NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?

Biblia inatuonyesha Dema na Marko walikuwa ni watenda kazi wazuri sana pamoja na Mtume Paulo, Tunayasoma hayo katika kitabu cha Filemoni 1:24

“na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami”.

Lakini pamoja na kwamba walikuwa ni watenda kazi pamoja na Paulo, tunaona kila mmoja alikuwa na historia yake tofauti, ambayo leo hii tunaweza kuitazama na kupata funzo ndani yake.

MARKO

Tukianzana na huyu Marko, mwanzoni kabisa mwa huduma ya mtume Paulo, ya kuipeleka injili kwa watu wa mataifa, utaona akiwa na Barnaba, walimchukua pia huyu Marko kama msaidizi wao katika safari yao ya utume Mungu aliowapa. Lakini kama tunavyosoma katika maandiko, walipopita nchi kadhaa wa kadha, ghafla Marko alibadilika tabia, hatujui sababu ni nini iliyomfanya awe vile pengine, aliona kazi ile ni ngumu, au aliona haina faida yoyote.. Na hatimaye akawaacha Paulo na Barnaba solemba katika kilele cha utumishi, akarudi zake alipotokea, (Soma Matendo 13:13)

Jambo hilo liliwaumiza kama sio kuwafadhaisha sana mitume hususani Paulo, kuona kwamba mtu ambaye angepaswa kuwafariji na kuwatia moyo ndio anakuwa wa kwanza kuwakimbia. Na ndio maana wakati wa ziara ya pili, Paulo alipotaka tena kusafiri kwenda kuyathibitisha makanisa, aligoma kwenda na huyo Marko shambani mwa Bwana, Kwasababu alijua kigeugeu chake.

Matendo 15:37 “Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.

38 Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini.

39 Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro”.

Lakini pamoja na hayo biblia inatuonyesha huyu Marko alikuja kugeuka baadaye , pengine alitubu na kutambua makosa yake, akaona hapa naelekea kulipoteza taji langu, hivyo akaendelea kufanya utumishi wa Mungu, na baadaye kabisa utaona mtume Paulo akimpokea tena, akisema ni mtenda kazi pamoja naye. Na huyu Marko ndiye aliyekiandika hicho kitabu cha Marko ambacho mpaka leo hii tunakisoma.

DEMA

Sasa tukimtazama na mtendakazi wake mwingine aliyejulikana kama Dema, yeye alikuwa katika utumishi mzuri sana na Paulo, pengine tangu mwanzoni kabisa mwa huduma alikuwa naye, lakini ilifika wakati pengine kwa kuona kuna ugumu fulani, akaamua kabisa kuachana na utume, hivyo akamwacha mtume Paulo peke yake vifungoni, ni heri angemwacha tu, kisha aende kuifanya kazi ya Mungu sehemu nyingine.. Lakini mtume Paulo anasema, aliupenda ulimwengu huu.

Yaani aliacha kabisa utumishi wa Mungu akayarudia mambo ya kale ya ulimwenguni, na wala hakurudi tena shambani mwa Bwana. Embu fikiria mtu huyu jinsi alivyouvunja moyo wa Mungu na Paulo. Pengine mwenzake Marko alikuwa anamwangalia, na kumwonya asifanye hivyo, kwasababu mwisho wake utakuwa ni mbaya, kwasababu yeye naye alijaribu kufanya hivyo lakini hakuona faida yoyote, lakini Dema hakusikia akaona ni heri arudie anasa zake, zile ziara zote za kuzunguka kuhubiri injili ndio mwisho, hakuna faida yoyote. Nitarudia miradi yangu mikubwa n.k.

2Timotheo 4:10 “MAANA DEMA ALINIACHA, AKIUPENDA ULIMWENGU HUU WA SASA, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia”.

Sasa mambo haya tunaweza kudhani hayatokei hata sasa.

Biblia inasema, TUISHINDANIE IMANI, ambayo tumekabidhiwa sisi watakatifu mara moja tu.

Yuda 1:3 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.”

Unaona Mungu hategemei sana mwanzo wetu, anautazama na mwisho wetu utakuwaje. Kama Dema alikuwa ni mtendakazi mzuri sana, mpaka Mtume Paulo anajivunia kwa kumtaja katika nyaraka zake nyingi, usidhani hakukuwa na watendakazi wengine wakati ule, walikuwepo,  lakini alijivunia Zaidi  Dema pengine kwa bidii yake..

Wakolosai 4:14 “Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu”.

Lakini mwisho wa siku anageuka na kuisaliti Imani, unadhani na sisi tusipoishindania Imani hatutaisaliti vivyo hivyo pale tunapoona mambo hayajaenda kama tunavyotaka?. Imani ya wokovu ni ya kuishindania kweli kweli haijalishi ni mazingira gani utapitia, kwasababu Bwana Yesu  alisema tangu kipindi cha Yohana mbatizaji hadi sasa ufalme wa mbinguni unapatikana kwa nguvu, na wenye nguvu ndio wanaouteka (Mathayo 11:12).

Utajiuliza ni kwanini Bwana Yesu alisema tangu kipindi cha Yohana mbatizaji na sio tangu kipindi cha akina Musa au Eliya, au Daudi?..Alisema vile kufuatana na maisha ya Yohana mbatizaji, jinsi alivyojikana nafsi kumtafuta Mungu, mtu ambaye hakujali mazingira aliyopo, hakujali nguo alizovaa, hakujali chakula alichokula, kule jangwani maadamu yupo sawa na Mungu wake, hiyo ilitosha.. Sasa kama yeye aliushindania hivyo, hata sisi hatuna budi kuishindania vivyo hivyo kama yeye, kulingana na maneno ya Yesu.

Mpaka mtume Paulo anakaribia kwenda kufa, na kusema IMANI NIMEILINDA, usidhani ilikuwa ni jambo jepesi jepesi, alipitia tabu zote lakini hakuukana au kuusaliti wokovu wake.

Itakuwa ni ajabu sana kama utataka kwanza uoelewe au upate kazi nzuri, au upate pesa ndio usimame katika wokovu, kwa namna hiyo kamwe hutakaa uustahimili wokovu, kwasababu hata kama Mungu akikupa hayo yote, kukitokea mtikisiko kidogo tu, utarudi nyuma kuuacha wokovu kama Dema.

Hivyo mapambano ya Imani yapo. Shikilia sana wokovu wako bila kuangalia au kujali mazingira, maana hiyo ndio tiketi yako ya kwenda mbinguni. siku hizi ni za mwisho. Maisha ni mafupi sana.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

TUMEKUWA TAMASHA KWA DUNIA; KWA MALAIKA NA WANADAMU.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments