EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.

EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.

Kuna swali limeulizwa na wasomaji wetu hapa..

“Bwana Yesu asifiwe mtumishi, pole na hongera na majukumu, mtumishi Mimi nilitaka kufahamu kuhusu Yohana mbatizaji, yeye ndiye aliyembatiza Yesu mwana wangu tena akasema nalishuhudia Roho wa Mungu akishuka kama hua toka mbinguni akatua juu yake tena yeye aliyempeleka yaani Mungu akamwambia yule utakayeona Roho akishuka juu yake huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho mtakatifu na kwa Moto, tena Yohana anawahakikishia kwamba ajaye nyuma yake huyo ni mkubwa kuliko yeye na ya kwamba alikuwako kabla yake…..Sasa swali kwanini alipokuwa gerezani anatuma wanafunzi wake wakamuulize kuwa yeye ndiye Yesu au tumtazamie mwingine? Ina maana alichotushuhudia mwanzo kuwa ajaye ni mkuu na alimuona Roho akishuka juu yake bado hakuamini kuwa ni yeye? Asante, Mungu akusaidie katika kujibu”.


Jibu:

Ni kawaida ya mwanadamu pale anapoahidiwa kitu au anapoonyeshwa jambo fulani na Mungu, wakati huo huo kuanza kuundia matarajio yake mwenyewe juu yake jinsi ahadi hiyo  itakavyotimia.. Sasa pale maono hayo yanapotimia nje ya hayo matarajio yake mwenyewe, inakuwa ni rahisi sana kutetereka kama sio kuiacha Imani kabisa.

Katika mazingira ya Yohana mbatizaji, Sio kwamba hakuamini alichoonyeshwa, aliamini na kujua kabisa Yesu Kristo ndio yule aliyekuwa anatarajiwa kwa muda mrefu,. Lakini shida ilianza kutokea pale alipoanza kubuni matarajio yake  mwenyewe, ambayo wakati mwingine sio kwamba yalikuwa sio sahihi, hapana pengine yalikuwa ni ya kutimia baadaye kabisa, sio kwa wakati ule.

Sasa alipoona Yesu hajaja kama mfalme, akiwa na pepeto mikononi mwake kukusanya ngano ghalani na makapi kuyachoma motoni, kama alivyoonyeshwa (Mathayo 3:12) kinyume chake amekuja katika upole na unyonge, anakataliwa na watu hiyo ikampelekea baadaye aanze kutilia shaka.. Labda pengine atakuwa sio huyu..

Umeona, hata leo hii, Mungu anawapa watu wengi ahadi ya mambo fulani, na wanajua kabisa ni Mungu amewajibu pengine walijibiwa kwa ndoto, au maono, au sauti, au ishara n.k. lakini kwa bahati mbaya, wameyatilia shaka, kama sio kuyaacha kabisa maono hayo kutokana na kuwa waliyaruhusu matarajio yao yatawale maono hayo Mungu aliyowapa.

Kwa mfano utakuta mwanamke Fulani, ameahidiwa na Mungu kwamba kabla ya miaka mitano atakuwa na watoto watatu. Sasa badala asubiri maajabu ya Mungu , yeye muda huo huo anaanza kujiundia matarajio yake, kwamba  mwaka wa kwanza atapata mmoja, kisha baada ya miaka miwili atapata mwingine , na mingine atakuja baada ya miaka mingine miwili ya mwisho kupita ili kutimiza mitano.

Sasa matarajio hayo sio mabaya, lakini yana athari pale ambapo atakapoona wakati huo unapita bila ya yeye kuona chochote, mwaka wa kwanza unapita, wa pili nao hivyo hivyo haioni chochote, watatu, na wanne hivyo hivyo.. hapo ndipo mtu huyo anapoanza kutilia shaka kudhani pengine Mungu hakusema naye, pengine Mungu hakumjibu, pengine maono yale yalimaanisha kitu kingine, pengine hivi, pengine vile, pengine kuna mahali alimkosea Mungu..

Unaona? Mwisho wa siku anayaacha kabisa, na kuanza kuhangaika tena. Lakini kama angekuwa mtulivu na kuamini kuwa ni Mungu aliyemjibu, angesubiria matarajio ya Mungu yatende kazi,  pengine Mungu amempangia mwaka wa tano ule wa mwisho apate ujauzito wa watoto mapacha watatu.

Ndicho kilichotokea kwa Yohana mbatizaji, hiyo inatufundisha kuwa Pale Mungu anapotuahidi kitu, basi tumwamini vile vile alivyotuonyesha, bila kuongezea matarajio yetu juu yake, na hapo ndipo tutakapoweza kuishi maisha ya kutotilia shaka maneno yote ya Mungu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?

WAKATI AHADI INAPOKARIBIA, HUWA KUNA MAMBO YANATOKEA.

Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments