafuta Mungu, utasikia mtu anakuambia “siku hizi manabii wa uongo wengi, sijui tumwamini yupi tumwache yupi” Hivyo anaamua tu!, kuacha kumtafuta Mungu, au kwenda kanisani..kwasababu tu manabii wa uongo wengi, au kwasababu tu, upotofu ni mwingi..

Mtu kama huyu hajaamua kutumia akili yake yote katika kumtafuta Mungu!! Ni mvivu wa akili.. kwasababu anao uwezo wa kutumia akili yake yote kutafuta simu orijino katikati ya feki, lakini si kuutafuta ukweli wa Mungu katikati ya uongo.

Lakini kama angeamua kutumia akili yake kidogo tu, na kuanza kuchambua hao wa uongo kupitia neno la Mungu, na kutafuta huku na huko, na kuulizia ulizia, na kutafiti tafiti, ni wazi kuwa siku moja angefika katika ukweli, na angewasaidia pia na wengine..

 Lakini anadhani kwa yeye kutomtafuta Mungu siku ile atatoa udhuru mbele za Mungu, pasipo kujua kuwa anaivunja amri ya kwanza ya Mungu, ya kumpenda yeye kwa akili zote.

Ndugu Dada/Kaka.. Usipomtafuta Mungu sasa katika nyakati hizi, usipompenda kwa moyo wako wote na roho yako yote, na nguvu zako zote na akili zako zote, fahamu kuwa siku ya mwisho hutakuwa na udhuru, wala hakuna mwanadamu yoyote atakayekuwa na udhuru.

Bwana Yesu atusaidie tumpende yeye kwa vitu hivyo vinne kwa bidii sana.

Maran atha!.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ILI TUONEKANE SAFI MBELE ZA MUNGU TUFANYE NINI?

Mtu asiye na akili ni nani kibiblia?

Watu wenye ulemavu wa akili, wataenda mbinguni?

Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

NINI KINAFUATA SIKU ILE ILE YA KUOKOKA!

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/10/17/nini-maana-ya-kumpenda-bwana-kwa-moyoroho-akili-na-nguvu-zetu-zote/