Biblia inasemaje kuhusu Nywele?

by Admin | 1 December 2022 08:46 am12

Biblia imetoa maelekezo kuhusu Nywele kwa jinsia zote mbili (Ya kike na Kiume).

JINSIA YA KIUME:

Biblia inasema Mwanaume hapaswi kuwa na Nywele ndefu.. kwasababu kichwa chake yeye ni Utukufu wa Mungu..

1Wakorintho 11:3 “Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu

Hivyo kwa Mwanaume kuziweka Nywele zake kuwa ndefu ni aibu kwake na ni kukiaibisha Kichwa chake hicho ambacho ni  Kristo.

Tusome..

1Wakorintho 11:14  “Je! Hayo maumbile yenyewe hayawafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake?”

Na sio tu hatakiwi kuwa na Nywele ndefu, bali hata “Kufunika kichwa” awapo ibadani, maana yake ni kwamba  mwanaume anapokuwa ibadani hapaswi kuvaa kofia, au kuweka kitu chochote kichwani kinachoashiria kufunikwa kwa kichwa chake (maana yake kichwa chake siku zote kinapaswa kiwe wazi).

Na vile vile Mwanaume hapaswi kusuka Nywele, wala kuweka mitindo mitindo kichwani kwasababu kichwa chake ni utukufu wa Mungu.

JINSIA YA KIKE:

Katika jinsia ya Kiume tumesoma kuwa ni aibu kwa mwanaume kufunika kichwa, lakini tukirudi katika jinsia ya kike ni kinyume chake. Kwamba ni Aibu mwanamke kuwa na Nywele fupi na ni FAHARI MWANAMKE KUWA NA NYWELE NDEFU.

1Wakorintho 11:15 “Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi”.

Wanawake wote ni sharti waache nywele zao ziwe ndefu kulingana na biblia, kuzikata Nywele au kuzifanya fupi, pasipo sababu yoyote ya msingi kama vile magonjwa, au udhaifu wa mwili, ni kwenda kinyume na maagizo ya Mungu.

Ndio maana Upara (Ulaza) huwa hauwapati wanawake, bali wanaume tu!!..Hiyo ni kuonyesha kuwa wanawake wamekusudiwa kuwa na Nywele vichwani mwao wakati wote wa maisha yao, na wanaume ni kinyume chake.

Na zaidi sana biblia inazidi kuelekeza kuwa hata kama Mwanamke atakata nywele zake kutokana na matatizo Fulani Fulani, labda magonjwa au kutokana udhaifu wa nywele kukatika zenyewe basi hapaswi kutembea nje akiwa na nywele zake hizo fupi, bali anapaswa afunike kichwa chake kwa kitambaa au kwa kitu chochote kile.

1Wakorintho 11:6  “Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe.

7  Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume”.

Na mwanamke anapokuwa ibadani awe na nywele ndefu au fupi, ni Agizo la Bwana kwamba afunike kichwa chake, kwasababu kuu 2

Sababu ya Kwanza ni ili asikiabishe kichwa chake ambacho ni MWANAUME. Na sababu ya pili ni kwaajili ya MALAIKA. Tunapokuwa ibadani Malaika wa Bwana wanahudumu pamoja na watakatifu. Malaika hawa Bwana aliowaweka kwaajili yetu wana uhusiano mkubwa sana sisi katika kutuhudumia Soma Mathayo 18:10.

Kwahiyo tunapokuwepo katika ibada na ndani yake kukawa kunafanyika mambo ambayo ni kinyume na Neno la Mungu, malaika hawa wanaondoka, na hivyo kufanya ibada kupoa na utukufu wa Mungu kupungua.

Na pia Wanawake hawapaswi kusuka nywele zao, au kuvaa wigi, au kuzibadilisha maumbile nywele zao aidha kwa kuziweka kemikali, au dawa za kuzifanya zilale, Biblia haijawapa maagizo ya kuzifanya nywele zilale au zing’ae au ziwe kama za jamii ya watu Fulani, Hapana!.. imesema “ZIWE NDEFU!!” Basii!!..

1Timotheo 2:9  “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10  bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.

11  Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)

Je kuchonga Nywele na Ndevu ni dhambi?

MSHAHARA WA DHAMBI:

FUVU LA KICHWA.

NGUVU YA MNADHIRI WA BWANA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/12/01/biblia-inasemaje-kuhusu-nywele/