EPUKA MAKUNDI ILI UTAKATIFU WAKO UDUMU!.

by Admin | 14 November 2022 08:46 am11

Silaha moja shetani anayoitumia kuharibu maisha ya kiroho ya watu wengi, hususani vijana ni MAKUNDI!..

Na mtu mkamilifu ni Yule anayeweza kuchagua aina ya watu wa kutembea naye. Biblia inatufundisha kuwapenda watu wote, lakini si kuambatana na watu wote.

2Wakorintho  6:14  “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani KATI YA HAKI NA UASI? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”

Umeona?..maana yake ni kwamba kama unaambatana na mtu ambaye si wa aina yako, basi unajiharibu mwenyewe!, Baada tu ya kumkiri Yesu, jambo lingine la muhimu linalopasa kufuata ni KUCHAGUA AINA YA WATU, utakaoanza kuwa nao karibu, kuanzia huo wakati na kuendelea.

Wengi wanalikwepa hili na mwisho wa siku wanajikuta wameurudia ulimwengu tena kwa kasi kubwa.. Ndugu ukishaokoka yale makundi ya walevi uliyokuwa unashinda nayo, ni sharti uyaache!, ukishaokoka zile saluni ulizokuwa unaenda ambazo kutwa kuchwa ni kuzungumzia mambo ya watu wengine, unaziacha.. Ukishaokoka wale watu uliokuwa unakula nao rushwa, au unaiba nao unawaacha!

Sasa unawaachaje?

Awali ya yote unapaswa uwaambie na uikiri imani yako mbele yao, na endapo wakikusikia na wao wakakubali kubadilika na kuwa kama wewe basi utakuwa umewapata, lakini kama hawataki kubadilika na zaidi sana njia zao ni zile zile, basi hapo UNAPASWA UWAACHE!!, Kwa usalama wa roho yako, anza kutafuta marafiki wengine wa imani moja na wewe, hao panga ratiba mara chache chache kwenda kuwatembelea na utakapowatembelea habari utakazowapelekea ni za injili kuanzia mwanzo wako hadi mwisho wako.

Na kamwe usijaribu kuwaza kuwa unaweza kuwa shujaa na kwamba hawataweza kukurudisha nyuma endapo utashikamana nao..Ni kweli katika siku za mwanzo unaweza kujiona wewe ni mshindi, lakini nataka nikuambie kwa kadiri siku zitakavyozidi kwenda tabia yako njema kidogo kidogo itaanza kuathirika, na baada ya kipindi fulani, utajioni umepoa kabisa na kufanana na hao, au kuishia kuwa mkristo vuguvugu tu!.

Ukitaka ukristo wako uimarike siku baada ya siku, watafute wakristo wa kweli ungana nao!..na iache kampani mbaya!.. binti ukitaka udumu katika kuvaa vizuri na kwa heshima, na katika usafi watafute mabinti wenzako wa imani kama yako hiyo, dumu nao hao!.. utautunza utakatifu wako kwa viwango vya juu.. lakini ukitaka kuanza na moto na kuishia baridi, basi endelea na makundi yale yale uliyonayo baada ya kuokoka. (Maisha yako ya wokovu hayatafika mbali).

Vile vile ukitaka kudumu katika eneo la Maombi, yaani uzidi kuwa mwombaji, na mtu wa ibadani na mtu wa kumpenda Mungu, sharti uwatafute watu wa namna yako!.. ambao ni wacha Mungu tena wanaopenda maombi, lakini kama hutawatafuta hao na ukasema mimi ninaweza kuendelea kuwa mwombaji hata nikiwa na makundi yangu yale yale, nataka nikuambie ndugu yangu, unapoteza muda.. mwisho wako utakuwa mbaya sana, na hautajua ni saangapi umepoa kiroho au umeanguka kabisa.

Sasa tunazidi kulithibitisha vipi hili kimaandiko?

Tusome,

2Timotheo 2:22  “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, PAMOJA NA WALE WAMWITAO BWANA KWA MOYO SAFI”.

Hapo anasema tuzikimbie tamaa za ujanani, tukatafute “haki, imani, upendo  na amani.” Lakini sasa tunatafuta hii haki, imani, upendo na amani pamoja na watu gani???..je! pamoja na walevi?, au pamoja na wazinzi?, au pamoja na watu wenye mizaa? Au pamoja na wahuni?..jibu ni la! Bali pamoja na WALE WAMWITAO BWANA KWA MOYO SAFI!!... Na wanaomwita Bwana kwa moyo safi si wengine zaidi ya wale wakristo waliosimama kikweli kweli, ambao Bwana kawapanda kila mahali.

Ukidhani kuwa unaweza kulirekebisha hilo andiko na kwamba  wewe unaweza kwenda kutafuta Imani pamoja na walevi, unapoteza muda!, ukidhani unaweza kuitafuta amani na kuipata pamoja na wazinzi,  au wahuni, au wauaji, au watu wa masengenyo basi nataka nikuambia kuwa unapoteza muda wako mwingi..Hata mwanafunzi hawezi kupata maarifa yoyote ya darasani endapo akikaa na wanafunzi wasiopenda shule, lakini akikaa na wenzake wapendao shule basi atapata faida anayoitafuta.

Vile vile na wewe leo hii, punguza makundi ya watu wa kidunia, na ongeza makundi ya watu wamwitao Bwana kwa moyo safi.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

EPUKA MUHURI WA SHETANI

EPUKA KUCHELEWA IBADA.

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.

EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/14/epuka-makundi-ili-utakatifu-wako-udumu/