KONDE LA DAMU (Akeldama).

by Admin | 1 November 2022 08:46 pm11

Shalom, karibu tujifunze biblia.

Leo napenda tujifunze juu ya lile Konde Yuda alilolinunua.. Biblia inaliita kuwa ni “konde la Damu”. Tafsiri na konde ni “shamba/kiwanja”.. Hivyo Konde lolote lililopatikana au kununuliwa kwa fedha za mauaji lilijulikana kama “konde la damu”.

Na maandiko yanaonyesha kuwa Yuda alilinunua shamba kwa fedha/kima cha mauaji.. Na hakulinunua kwa matakwa yake, bali Maukuhani ndio waliokwenda kulinunua, lakini hati ya kile kiwanja ikaandikwa kwa jina la YUDA!.. kwasababu ni fedha zake ndizo zilizonunulia kiwanja hicho..

Sasa tendo walilolifanya makuhani kwenda kununua mahali pa kuzika wageni lilikuwa ni tendo la heshima na lenye kugusa hisia za wengi, kwani katika desturi za wayahudi ilikuwa wageni na Wayahudi hawazikwi mahali pamoja, sasa ilikuwepo changamoto ya wageni kutoka mbali wanaokuja Yerusalemu na kufia huko, changamoto ya mahali pa kuwazika ilikuwa kubwa, kwahiyo hawa makuhani kitu walichofanya kilikuwa ni cha kiungwana.. Hivyo wakaenda kununua sehemu ya gharama ya juu, katikati ya Yerusalemu karibu na bonde la mwana wa Hinomu.

Lakini sasa watu walipoulizia ni nani kanunua konde lile na kiasi kilichotolewa, siri ikajulikana kuwa kiwanja kile kilinunuliwa na mtu mmoja (marehemu) aliyeitwa Yuda kwa fedha iliyotokana na kumsaliti Bwana Yesu. Kwahiyo kila aliyepita karibu na kiwanja hicho na kuulizia habari za kiwanja hicho na mmiliki, basi alisimuliwa habari ya Yuda.. Hivyo kiwanja kile kikawa na sifa mbaya kutokana na tukio la Yuda.

Ni sawa sasahivi upite mahali uone jengo limejengwa na linatoa huduma Fulani nzuri…halafu unaambiwa jengo lile limejengwa kwa fedha za ujambazi/mauaji yaani mmiliki wa jengo aliua watu Fulani ili kupata fedha za kujenga hilo jengo. Bila shaka, hata kama lile jengo linafanya kazi nzuri kiasi gani, bado sifa yake itabaki kuwa mbaya. Ndivyo na konde alilolinunua Yuda.

Mathayo 27:3 “Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.

4  Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

5  Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.

6  Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu.

7  Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

8  Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo”.

Habari hii tunaweza kuisoma tena vizuri katika Matendo 1:16-19.

Matendo 1:16 “ Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu;

17  kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii.

18  (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.

19  Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.)”

Ni nini tunajifunza katika habari hii?

1. Ukifanya jambo baya litakuja kujulikana tu hata baada ya kufa kwako!.

Yuda alimsaliti Bwana mbele ya wanafunzi wake 12 tu!, pengine wale wanafunzi wangeshuhudia kuwa Yuda ni msaliti wasingeaminika, lakini LILE KONDE lilikuja kumtangaza Yuda kwa watu wote, hata ambao walikuwa hawamjui walimjua kupitia konde lile. Vile vile Daudi alimfanyia ubaya Uria, kwa kumwua na kumchukua mke wake, jambo lile alilifanya kwa siri, lakini Mungu alikuja kulitangaza mbele ya jua, mpaka leo tunalisoma tukio lile.

2. Mali ya dhuluma ni lazima iishie kuwa na sifa mbaya.

Haijalishi mali ya dhuluma itadumu kuwa na heshima kwa muda gani, utafika wakati heshima yake itapotea na itabaki aibu!!.. Kama umepata nyumba kwa dhuluma mwisho wake utakuwa ni aibu, kama umepata shamba kwa dhuluma mwisho wake utakuwa ni aibu, na kitu kingine chochote kama ni cha dhuluma mwisho wake ni aibu.

Vile vile kama umemwibia Bwana kwa matoleo yako, na ukatumia matoleo yale kufanya mambo yako ikiwemo kununua shamba kama Yuda, basi utaishi kuwa kama Yuda.

Vile vile kama unamsaliti Bwana na injili yake kwa kazi yako, au uzuri wako, au hadhi yako, au fedha zako au kwa chochote kile, basi fahamu kuwa unaelekea mahali pabaya.

Bwana Yesu atusaidie tuishi maisha ya uangalifu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UNAWAZA NINI SASA, JUU YA UFALME WA MBINGUNI?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Je Mtu anaweza kusema uongo, Na Mungu akambariki?

Paulo alikuwa na maana gani aliposema “nimeaminiwa uwakili”

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/01/konde-la-damu-akeldama/