Karismatiki ni nini?

by Admin | 23 December 2022 08:46 am12

karismatiki maana yake nini?

Karismatiki ni neno la kiyunani lenye maana ya “Zawadi za neema”.. Au kwa lugha nyepesi zaidi, tunaweza kusema, “vipawa vya neema”. Ambavyo hivyo hutolewa na Roho Mtakatifu mwenyewe na sio mwanadamu. Neno hili utalisikia sana vinywani vya madhahebu mbalimbali ya kikristo.

Ni mkondo ambao ulianza, mwanzoni mwa karne ya ishirini, (1906), kule Azusa Marekani, wakati ambapo dhehebu la Pentekoste lilipoanza. Lililoamini kuwa uthibitisho wa Mungu kuwepo katikati ya watu basi ni kuonekana kwa zile karama za Roho Mtakatifu, ambazo zinazungumziwa katika kitabu cha 1Wakorintho 12.

Kwamba kanisa ili liwe hai, ni sharti vipawa vya Roho kama vile Kunena kwa lugha, kutoa unabii, uponyaji na miujiza, vidhihirike ndani yake. Ikumbukwe kuwa tangu kanisa la kwanza la mitume kupita, vipawa hivi vilionekana kama vimekufa, havipo tena, lakini, viliibuliwa tena na Roho Mtakatifu mwanzoni mwa hiyo karne ya ishirini, ambapo baadhi ya wakristo walikaa chini na kufunga na kumwomba Mungu ajifunue kwa namna hiyo kama ilivyokuwa katika kanisa la kwanza la mitume. Na kweli wakiwa katika maombi hayo, Roho Mtakatifu alishuka, watu wengi wakaanza kunena kwa lugha, na karama mbalimbali kuonekana.

Ni jambo ambalo lilikuwa  gheni, kwa madhehebu mengi makongwe, ambayo yalikuwa tayari yameshajikita katika mifumo ya kidini kwa muda mrefu. Kama vile Katoliki, Lutheran, Angalican, Moravian n.k.

Hivyo basi mvuto  wa vipawa hivi, ulivyoendelea kuwa mkubwa, mpaka kufikia miaka ya 1980, madhehebu mengine mengi yakaanza kurithi mfumo huu wa karismatiki, ikiwemo dhehebu kama Katoliki, ( wakaitwa Karismatiki Katoliki), mengine ni Lutheran, na Anglikana, n.k. ijapokuwa yamekuwa na upishano kati ya wao kwa wao katika mifumo ya imani hii .

Hivyo kwa ufupi tunaweza kusema kanisa lolote linalosisitiza udhihirisho wa vipawa/karama za Roho, kama vile uponyaji, unabii, kunena kwa lugha, huitwa Kanisa la Karismatiki.

Ni nini tunapaswa tufahamu kuhusu vipawa vya Roho(Karismatiki).

Ni kweli kanisa linalokosa vipawa hivi, ni kanisa lililo nusu-mfu, au mfu kabisa. Kwasababu Mungu sio sanamu, ambaye anapokea tu ibada, lakini hatoi vipawa/zawadi kwa watu wake. Hayupo hivyo. Lakini pia ukengeufu mkubwa umeingia na kuvichafua vipawa vya Mungu, ikiwa na maana, kuwa mkristo usipokuwa makini utajikuta unapokea Roho nyingine na sio Yule wa Mungu.

Ni kuwa makini katika siku hizi za mwisho, wimbi kubwa la manabii wa uongo, linazukia huku, mafunuo yasiyo ya ki-Mungu yanaibuka na kuwapoteza watu kutoka huku, matumizi ya visaidizi kama maji, na chumvi za upako, vimewapoteza wengi,..Hivyo kumetokea mvurugano mkubwa sana. Mtu atanena kwa lugha leo, kesho atakwenda kuzini, jiulize ni roho gani ameipokea huyo?

Ni nini tunapaswa tufanye?

Nyakati hizi za mwisho, Tujitahidi sana kuitegemea  BIBLIA kwa kila kitu tunachokitenda, au tunachoongozwa kukifanya, Ikiwa ni karama hakikisha haikinzani na kanuni za msingi za Neno la Mungu, hiyo ndio njia pekee ya kuthibitisha kuwa kipawa hicho ni cha ki-Mungu. Lakini nje ya hapo utapotea. Ikiwa utapokea ufunuo, au unabii, usiupokee tu, ilimradi ni fulani kasema, kisa kaona maono, hakikisha kwanza katika biblia, Je! Ndivyo ilivyo? Au La!. Kwasababu  shetani ameingilia sana mikusanyiko mingi, ajaribu kuiangusha kwa namna hii.

Haiwezekani,  useme mimi nimepokea Roho Mtakatifu, ninanena kwa lugha, ninaimba kwa Roho,  Halafu  anakuacha uendelee kuabudu sanamu la mtakatifu Fulani,sanamu la Mariamu au uombe sala za wafu. Huyu sio Roho Mtakatifu, haijalishi atajiita ni Karismatiki namna gani.

Hivyo ni kuwa makini, tusije pokea roho nyingine isiyokuwa ya Mungu. Hizi ni zama za uovu.

1Yohana 4:1  “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani”

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Au jiunge na makundi yetu ya mafundisho ya kila siku kwa kwa njia ya Whatsapp kwa kubofya hapa >>>> WHATSAPP GROUP

Mada Nyinginezo:

Nini tofauti kati ya Kipawa na Karama?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

HATA ILIPOTIMIA SIKU YA PENTEKOSTE.

SEMA KWA LUGHA NYINGINE.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/12/23/karismatiki-ni-nini/