NGUVU YA MNADHIRI WA BWANA.

NGUVU YA MNADHIRI WA BWANA.

Jina la Mwokozi wetu Yesu, libarikiwe.

Mnadhiri ni mtu aliyejitenga na mambo fulani ili atimize nadhiri/Ahadi aliyoiweka kwa Mungu wake. Kwamfano katika agano la kale, kama mtu ameweka nadhiri fulani kwa Mungu, labda  ya kumtolea sadaka Fulani, na akatamka kwa kinywa chake mwenyewe mbele za Mungu, basi yalikuwepo maagizo Fulani ya kufanya ambayo yanaambatana na nadhiri hiyo aliyoiweka ili asije akaisahau nadhiri hiyo aliyoiweka.

Na agizo la kwanza kwa mtu aliyeweka nadhiri, ni kwamba hakupaswa kabisa kunywa divai wala kilevi cha aina yoyote ile.

Hesabu 6: 1 “Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa Bwana;

3 atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi wala zilizokauka.

 4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda”.

Na kwanini Mungu akataze mtu asinywe kileo chochote, wakati wa nadhiri yake? . Ni kwasababu kileo kinamtoa mtu ufahamu, na kumfanya ajisahau, hata ajikute anazungumza maneno au anafanya vitendo ambavyo ni kinyume na ile nadhiri aliyomwekea Mungu, hivyo ikawa dhambi kubwa kwake. Maana yake ni kwamba mtu aliyemwekea Mungu nadhiri ni lazima awe katika akili yake timamu wakati wote, hapaswi hata dakika moja kujitoa nje ya ufahamu wake kwa kileo, au kwa kitu kingine chochote.

2. Sheria ya Mnadhiri (yaani mtu aliyeweka nadhiri) ilikuwa ni lazima, aziache nywele zake ziwe ndefu, (Hapaswi kuzikata kabisa).

Hesabu 6: 5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani mwake zikue ziwe ndefu”.

Siku zote nywele ni ishara ya uwepo wa Mungu juu yetu. Na nywele huwa ni nyingi kichwani, na zina tabia ya kukua, kila siku zinaongezeka kimo, Ndivyo rehema na Neema za Mungu zilivyo nyingi juu yetu, zinaongezeka kila kukicha.

Maombolezo 3: 22 “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.

23 Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu”

Kwahiyo mnadhiri yeyote, ambaye alikuwa amemwekea Mungu nadhiri, hakukata nywele zake, mpaka siku ambayo atatimiza nadhiri hiyo ndipo ataruhusiwa kuzikata. (Matendo 18:18, matendo 21:23).

Sasa kama ukiendelea kusoma zaidi juu ya sheria hizo za mnadhiri, utaona kuwa pia mnadhiri yeyote pamoja na kutokukata nywele zake na kunywa kileo, alipaswa pia siku zote ajitenge na kila aina ya unajisi, maana yake alipaswa ajiweke katika hali ya utakatifu. Na kama akishindwa kutimiza vigezo hivyo nadhiri yake hiyo inakuwa ni batili na ni dhambi kwake.

Lakini pia kulikuwa na Baraka za kipekee kwa mtu aliyemwekea Mungu nadhiri, kipindi chote wakati yupo katika hiyo nadhiri na hata baada ya kuimaliza hiyo nadhiri. Na baraka hiyo ya kipekee ilikuwa ni kutembea na nguvu za Mungu, kwa namna isiyokuwa ya kawaida..Na nguvu hiyo kazi yake ni kumweka mtu mbali na maadui wa kiroho.

Sasa leo kwa msaada wa Bwana tutajifunza mtu mmoja katika maandiko, ambaye alikaa katika nadhiri za Mungu, na kuzifurahia nguvu za Mungu, mpaka siku alipojisahau na kutoka nje ya nadhiri na kupata madhara, na kupitia mtu huyo tutajua umuhimu wa kukaa katika nadhiri kwa Mungu wetu tulizomwekea.

Na mtu huyo ambaye tutajifunza habari zake  si mwingine zaidi ya Samsoni.

Biblia inasema Samsoni alikuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake.  Mungu mwenyewe ndiye aliyemfanya awe mnadhiri wake.

