Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?

Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?

SWALI: Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yefhta, ya kumtoa binti yake kafara? Je Mungu anakubali sadaka za kuteketeza watu?


JIBU: Kabla ya kwenda kwa Yeftha turudi kwanza kwa Ibrahimu…swali ni je! Kwanini Mungu amwambie Ibrahimu akamtoe mwanawe kama sadaka ya kuteketezwa?..Je Mungu anaziridhia sadaka za kuchinja watu na kutoa kafara?..Kwanini asingemwambia akamtoe mbuzi tu na si mwanae? Ni muhimu kufahamu nyakati na majira Mungu aliyokuwa anatembea na watu wake…Zamani sana kabla Taifa la Israeli halijazaliwa…Kulikuwa hakuna mfumo maalumu wa kumwabudu Mungu…wengi walikuwa hawajui mapenzi kamili ya Mungu..Sheria ilivyokuja ndipo angalau watu wakaanza kumwelewa Mungu anataka nini.. Hivyo kabla ya Torati watu walikuwa hawaelewi kwa mapana Mungu anataka nini na hataki nini, au anapendezwa na nini na hapendezwi na nini…

Hivyo watu pia walikuwa wanatoa sadaka za kuteketeza watu (Au kuwapitisha watu kwenye moto) wakidhani wanampendeza Mungu…hali kadhalika watu walikuwa wanajitoa hata wao wenyewe wachomwe moto kama sadaka ya kuteketezwa wakijua wanampendeza Mungu… Hivyo hata wakati wa Ibrahimu, sadaka za watu kujitoa kuteketezwa zilikuwa zinaendelea…Na hivyo hata Ibrahimu alikuwa anajua ni sawa chochote kile Mtu anaweza kukitoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu wake…

Kwasababu sheria bado ilikuwa haijaja!..Kwasababu sheria/Torati ndio ilikuwa kuwafumbua watu macho kuelewa mambo gani Mungu hayapendi na yapi anayapenda.

Warumi 7:7 “Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani”.

Na Mungu aliutumia huo huo mfumo wao wa kuteketeza watu kumjaribu Ibrahimu…Ili kupitia huo amwonyeshe kuwa yeye haridhii sadaka za kuteketezwa watu..Ndio maana unaona alimwambia Ibrahimu akamtoe mwanawe kama sadaka ya kuteketezwa…na alipokuwa anaenda hata kabla ya kumchinja mwanawe Mungu alimzuia akamwonyesha mwanakondoo pembeni…akimfundisha kuwa Sadaka za kuwachinja wanadamu kama wanyama na kuwateketeza kwenye moto hazikubali na wala hazimfurahishi….bali sadaka za wanyama ndizo anazozikubali..ndio maana hakumruhusu amchinje mwanawe badala yake alimtumia mwanakondoo ambaye alitokea pale pale alipokuwepo…

Angekuwa anapendezwa na sadaka za watu asingemzuia Ibrahimu kumchinja mwanawe. Hivyo hiyo ikawa somo kwa Ibrahimu na wanawe kutojaribu kutoa sadaka za kuteketezwa watu..kwani Mungu hazikubali hizo hata kidogo. Na ilipofika wakati wa Sheria Mungu alitoa amri kwamba watu wasiwatoe wana wao kama sadaka ni machukizo na ni dhambi..Kasome Walawi 20:1-5,

Yeremia 7:30 “Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema Bwana; wameweka machukizo yao ndani ya nyumba hiyo, iitwayo kwa jina langu, hata kuitia unajisi.

31 Nao wamepajenga mahali palipoinuka pa Tofethi, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ILI KUWATEKETEZA WANA WAO NA BINTI ZAO MOTONI; jambo ambalo mimi sikuliagiza, wala halikuingia moyoni mwangu”.

Soma tena..

Yeremia 19:4 “Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia;

5 nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu;”

Na mwisho..

Yeremia 32:33 “Tena wamenigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao; ingawa naliwafundisha, niliondoka mapema na kuwafundisha, lakini hawakusikiliza ili wapate mafundisho.

