Nini tofauti kati ya Kipawa na Karama?

by Admin | 16 November 2022 08:46 am11

Jibu: Ili tuelewe vizuri tofauti ya haya maneno mawili “kipawa na karama” hebu tuutafakari mfano ufuatao;

Watu wawili wamepewa zawadi ya magari ya kutembelea, tena yanayofanana, kila mmoja la kwake.. Ila wa kwanza akalitumia lile gari kwa faida yake yeye, yaani kumrahisishia usafiri, na kwa matumize yake binafsi…..na wa pili akalichukua lile gari alilopewa na kwenda kulifanya kuwa gari la kuwasaidia wagonjwa mahospitalini (ambulance) tena bure…

Sasa kibiblia Magari waliyopewa hawa watu wawili ndiyo yanayofananishwa na  VIPAWA vya Mungu,  lakini huyo wa pili aliyelifanya gari lake kuwa gari la huduma (msaada kwa wengine), gari lake hilo ndilo linalofananishwa na KARAMA, kwasababu alilitoa kwaajili ya kuwasaidia wengine na si kwa faida yake yeye… Yeye alikuwa radhi atembee kwa miguu, lakini si wagonjwa wasifie nyumbani kwa kukosa usafiri wa haraka kufika katika vituo vya huduma..

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Kipawa ni zawadi ya kipekee kwa Mtu anayopewa na Mungu , lakini karama imeenda mbali zaidi;ni zawadi ya kipekee kwa Mtu kutoka kwa Mungu yenye lengo la kuwasaidia wengine (kuwanufaisha wengine).

Kwamaana hata asili ya neno lenyewe karama ni “kukirimu” na kukirimu maana yake ni kusaidia..na mtu anayekirimu ndio anaitwa Mkarimu.

Na leo hii kuna watu wengi wenye vipawa makanisani lakini hawana karama!… Wengi leo wana vipawa vya kuimba lakini hawana karama ya kuimba…

Wana vipawa vya kunena kwa lugha lakini hawana karama ya kunena, wana vipawa vya kutabiri lakini hawana karama za kutabiri..

kwasababu gani?…Ni kwasababu vile vipawa wanavitumia kwa faida zao wenyewe na si kwa faida ya mwili wa Kristo…wanavitumia kwaajili ya umaarufu wao na kwa matumbo yao, na si kwaajili ya kuujenga mwili wa Kristo.

1 Wakorintho 14:12 ”Vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa”.

Hapo anasema “ili kulijenga kanisa”, na si kwaajili yetu…

Jitazame!..Je kipawa ulichonacho ni kwa kukunufaisha wewe au wengine?..

Je kipawa ulichonacho cha kuimba, kufundisha au kuhubiri au kuimba au unabii.. je kinafanya kazi ya kuujenga mwili wa Kristo au kujenga umaarufu wako na kujaza tumbo lako?..na kujiongezea utukufu?.

Kama kipawa chako kinakunufaisha wewe zaidi ya wengine, kama hakilitukuzi jina la Yesu, bali kinakutukuza wewe zaidi….basi tambua ya kuwa bado hauna Karama yoyote!…haijalishi unafanya miujiza kiasi gani, haijalishi unajua kuimba kiasi gani au unasifiwa na watu wote duniani..bado huna karama ya Roho.

Kifanye kipawa chako kuwa Karama!!.

Na madhara ya kutokuwa na karama yoyote maana yake hutakuwepo “karamuni” siku ile!!…Kwasababu watakaoalikwa katika karamu ya Mwanakondoo ni wale waliokuwa na karama na walizitumia vizuri kwa manufaa ya mwili wa Kristo…Kwasababu hata mzizi wa neno hilo karamu ni “karama”.

Je unataka karama za Rohoni basi Kifanye kipawa chako kuwa baraka kwa wengine..

1 Wakorintho 12:4 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.

5 Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.

6 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

7 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho KWA KUFAIDIANA”.

Nataka tuutazame huo mstari wa mwisho unaosema “KWA KUFAIDIANA”.

Hapo mwisho anasema “kwa kufaidiana”

Siku zote kuwa mtu mwenye Nia ya kuujenga mwili wa Kristo, kuwa na nia ya kuwasaidia wengine pasipo kutegemea faida wala malipo!..na Kipawa chako Bwana atakigeuza kuwa KARAMA.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

USINIE MAKUU.

KUOTA UNAENDESHA GARI.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/16/nini-tofauti-kati-ya-kipawa-na-karama/