Na kama sheria ya Mnadhiri wa Mungu inavyosema, hakupaswa anywe divai, wala kileo kingine chochote, hivyo Samsoni hakunywa kileo chochote tangu akiwa tumboni mwa mama yake, ndio maana Mungu alimwambia mama yake asinywe divai wakati wa uja uzito wake, kadhalika kama mnadhiri wa Mungu hakupaswa kukatwa nywele zake, kulingana na maagizo Mungu aliyotoa katika torati kumhusu mnadhiri..

Waamuzi 13:3 “Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume.

4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;

5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti”.

Umeona hapo?..ni kwanini Samsoni nywele zake hazikupaswa kukatwa.? Si kwasababu alikuwa ni mtu maalumu sana, bali ni kwasababu tayari alikuwa ni Mnadhiri, na sheria ya mnadhiri tangu wakati wa Musa ni kutokukata nywele, wala kunywa divai. Hivyo Samsoni hakupaswa kukata nywele zake wala kunywa kileo chochote maisha yake yote, ili nadhiri yake iwe na maana.

Sasa imezoeleka kufahamika kwamba, Samsoni nguvu zake zilikuwa katika nywele tu!..Lakini kiuhalisia ni kwamba hazikuwa katika nywele zake tu, bali hata katika kitu alichokuwa anakunywa… Ndio maana alionywa asinywe kileo chochote tangu akiwa tumboni…

Maana yake ni kwamba hata kama Delila asingejua siri ya nywele zake, lakini akajua siri ya kutokunywa kwake kileo, na hivyo akaenda kumtengenezea kileo na kumpa, bado nguvu za Samsoni  zingeisha mpaka atakapolevuka na kurudia akili yake, Kwasababu siri za nguvu za Samsoni, zilikuwa katika Neno la Mungu, ambalo linatoa maagizo juu ya mnadhiri, na neno hilo Mungu alilizungumza tangu wakati wa Torati ya Musa…

Hesabu 6: 1 “Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa Bwana;

3 atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi wala zilizokauka.

 4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda

5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani mwake zikue ziwe ndefu”.

Kwahiyo kama mtu yupo katikati ya nadhiri halafu akakata nywele zake, anakuwa kashaharibu kila kitu…kadhalika kama yupo katikati ya nadhiri halafu akalewa na kilevi cha aina yoyote ile,  vile vile anakuwa kashaharibu kila kitu.. Kwahiyo Samsoni akiwa bado yupo katika nadhiri yake ambayo hiyo ilikuwa ni ya maisha, nywele zake  zilikatwa…na hivyo akawa amejiharibia mwenyewe.

Hiyo ilikuwa ni agano la kale, kwamba mtu akiweka nadhiri ni lazima aziache nywele zake zikue… na mtu akivunja maagizo hayo ya torati anakuwa amejiharibia mwenyewe.

Hali kadhali katika agano jipya, tunazo nadhiri; Zipo nadhiri ambazo sisi wenyewe tunaziweka…kwamfano zile za kuahidi kufanya jambo Fulani kwa Mungu, lakini zipo nadhiri ambazo sisi hatuamui kuziweka, bali Mungu mwenyewe ndiye anayeziweka katika maisha yetu, kama vile Samsoni.

 Samsoni hakumwekea Mungu nadhiri kwa kuamua yeye, isipokuwa Mungu mwenyewe ndiye aliyemwekea ile nadhiri tangu akiwa tumboni mwa mama yake,  yeye alijikuta tu tayari kazaliwa na ile nadhiri. Vivyo hivyo pia mtu anayezaliwa mara ya pili katika roho, tayari anakuwa na nadhiri ya Maisha,  ambayo hiyo ni Mungu anaiweka katika maisha yake, na inamfunga aishi katika sheria za Mungu, na wakati wote na ni lazima aishi kulingana na Neno la Mungu ili nguvu zake za rohoni zisipotee, wakati wote anapoishi hapa duniani.. Lakini kama akitoka nje ya neno la Mungu, na kuruhusu  adui shetani yake akate nywele zake za rohoni, kama alivyofanya kwa samsoni, atakuwa amejiweka katika hali ya hatari sana, ni heri hata asingezaliwa mara ya pili.

Sasa ifuatayo ni milango ambayo shetani anaitumia kuzikata nywele zetu za rohoni, na kututoa katika unadhiri mtakatifu.

1.Uzinzi na uasherati.

Unapofanya uzinzi au uasherati baada ya kuzaliwa mara ya pili,  au unapojihusisha na mahusiano yoyote ya kipepo, hapo tayari unakuwa umejiuza kwa shetani moja kwa moja.. Na hicho ndicho kilichomwangusha pia Samsoni…Biblia inasema katika Mithali 31:3 “Usiwape wanawake nguvu zako;…”.  Na inasema pia..

