USIZISHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE.

by Admin | 11 November 2022 08:46 pm11

1Timotheo 5:22 “Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi”.

Hapa tunaona mtume Paulo, anampa Timotheo maagizo ya namna ya kuwa kiongozi bora (Askofu bora) wa makanisa la Mungu. Utaona anampa maagizo ya utaratibu wa kuwaandika wajane, kwamba ahakikishe wanaoandikwa ni wale walio wajane kweli kweli. (soma 1Timotheo 5:9-16).

Pia utaona anampa vigezo vya uongozi kwa viongozi wapya wa makanisa mapya, kwamba wanapaswa wawe wameshuhudiwa kuwa na sifa njema…ndipo awawekee Mikono!, lakini asiwe mwepesi wa kuwawekea mikono kwa haraka.

Na pia viongozi wa makanisa (yaani wachungaji, maaskofu na wote wanaosimama kama viongozi wa kanisa) basi wanapaswa wapewe heshima maradufu, maana yake Wakumbukwe katika riziki na mahitaji yao mara dufu zaidi ya wengine, kwasababu wanakesha kwaajili ya roho za watu, kuwaombea na kuwachunga na kufundisha.

1Timotheo 5:17  “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.

18  Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake”

Na zaidi sana asikubali Mashitaka ya Wazee kwa haraka, (Juu ya wachungaji, au mashemasi)..isipokuwa kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.. kwamaana ibilisi anapenda kuwatumia watu kuzusha jambo Fulani la uongo juu ya kiongozi wa kanisa, lengo lake likiwa ni kuliharibu kundi hilo..

Kwahiyo hapa Mtume kwa uongozo wa Roho anamwonya Timotheo asiwe mwepesi kusikiliza au kuamini maneno yazungumzwayo au mashitaka yaletwayo dhidi ya viongozi wa makanisa.. Bali alichunguze jambo kwa makini mpaka atakapopata uthibitisho kamilifu kwa vinywa vya mashahidi wengi.

Lakini la mwisho kabisa Paulo anamwambia Timotheo kuwa ASIZISHIRIKI DHAMBI ZA WENGINE!.

1Timotheo 5:22 “Usimwekee mtu mikono kwa haraka, WALA USIZISHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE. UJILINDE NAFSI YAKO UWE SAFI”.

SASA NINI MAANA YA KUZISHIRIKI DHAMBI ZA WENGINE?

Kwanza ni muhimu kufahamu hao “wengine” wanaotajwa hapo ni akina nani?.. Wengine wanaotajwa hapo sio watu wa mataifa (yaani ambao hawajaokoka), la! Bali wengine wanaotajwa hapo ni “watu walio ndani ya Kanisa”. Watenda dhambi hawapo tu Bar!, au kwenye madanguro..bali wapo wengi pia kanisani.

Sasa Mtu wa kanisani anapofanya dhambi na wewe ukaiona na kuifanya kama hiyo hiyo? Maana yake na “wewe umeishiriki ile dhambi”, Kwamfano unapomwona mtu kaingia kanisani kavaa Nusu tupu, au kavaa nguzo zinazobana au zisizo na maadili, na wewe ukaona na ukamwiga, siku inayofuata na wewe ukavaa kama yeye..basi hapo kibiblia umeshiriki dhambi za huyo mwingine, hata kama kanisa zima linafanya mambo yasiyofaa sisi tunapaswa kushiriki dhambi zao, Kwasababu kuna madhara makubwa sana ya kushiriki dhambi za wengine.

Vile vile inawezekana wewe ni Mwimbaji ndani ya kanisa, lakini kuna waimbaji wenzako matendo yao ni ya giza, maandiko yanatuonya tusishiriki dhambi zao, maana yake tusiwe kama wao..

Vile vile wewe kama ni kiongozi (Mchungaji, askofu, shemasi)..halafu ukamwona kiongozi mwingine anafanya mambo yaliyo kinyume na maandiko, aidha ni mla rushwa, au ni mwizi, au mzinzi, au mlevi na anafanya mambo mengine mabaya na wewe ukaiga ule ubaya au ukaufumbia macho..kibiblia umeshiriki dhambi zake huyo kiongozi.

Na hapa Mtume Paulo anamwonya Timotheo kuwa ajihadhari asije akashiriki dhambi za wengine, ajilinde nafsi yake awe safi.

SASA MADHARA YA KUSHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE NI NINI?

Unaposhiriki dhambi za mwingine, maana yake MAPIGO nayo mnashiriki sawasawa, na LAANA pia mtashiriki sawasawa, maana yake kama Mungu amemkusudia kumwangamiza kabisa mtu huyo kutokana na tabia yake ya wizi anaoufanya kila siku ndani ya Nyumba ya Mungu, na wewe ukamwiga kwakufanya mara moja moja tu.. basi mtashiriki kiwango cha adhabu sawa.. Wewe unayeiba mara moja moja na Yule anayeiba kila siku wote kiwango chenu cha adhabu kitafanana, kwahiyo utajikuta wewe unayefanya kidogo mnapata adhabu sawa na Yule anayefanya sana.

Ndio maana Paulo anamwonya Timotheo asizishiriki dhambi za wengine, bali ajilinde nafsi yake awe safi.. Na sisi hatuna budi kuzilinda nafsi zetu ziwe safi.. Na tujiepushe na dhambi za wengine.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

REKEBISHA YAFUATAYO ILI MAMBO YAENDE SAWA.

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

Je ni kweli miaka yetu ya kuishi ni 80 tu (kulingana na Zaburi 90:10).

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/11/usizishiriki-dhambi-za-watu-wengine/