34 Bali waliweka machukizo yao ndani ya nyumba iliyoitwa kwa jina langu, ili kuinajisi.

35 Tena walijenga mahali palipoinuka kwa Baali, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ILI KUWAPITISHA WANA WAO NA BINTI ZAO KATIKA MOTO KWA AJILI YA MOLEKI, JAMBO NISILOWAAGIZA; WALA HALIKUINGIA MOYONI MWANGU KWAMBA WALITENDE CHUKIZO HILO; wapate kumkosesha Yuda”.

Mistari yote hiyo Bwana anasema tendo la kuteketeza watu kwenye moto hata halikumwingia moyoni mwake kabisa..Ni machukizo kufanya vile….Ndio maana hata Mungu alimzuia Ibrahimu. Sasa pamoja na kuwepo kwa sheria hizo..Bado wana wa Israeli walikuwa wanaendelea kufanya hizo sadaka..kama Bwana anavyosema hapo juu…Sasa tukirudi kwenye Biblia ndio tunamkuta Mtu ambaye anaitwa Yeftha ambaye alizaliwa baada ya sheria hiyo kuwekwa..

Huyu Yeftha alikuwa ni Mwamuzi wa Israeli ambaye alichaguliwa na Mungu kabisa…habari zake unaweza ukazisoma kwenye kitabu cha Waamuzi, historia ya maisha yake…Lakini kuna kipindi alitaka kwenda vitani kupigana na maadui zake ambao walikuwa ni maadui pia wa Taifa zima la Israeli..mtu huyu akamwekea Mungu nadhiri…pasipo kufikiri, akamwahidi Mungu endapo akipata ushindi chochote kitakachokuja mbele yake kumlaki atakitoa kuwa sadaka ya kuteketezwa..Bila kufikiri kuwa anaweza kuja hata ndugu yake au mwanawe…na aliposhinda akaja binti yake aliyemzaa kumlaki. Na kwasababu ameshaweka nadhiri ni lazima aitimize…hivyo akampitisha mwanawe kwenye moto…

Waamuzi 11:30 “Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,

31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa”.

Sasa utauliza Yeftha alifanya dhambi kumpitisha mwanawe motoni?..Jibu ni ndio kwasababu alikwenda kinyume na Torati ya Mungu…iliyosema “msiwatoe wana wenu kuwapitisha motoni”…

Na utauliza pia je! Asingemtoa mwanawe pia angekuwa amefanya dhambi?..Jibu ni ndio angekuwa amefanya dhambi kwasababu amemwekea Mungu nadhiri ya upumbavu ambayo ameshindwa kuitoa…

Hivyo aidha angeitoa au asingeitoa bado Yeftha alikuwa hatiani?……Ingawa Yeftha alikuwa anamambo mengi ya kujifunza kutoka kwake lakini kwa hilo lilimtia doa kama lile la mke Uria lilivyomtia doa Daudi. Na ndio maana Yeftha hakutawala muda mrefu Israeli..alitawala miaka 6 tu wakati wengine walikuwa waamuzi wa Israeli hata kwa miaka 40..yeye alikaa miaka sita tu akafa..na ndiye mwamuzi aliyetawala muda mfupi kuliko wote.. Lakini yote hayo Mungu aliyaruhusu ili sisi tujifunze kwamba tusiweke nadhiri za upumbavu..Tujihadhari na nadhiri tunazoziweka…Nadhiri tuiwekeayo tuahakikishe inakubalika na Neno la Mungu na tumeifikira kwanza kabla ya kuiweka ili tusije tukajikuta tumejiweka katika mtego…(hali kadhalika tukio lile la Yeftha pia limebeba siri nyingine juu ya Yesu Kristo). Bwana akubariki. 

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Jehanamu ni nini?

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.

SADAKA YA MALIMBUKO.

JE UNAMTHAMINI BWANA?

JE KUCHOMA MAITI NI DHAMBI?

KIFO CHA MTAKATIFU POLIKAPI (Policarp).

SAKRAMENTI NI NINI, NA JE! IPO KATIKA MAANDIKO?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Justin kadakala
Justin kadakala
8 months ago

Asante Sana kwa mafundisho haya, lakini nimejikuta Nina swali hapa.
* Sasa kwenu ninyi, ki biblia mungeweza mushauri yeftha jambo gani sahihi lakufanyo kipindi kile!?

Asante kwa jibu, sababu ni fundisho piya n’a kwangu mimi.