1Wakorintho 6:18  “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”.

Hapo inasema, ikimbieni sio ikemeeni…

Siku hizi ni fashion kila kijana kuwa na girlfriend, na binti kuwa na boyfriend, tena hayo yanafanyika kanisani, na kila mtu anajua..halafu huyo huyo analalamika siku hizi nguvu za kusali zimeisha, anasumbuliwa na mapepo, anaota ndoto mbaya, akisoma neno dakika mbili anasikia usingizi, anashindwa kujizuia kutenda dhambi, mambo yake hayaendi sawa n.k..Sasa hizo nguvu zitatoka wapi wakati tayari umeshampa shetani?…tayari shetani kashakata nywele zako, kwa uasherati wako huo, hiyo nguvu ya kuomba utatolea wapi?, hiyo nguvu ya kusoma neno utatolea wapi, hiyo nguvu ya kwenda kuhubiri utatolea wapi, hiyo nguvu ya kufunga utatolea wapi?, utakemea pepo gani litoke?..kwaufupi katika roho, shetani ameshakupofusha macho na anakusagisha ngano katika gereza lake kama alivyomfanya Samsoni. (Waamuzi 16:21).

2.Ibada za sanamu.

Huu ni mlango wa pili, shetani anaoutumia kututoa katika unadhiri mtakatifu. Kumbuka siku zote pale tunapozaliwa mara ya pili, hatupaswi kumwambudu mtu yeyote wala kitu chochote. Tunapomfanya mtu Fulani, achukue nafasi ya Mungu, au kitu Fulani tulichokitengeneza kwa mikono yetu kichukue nafasi ya Mungu..tayari tumemfungulia shetani mlango wa kutuondoa kwenye unadhiri wetu mtakatifu.

Na mambo mengine yote yaliyosalia yaliyo kinyume na Neno la Mungu, ni mlango wa adui kututoa kwenye unadhiri mtakatifu.

Sasa inawezekanana tayari shetani kashakutoa katika  unadhiri wako, ambao Bwana alikuwekea tangu siku ile ulipozaliwa mara ya pili, ndio maana ulikuwa unanguvu nyingi za rohoni, kuangusha ngome na mamlaka kwa jina la Yesu, hata adui akuzingire kiasi gani, hakukuweza, kama vile Samsoni, ulikuwa una nguvu za kusali na kusoma Neno, na kushinda dhambi.. Lakini ulimfungulia shetani mlango mahali Fulani na akaziondoa nguvu zako, na mpaka sasa huwezi tena kufanya yale uliyokuwa unafanya mwanzo.

Suluhisho ni moja, ni kuanguka chini na kujinyenyekeza kwa Mungu, kwa kutubu kama Samsoni alivyofanya, na kuachana na mambo yote yaliyo kinyume na Neno la Mungu, kama ulikuwa unaishi maisha ya uasherati unayaacha kwa vitendo, ikiwemo kukata mawasiliano na hao uliokuwa unafanya nao uashetari, kama ulikuwa unaabudu sanamu, unaacha na kutubu, kama udanganyifu wa mali ulikuwa umekushika, unapunguza muda wa kufanya shughuli na kuongeza muda wa kumtafuta Mungu n.k. Kama ukifanya hayo Mungu ni wa rehema, kama alivyomrehemu Samsoni, na kumrejeshea tena nguvu zake. Na wewe utarudia katika hali yako ya unadhiri mtakatifu,kama ule wakati ambapo majeshi ya adui yalikuwa hayawezi kusimama mbele yako.

Lakini kama bado unaupenda ulimwengu, fahamu kuwa upo gereza na macho yako yamepofushwa, na kama bado hujampokea Yesu kabisa maishani mwako, ni vyema ukampokea leo, maadamu anapatikana, itafika wakati utatamani siku moja ya mwana wa Adamu katika maisha yako usiione, kama ukiipuuzia sauti yake inayokuita leo.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NADHIRI.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?

Fadhili ni nini? Nini maana ya “fadhili zake ni za milele” kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Rowland Asante Robert
Rowland Asante Robert
2 years ago

Am blessed!

Mathew Msaka
Mathew Msaka
2 years ago

Asante kwa jumbe nzuri za kutujenga kiimani. Mbarikiwe sana.